RAIS wa Gabon, Ali Bongo Ondimba ameahidi kutoa sehemu kubwa ya urithi alioachiwa na marehemu baba yake, Omar Bongo kwa vijana wa taifa hilo.
âKwa macho yangu, sote tu warithi wa Omar Bongo,â Rais alisema wakati akilihutubia taifa jana ikiwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa nchi hiyo.
Kiasi rasmi cha urithi wa baba yake ambaye alitawala taifa hilo kwa miaka 41 hadi alipofia madarakani mwaka 2009, bado hakijajulikana, lakini ameripotiwa kujilimbikizia utajiri wenye thamani ya mamilioni ya dola.
Rais Bongo alisema mbali ya kutoa fedha za urithi kwa mfuko wa vijana, familia yake itatoa jumba la fahari lililopo katika mji mkuu, Libreville, kwa ajili ya chuo kikuu kipya.
âHakuna Mgaboni atakayeachwa njiani,â aliongeza.
Majumba mengine mawili ya fahari yaliyopo Paris Ufaransa yatauzwa na fedha itakayopatikana itaingizwa katika mfuko wa ukuzaji uchumi wa vijana na jingine nchini Gabon litatolewa kwa taifa.
âNajua baba yangu pale alipo sasa anatutazama, anatusikia. Pia najua anaridhia uamuzi huu na anatupa baraka zake,â AFP lilimkariri Rais Bongo akisema.
Ahadi hizo za Rais Bongo zinatolewa wakati ambao majaji nchini Ufaransa wamekuwa wakifuatilia na kuchunguza chanzo cha mamilioni ya fedha zilizotumika kununua na kujenga majumba ya fahari nchini humo.
Wapinzani na wanaharakati wa kupambana na ufisadi wanasema huenda Rais Ali Bongo ameona kibano kinachokuja akaamua kulirejeshea taifa mali zake.
Awali Shirika la Kimataifa la Kupambana na Ufisadi, Transparency International, liliwasilisha kesi mahakamani likitaka majaji wa Ufaransa kuamuru kuwa mali ya umma ilitumika kujinufaisha wakati wa utawala wa marehemu baba yake.
Kwa miaka mingi wanaharakati wamekuwa wakiihusisha familia hiyo ya Bongo kwa ubadhirifu wa mali ya umma, madai ambayo familia hiyo imekuwa ikiyakana kwa nguvu.
Mbali ya kuchunguza mali ya Bongo, Ufaransa pia inachunguza mali za familia za viongozi wa Equatorial Guinea na Congo-Brazzaville.
Ali Bongo alishinda uchaguzi wa urais Septemba 2009 na kumfanya kuwa rais wa tatu wa taifa hilo tangu lipate uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960.
Gabon ni miongoni mwa nchi katika Afrika zinazotoa mafuta kwa wingi lakini theluthi moja ya wananchi wake wanaishi katika umasikini, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.
Recent Comments