Kile kilichoonekana kuwa huenda ukawa ndio mwanzo wa kurejesha uhusiano mwema baina ya Rwanda na Burundi mwanzoni mwa wiki hii, kimegeuka kuwa muendeleza wa mchezo wa paka na panya baina ya Burundi na Rwanda.
Mwanzoni mwa wiki hii, wakimbizi wa Burundi waliopo katika kambi nchini Rwanda walimuandikia barua rais wao Evariste Nayishimiye wakimuomba warejee nyumbani, barua na wakatuma nakili yake kwa serikali ya Rwanda na Shirika la Umoja wa Mataifa la huduma kwa wakimbizi- UNHCR.
Majibu ya barua hiyo awali kutoka kwa serikali ya Burundi na Rwanda kupitia mtandao wa Twitter yalionesha kwamba pande mbili ziko tayari kuwawezesha wakimbizi hao wapatao 60,000 kurejea nyumbani.
Hata hivyo mambo yamegeuka baada ya hotuba aliyoitoa siku ya Ijumaa rais Evariste Ndayishimiye alipokua katika eneo la Busoni katika mkoa wa Kirundo siku ya Ijumaa iliyoashiria kuwa uhusiano baina ya nchi hizi mbili ulioingia dosari wakati wa utawala wa mtangulizi wake Pierre Nkurunziza huenda ukaendelea kuzorota na hata zaidi.
Katika hotuba yake aliyoitoa katika eneo la Busoni mkoni Kirundo siku ya Alhamisi Rais Evariste Ndayishimiye alisema kuwa nchi yake haitakuwa na uhusiano na nchi ambayo inatumia unafiki, akisisitiza kuwa wakimbizi walioiandikia serikali yake wakiiomab warejee nyumbani wameshikwa mateka katika nchi walikokimbilia.
“Tunafahamu kuwa wamewateka nyara kwasababu hakuna mtu anayetaka kurejea nchini mwake huku kukiwa na nchi inayomkataza kurudi kwao…ina maanisha kuwa wamewashikilia kama wafungwa”, alisema rais Ndayishimiye.
” Kwahiyo tunaomba nchi hiyo iwaachilie warudi nyumbani katika nchi yao walikozaliwa”, aliongeza
Aliwaambia raia: “Kama wamewakataza kurudi nyumbani, njooni sisi tumejiandaa kuwapokea, halafu tutaona ni nani atakayewazuwia kwenye mpaka watu wanaotaka kurudi kwao”.
“Tunafahamu fika ni kwanini wale wakimbizi wametekwa nyara!.Waliwateka ili waendelee kuwalinda waliofanya maasi nchini mwetu. Tunafahamu . Kwani hao waliofanya maasi wanawafaidi nini kwa kuwapatia hifadhi ?”
Ndayishimiye alirejelea tuhuma za mtangulizi wake Hayati Pierre Nkurunziza ambaye mara kwa mara alikua akiishutumu Rwanda kuwapatia hifadhi waliojaribu kumpindua madarakani mwaka 2015.
Alisema kuwa jirani mwema anapaswa kukuletea wahalifu ili waaadhibiwe, badala ya kuwalinda.
Rwanda haijajibu lolote kuhusiana na kauli za hivi karibuni za rais Evariste Ndayishimiye hadi sasa.
Baada kumuandikia barua rais wao Evariste Ndayishimiye wakimuomba awasaidie kurejea nyumbani, mkimbizi aliyeishi katika kambi ya wakimbizi hao ya Mahama kwa miaka mitano, Emmanuel Bizimana aliwambia waandishi wa habari kuwa wamekua wakikatazwa kurejea nyumbani kwa njia zisizokubalika kisheria ”Kwahiyo sisi tumeandika barua ili tutumie njia halali kisheria kurejea nyumbani.”
Aliongeza kuwa kuna watu wanaowashawishi wasubiri kwanza kurejea nyumbani , lakini ni watu walioko ng’ambo, inawezekana ni wanasiasa wa Kirundi na wanafanya hivyo kwa manufaa yao ya kisiasa kwa kuwatumia wakimbizi.
“Baadhi yao wanataka kututumia kwa faida zao, ndio wanaosema tusirudi nyumbani kwasababu (matatizo). Hapa kambini kuna watu wanaoongea na wanasiasa walioko Ulaya na kwingine, wanaowatumia kwa ajili ya faida yao. “, alisema Bizimana.
Jumatatu wiki hii wizara inayohusika na shughuli za uokozi, ambayo ndio yenye jukumu la masuala ya wakimbizi ilitangaza kupitia ukurasa wa Twitter kuwa imejiandaa” kusaidia kuwarejesha nyumbani wakimbizi waliochagua kurudi kwao kwa ushirikiano na UNHCR pamoja na serikali husika”.
Elise Laura Villechalane, msemaji wa UNHCR nchini Rwanda, mwanzoni mwa Juma kuwa licha ya kwamba kuna makubaliano ya kuwarudisha nyumbani wakimbizi katii ya Rwanda na burundi ya mwaka 2005, pande zote tatu (nchi hizo mbili na UNHCR) lazima zikutane na kutatua tatizo hilo kwa pamoja
“Mnafahamu kuwa ili wakimbizi waweze kurejeshwa makwao pande zote tatu lazima ziafikiane”, aliongeza msemaji huyo wa UNHCR.
Kulingana na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) kufikia mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, kulikua na wakimbizi wa Kirundi 430,000 waliokimbilia katika mataifa jirani na Burundi
Kuanzia mwezi Juni 2015, wakimbizi wa Burundi walianza kuingia nchini Rwanda wakitokea nchini mwao kufuatia ghasia za umwagajidamu zilizoibuka nchini mwao baada ya uchaguzi wa urais na njama za kumpindua aliyekua rais wa nchi hiyo Hayati Pierre Nkurunziza kufeli.
Watu wengi waliuawa nchini humo na maelfu kuyakimbia makazi na wengine kukimbilia nchi jirani zikiwemo Tanzania, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Uganda na Rwanda
Rwanda ilipowapokea wakimbizi wa Burundi iliwaruhusu waliokua wanafunzi kuendelea kusoma hadi darasa la 12, katika kambi ya wakimbizi ya Mahama walipewa shule, hospitali, kila familia ikapewa nyumbailiyoezekwa kwa mabati.
Na hata kijana aliyefikisha umri wa kuoa aliyeomba nyumba hupewa nyumba.
Wakimbizi Warundi waliopo Rwanda hupewa pesa za kununua chakula na mahitaji mengine ya kimsingi, wanaobahatika kufaulu na kuweza kuingia Chuo Kikuu au sekondari hupata wasamalia wema wanaowalipia ada na pia serikali huwalipia bima ya matibabu kwa wote sawa na inayotumiwa na raia wa Rwanda.
Wakimbizi katika kambi ya Mahama pia walipewa gesi ya kupikia ili wasiharibu mazingira kwa kukata miti ovyo.
Kulingana na msemaji wa UNHCR nchini Rwanda, Elise Laura Villechalane, tangu mwishoni mwa mwaka jana wakimbizi wa Burundi walianza kurejea nyumbani na kuongeza kuwa walau kila mwezi mmoja wakimbizi 200 wamekua wakirudi nyumbani.
Aliongeza kuwa UNHCR inafanya kila liwezekanalo kuwezesha mazungumzo baina yake na pande mbili yafanyike haraka, hususan wakati huu wa janga COVID-19, kuhakikisha kuwa usafiri wanaoutumia ni wa kuaminika, wapimwe kwenye mipaka ili kuhakikisha kuwa hawana maambukizi ya corona .
Elise Laura Villechalane amepuuzilia mbali madai kuwa Rwanda imewateka nyara wakimbizi wa Burundi:”Nimesema kuanzia mwaka jana watu wapatao 200 wamekua wakiondoka kila mwezi , hiyo ni ishara kwamba watu wakimbizi wamekua wakiondoka .”
Tangu enzi ya utawala wa Hayati Pierre Nkurunziza , Rwanda na Burundi zimekua zikilaumiana kila upande kwa kuwahifadhi wapinzani na waasi wanaoendesha mashambulio kwenye ardhi ya kila upande
Uhasama baina ya nchi hizi mbili umedhoofisha biashara kati ya nchi hizo na urafiki wa raia wa pande mbili wanaozungumza lugha zinazofanana. Mzozo huu pia ni mojawapo ya mambo yanayokwamisha juhudi za kuimarisha mahusiano na maendeleo katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Recent Comments