MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amewataka wanaosema kuwa hataweza kuleta mabadiliko kwa kuwa yuko ndani ya mfumo wa chama hicho, wakajifunze China.
Akizungumza katika mikutano aliyofanya Mbeya vijijini jana, Dk Magufuli alisema China imefanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kiteknolojia na kijamii, kwa kutumia chama cha Kikomunisti chenye mfumo wa kijamaa kama CCM.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, walichofanya katika nchi hiyo ni kutumia watu wa ndani ya chama hicho cha Kikomunisti, kuleta mabadiliko yanayoonekana dunia nzima leo mpaka Marekani imeshangazwa.
âNchi ya China ilikuwa chini ya Chama cha Kikomunisti chini ya Mwenyekiti Mao, walipopata uzoefu wakafanya mabadiliko bila kuondoa chama kilichokuwepo madarakani,â alisema.
Dk Magufuli pia aliwaonya Watanzania kuwa uongozi wa nchi haujaribiwi na hata yeye alipochukua fomu za kuwania urais, alijua kuwa haombi urais kwa ajili ya majaribio, ndio maana alichukua fomu na kutafuta wadhamini kimya kimya, huku akimtanguliza Mungu mbele.
Aliwahadharisha Watanzania uwezekano wa kutokea watu watakaowapa fedha, ili wawachague na kuwataka wawaepuke kwa kuwa watakuwa na deni watakalotakiwa kulipa huko walikotoa fedha.
Alisema yeye deni lake ni kutumikia Watanzania wote bila kujali vyama vyao, lakini si deni la fedha kwa watu wenye fedha kwa kuwa hatoi fedha mahali popote ya kuomba kuchaguliwa.
Dk Magufuli alisema nchi zilizofanya majaribio ya uongozi, kwa kutumia nguvu kuondoa uongozi uliokuwepo madarakani, leo hii wananchi wake wanakumbuka viongozi waliowatoa baada ya kujikuta uongozi ulioingia kwa nguvu, kushindwa hata kulinda umoja wao, na sasa wanabaguana Waislamu kwa Waislamu na ni watu wa nchi moja.
âNitoe mfano wa Libya, Gadaffi alikuwa Rais na nchi ilikuwa na rasilimali ya mafuta ambayo akaitumia vizuri akafikia hatua kijana akioa, Serikali ilimpa fedha za mahari na nyumba ya kuishi, leo wamemtimua wanapigana na kuvurugana,â alisema Dk Magufuli na kuongeza kuwa haraka haraka haina baraka.
Mgombea huyo wa CCM, aliwataka Watanzania katika umoja wao bila kujali vyama, waungane kumchagua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili alete mabadiliko. Aliwataka wanaChadema wenye msemo wa Peoples Power, wampe yeye Power aondoe kero za Watanzania na kuleta mabadiliko.
Kwa wana CCM wenye msemo wa Kidumu Chama Cha Mapinduzi, aliwataka wampe alama ya dole, ili aongoze nchi na kuleta mabadiliko katika maisha ya kila Mtanzania.
Akizungumzia kero ndogondogo, Dk Magufuli alisisitiza kuwa Serikali atakayoiunda itahakikisha wafanyabiashara wadogo wanaheshimiwa na kutunzwa ili biashara zao zikue. Kwa mujibu wa Dk Magufuli, wafanyabiashara hao wakitunzwa na kuheshimiwa, biashara zao zitaongezeka na kuwa kubwa kwa kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha.
Dk Magufuli pia alitangaza kuanza kwa elimu ya msingi mpaka sekondari bure, ili wafanyabiashara na wakulima watumie fedha zao kufanya maendeleo mengine.
âNataka kuongoza nchi isiyo na kero kwa wanyonge,â alisema Dk Magufuli ambaye alisema yeye ni mtoto wa mkulima na anajua maisha ya watu wa chini.
Katika hatua nyingine, alionya watu wanaouza dawa za Serikali katika maduka binafsi na kuongeza kuwa, watu hao moto unawajia kwa kuwa hataki wananchi waandikiwe dawa hospitali, kisha watumwe kwenda kununua dawa katika maduka binafsi.
Alihoji hayo maduka yanakopata dawa ambako Serikali haiwezi na kuongeza kuwa anajua kuna mchezo mchafu wa kuuza dawa za umma hivyo wauzaji hao wasubirie moto wake.
Kuhusu atakapopata fedha za kutekeleza ahadi zake, alisema yeye amekuwa serikalini kwa miaka 20 anajua kuna wala rushwa na kuonya kuwa, walarushwa hao watarajie kupambana na yeye.
Pia aliahidi kutoa mikopo ya kila kijiji, ili kusaidia vijana, wanawake na wananchi wengine kwa ujumla, kuanzisha na kukuza biashara zao, huku akiwahakikishia kuwa hakutakuwa na manyanyaso kwao kwa kuwa anataka wajenge maisha yao.
Recent Comments