MGOMBEA wa Ubunge Jimbo la Kibamba kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Issa Mtemvu, amewataka wananchi wa jimbo hilo, kutumia wakati wa kampeni kuomba radhi kwa Rais Dk. John Magufuli, kwa kumkosesha kura za jimbo hilo wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015.
Amesema licha ya kutompigia kura Rais, na wagombea wengine wa CCM mwaka huo, lakini Dk. Magufuli, amelifanya jimbo hilo kuwa la kimkakati kwa kuelekeza miradi mbalimbali ya maendeleo na ujenzi wa miundombinu.
Hayo aliyasema juzi wakati wa kampeni za kumtambulisha mgombea wa Udiwani wa Kata ya Kibamba kwa tiketi ya CCM, Peter Ikamba, zilizofanyika Kibamba Chama, jijini Dar es Salaam.
Alisema Dk. Magufuli ameonyesha mfano wa uongozi bora kwa kutolipa kisasi cha kutopewa kura nyingi katika jimbo hilo kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, hivyo uchaguzi wa mwaka huu, wananchi wautumie kumuomba radhi kwa kumpa kura za kutosha.
Kwa mujibu wa Mtemvu, jimbo hilo ni miongoni mwa majimbo yaliyofanywa kuwa ya kimkakati na Dk. Magufuli, kwani miradi mingi ya maendeleo ameelekeza kujengwa na miundombinu ya barabara ameboresha.
Alisema viongozi wa upinzani waliochaguliwa kuwakilisha wananchi katika jimbo hilo, wameishia kula fedha za wananchi walizochanga kwa ajili ya kukarabati barabara za ndani na madaraja.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa wananchi kutumia vilelezo hivyo kuwakataa wanasiasa wa upinzani katika uchaguzi wa mwaka huu, wachague viongozi wa CCM.
Alisema uongozi wake utajikita katika kutatua kero za wananchi kwa kuandaa utaratibu maalumu wa kuwasikiliza na kushirikiana na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali.
Alivitaja vipaumbele vyake atakapopata ridhaa ya wananchi wa jimbo hilo ni kuboresha barabara za ndani kwa kiwanngo cha lami, kushughulikia changamoto za mikopo ya makundi maalumu, vijana na wanawake, ujenzi wa shule ya sekondari kidato cha tano na sita katika jimbo hilo.
Alitaja vingine ni kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji kwa wakazi wa jimbo hilo.
Naye Mgombea wa Udiwani wa Kata ya Kibamba, Peter Ikamba, alisema uongozi wake katika kata hiyo, hatautumia kama fursa ya kujinufaisha na badala yake atatengeneza na kuzitumia fursa mbalimbali kwa maslahi ya wananchi wa kata hiyo.
Recent Comments