Miongoni mwa mambo magumu kabisa katika ufanikishaji wake ni mtu kuachana na uvutaji wa sigara. Watu wengi wamekuwa wakionywa kuachana na uvutaji wa sigara kwa sababu ya madhara yake, lakini wamekuwa wakishindwa kutokana na kukolewa na kiwango cha Nikotini inayopatikana katika tumbaku.
Vijana wengi wamekuwa wakijiingiza katika uvutaji kwa kufuata mkumbo, lakini baadaye wanapokuja kutambua kuwa wako katika hatari ya kuambukizwa au pengine wana ugonjwa wa kifua kikuu, wanakuwa katika wakati mgumu wa kuachana na uvutaji huo. Wengi wao wamekufa huku makundi kwa makundi wakitangatanga kutafuta suluhu ya kuchana na uvutaji, si tu kwa sababu ya kuhofia ugonjwa, bali hata kukosa uwezo wa kununua bidhaa hiyo.
Hata hivyo idadi kubwa ya wanaojaribu kuacha wamejikuta wakipata majibu ya kutoweza, kutokana na kusumbuliwa na hamu ya uvutaji, umbumbu wa mawazo pindi wanapokaa muda mrefu bila kuvuta, kuumwa na kichwa na hata udhaifu katika kukumbuka vitu au mambo waliyofanya au waliyopanga kuyatenda.
Pamoja na yote hayo watalaam na washauri wa masuala uvuaji wa sigara wanasema wanaopatwa na hayo wamekosa mbinu na muongozo wa kuwasaidia waachane na uvutaji wa sigara bila kupata madhara.
Kwa ufupi somo hili limehusisha uchunguzi wa kina pamoja na kumbukumbu za kitaalamu kutoka kwa washauri kama Anderson JE, Jorenby DE, Scott WJ, Fiore MC, Bailey WC, Cohen SJ, ambao wote kwa pamoja kupitia vituo vyao kikiwemo cha US Department of Health and Human Services na Public Health Service walishawahiwa kueleza mbinu salama za kuachana na uvuaji wa sigara.
Zifuatazo ni dondoo kadhaa za kufuata ili mvutaji aache sigara kwa usalama.
- Mvutaji lazima afahamu ni muda gani ambao huwa anavuta sigara kwa wingi, je ni wakati akiwa amelewa au akiwa na mawazo mengi ya kimaisha? Akishafahamu hilo ajiulize ni kiwango gani cha sigara ambacho huwa unavuta kwa siku?
- Baada ya hapo achukua kitabu chake cha kumbukumbu na aandike muda huo ambao yeye huvuta sigara kwa wingi. Ajiulize kwa nini huwa unavuta, atathimini madhara ya uvutaji wa sigara kwake binafsi na kwa familia yako.
- Kaa chini upitie kwa makini kumbukumbu zako za muda na kiwango cha sigara unazovuta kwa nyakati hizo, kisha panga utaratibu mpya. Kwa mfano kama unavuta sana wakati ukiwa kwenye mawazo hakikisha kuwa unapoanza kufikiria juu ya jambo fulani uwe na kitu mbadala kitachukua nafasi ya sigara. Mfano kahawa au chai? Hakikisha kila penye hamu ya uvutaji unaweka kitu kingine mbadala cha kufanya zaidi ya kuvuta sigara.
- Ondoa masalio ya sigara katika sehemu ambazo unaishi, fua nguo zote na vitambaa ili kuondoa harufu ya sigara katika eneo unalokuwepo. Usikae karibu na mtu anayevuta, usikubali kuwa mshirika wa mvutaji na usiwe mtu wa kuendekeza sana msukumo wa mwili unaotaka uvute, bali kila unapowaza juu ya kuvuta fikiria madhara na nia yako ya kuacha.
- Wafahamishe rafiki zako kuwa umeamua kuachana na uvutaji, ili upate watu wa kuwaonea aibu pale utakapoanguka na kurudia uvutaji wa sigara. Panga tarehe ya kuacha na iwe kwenye kumbukumbu.
- Wakati ukiiendea tarehe hiyo ya kuacha hakikisha unapunguza kiwango cha uvutaji kadiri unavyoisogea siku hiyo. Jipangie muda mrefu zaidi ya kuvuta kulingana na kiwango chako cha uvutaji na kuendelea kuuongeza kila siku ili uzoee kukaa saa nyingi bila kuvuta.
- Fuata ratiba mbadala uliyojiwekea kuziba pengo la uvutaji, kama umepanga kutumia kahawa kila unapokuwa mpweke sebuleni hakikisha unajizoeza ili ikifika tarehe yako ya kuacha usiwe mtu wa kujiuliza cha kufanya nyakati ambazo utakuwa na hamu ya sigara.
- Lengo lako liwe ni kufanikiwa na usikate tamaa utakaposhindwa kufanikisha lengo lako kwa wakati uliojipangia. Mara kwa mara nenda kamuone daktari mshauri ili akupe muongozo zaidi wa kukusaidia na ikiwezekana akupe nafasi ya kuwatembelea wagonjwa waliopata ugonjwa wa kifua kwa sababu ya kuvuta sigara.
Kwa kifupi hizo ni dondoo chache tu za kukusaidia kuachana na uvutaji wa sigara, lakini mara nyingi kinachoweka nguvu za kufanikisha uachaji wa sigara ni utashi wa mtu ambao hutokana na tathimin ya kina ya muhusika na mtazamo wake juu ya sababu za kuacha. Mara nyingi wanaoshindwa ni wale ambao hawakuzitia nguvu sababu za kuacha kwao.
Siku zote mwanadamu anaongozwa na utashi na kila mwenye kutaka hufanikiwa. Hii ina maana kuwa kama mwanadamu atasema hawezi kuacha kitu fulani, haina maana kama hawezi kwa sababu ameshindwa kujizuia bali ameamua kutokutaka na kinachomshinda ni matokeo ya  maamuzi yake. Kila anayetaka jambo hufanikiwa na hata wavutao sigara wanaweza kuacha kama wakitaka kufanya hivyo.
Recent Comments