Na, Mwandishi wetu kutoka Ngara
Baada ya Kitendawili cha nani apewe dhamana ya chama kupeperusha bendera ya CCM jimbo la Ngara,waliokuwa watia nia na washindani wa karibu kwenye mchakato wa ndani wa kura za maoni katika jimbo hilo wameungana na kuahidi kushirikiana kutafta kura za chama hicho kuanzia ngazi ya udiwani ,ubunge pamoja na kura za Rais Dkt John Magufuli.
Chama cha Mapinduzi baada ya kupitia hatua zote za kumpata mgombea anayefaa katika jimbo la hilo, hatimaye August 20 mwaka huu kilimtangaza Ndg Ndaisaba George Ruhoro kugombea katika jimbo hilo ambapo siku iliyofuata alichukua fomu tayari kuanza mchakato wa kuomba ridhaa ya wananchi baada ya kuaminiwa na chama.
Mapema Kura za maoni katika jimbo hilo zilionekana kuwa na ushindani mkubwa licha ya kuwa maamuzi ya mwanzo yalianzia kwenye maoni ya wajumbe waliopiga kura na wagombea kila mmoja kuhesabu kura zake bila kificho wajumbe wakishuhudia kila hatua.
Jambo la Furaha ni kuwa baada ya mchakato wa chama kukamilika na Mgombea kupatikana wanachama ambao walikuwa watiania katika jimbo hilo lililokuwa na watia nia 43 wamejitokeza kumsindikiza mwenzao kuchukua fomu kwa msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo huku wakiahidi kuhakikisha kura za chama zinapatikana .
Mbunge aliyemaliza muda wake Alex Gashaza ambaye pia katika kura za maoni za wajumbe alikuwa mshindi wa pili akiwa katika msafara wa pamoja na mgombea huyo kuelekea kuchukua fomu,amesema kuwa maamuzi ya chama yanalenga kuboresha na kwamba katika chama cha mapinduzi hakuna kushindwa bali uongozi ni kupokezana ili kuhakikisha wananchi wapata maendeleo ya kweli.
Amesema imani ya chama na wananchi kwa miaka mitano ya ubunge wake 2015-2020 ameitendea haki kwakuwa kila kilichofanyika ni mipango ya chama na serikali kuhakiksha uchumi wan chi pamoja na watu unaongezeka.
Kwa upande wake ndg Issa Samma aliyekuwa mshindi wa tatu katika kura za maoni za wajumbe amesema shughuli ya kujenga chama hajaianza jana wala hategemei kuiacha kesho zaidi ni kwamba mchakato wa kusaka mgombea ndani ya chama ni utaratibu wa kawaida ambao lazima ateuliwe mmoja na wenzake wasubiri huku wakiendelea kushauriana namna ya kuboresha chama.
Nae Mgombea alieteuliwa na chama amesema ataendelea kuchota busara na mawazo ya wenzake ili kuendelea kulinda heshima ya chama wakati na baada ya uchaguzi.
Nae mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilayani hapa,Bw George Rubagola amesema baada ya majina ya wagombea udiwani na nafasi ya Mbunge kuwekwa hadharani chama kiko tayari kufanya kampeni za kistaarabu bila kuvunja sheria za nchi pamoja na sheria za uchaguzi .
Ikumbukwe kuwa zoezi la kuchukua na kurudisha fomu kwa wagombea wa vyaa vyote vya siasa litakamilika august 25 mwaka huu huku mikutano ya kampeni ikitarajiwa kuanza siku inayofuata ya tarehe 26 mwezi wa nane.
Recent Comments