Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) kimezindua kampeni ya michoro inayolenga kuzuia unyanyasaji wa kingono unaofanywa na walinda amani.
Maneno yanayosomeka “ngono na watoto ni uhalifu” yamezagaa kwenye picha zilizotolewa kwa ajili ya kampeni hiyo ya MONUSCO, moja ya vikosi vikubwa kabisa vya Umoja wa Mataifa vinavyolinda amani duniani.
Kampeni hiyo inakuja baada ya Katibu Mkuu Ban Ki-moon kumfukuza kazi mkuu wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) baada ya mkururo wa tuhuma za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto uliotendwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa walioko huko.
Kikosi cha kulinda amani nchini Kongo nacho pia kimekuwa kikikumbwa na kashfa kama hizo. Mnamo mwaka 2005, Umoja wa Mataifa uliwapiga marufuku wanajeshi wake kuwa na mahusiano na wakaazi wa huko baada ya kuibuka tuhuma kwamba wanajeshi hao walikuwa wamewanyanyasa kingono wasichana wenye umri wa miaka 13.
Miongoni mwa picha za kampeni hii mpya ya MONUSCO ni ile inayomuonesha msichana wa Kiafrika kitandani, kauziba uso wake kwa viganja, huku kofia ya chuma ya Umoja wa Mataifa na sare ya mwanajeshi wa Umoja huo vikiwa kando yake sakafuni. Picha nyengine inamuonesha mwanajeshi wa Umoja wa Mataifa akiwa hana shati kwenye chumba cha jela huku maandishi mekundu yakisomeka: “Ngono na watoto ni uhalifu”.
Maafa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati
Chanzo kimoja cha habari ndani ya MONUSCO kimeliambia shirika la habari la AFP kwamba kampeni hiyo ilikuwa imeshaandaliwa hata kabla ya kashfa ambayo ilipelekea kufukuzwa kwa mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kati, Babacar Gaye, Jumatano iliyopita.
Kikosi cha MINUSCA, ambacho kilichukuwa nafasi ya Kikosi cha Umoja wa Afrika takribani mwaka mmoja sasa, kimekuwa kikiandamwa na mkururo wa kashfa kama hizo zinazowahusisha wanajeshi wake. Hadi sasa kumeripotiwa malalamiko 57 ya utovu wa adabu, 11 kati yao yakihusisha unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.
Tuhuma za hivi karibuni kabisa ziliwekwa hadharani na shirika la haki za binaadamu la Amnesty International, ambapo msichana wa miaka 12 aliwaambia mashahidi kwamba alibakwa na mwanajeshi mmoja wa Umoja wa Mataifa wakati wa msako mjini Bangui mwezi huu. “Nilipopiga makelele, alinipiga vibao na kuniziba mdomo,” alisema msichana huyo.
Wiki iliyopita, Marekani ilisema imefadhaishwa sana na madai hayo ya unyanyasaji na kutoa wito kwa wakosaji kuadhibiwa, huku ikionya kuwa tuhuma hizo zinavidhalilisha vikosi vya Umoja wa Mataifa.
Kampeni hii ya picha ya MONUSCO, ambazo zimechapishwa pia kwenye mtandao wa kikosi hicho sambamba na mitandao ya kijamii, tayari zimechochea maoni mengi sana kwenye ukurasa wa Facebook, mmoja wao akisema “licha ya uzuri wa kampeni hiyo, ni aibu kwamba ilipaswa kufanyika kwani Umoja wa Mataifa ulitazamiwa ulinde na sio kuwashambulia watoto wadogo.”
Recent Comments