Recent Comments

Sekeseke la Afrika Kusini na Kizungumkuti cha Uhuru Bandia Afrika

By Denis Mpagaze Sep 29, 2019

“Wasauzi” wamekuwa kero Afrika. Wanaua ndugu zao kwa makusudi bila kujua. Afrika Kusini kwa Madiba hapafai tena. Bondeni pamekuwa bondeni hasa. Tatizo siyo “Wasauzi”. Tatizo ni Uhuru bandia wa Afrika yote. Afrika bado ni mali ya wazungu. Tangu waigawane katika kile kikao cha majambazi mwaka 1885 pale Berlin na kupeana hati hawajakutana tena kuzibatilisha. Bado hizo hati zipo. Zimehifadhiwa Vatican City kwa Baba Mtakatifu, mahali wanapokula minofu ya Ziwa Nyanza na wenye ziwa kula mapanki.Wa kanda ya ziwa wananielewa maana ndo zao kula mapanki na wakati ziwa liko kwao.Hii haijakaa freshi kabisa.

Hizi fujo za ‘Sauz’usidhani zilianza leo. Zimeanza kitambo sana. Toka karne ya nne wabantu walivyovamia Sauz na kuwavuruga wenyeji walioishi kwa raha mustarehe wakila mawindo ya mikono yao na kunywa maziwa ya mifugo yao. Wakati huo Sauz haina mbantu hata mmoja. Nchi ilikaliwa na jamii za San au Bushmen wale wanaochekesha mapori na Khoikhoi. Wanaitwa Khoisan yaani muunganiko wa Khoikhoi na San kwa sababu wanafanana kimaumbile na kutofautiana kimajukumu, Bushmen ni wawindaji na Khoikhoi wafugaji.

Wazungu wa kwanza walitia nanga Sauz wakitokea Ureno. Waliongozwa na mpelelezi Bartolomeu Dias, wakitafuta route ya kwenda Asia kufanya biashara ya viungo vya pilipili, tangawizi, mdalasini na bamia, siyo vibamia. Ilikuwa mwaka 1488. Safari hiyo iliyojaa raha na karaha ilianzia Mto Tagus pale Lisbon Ureno. Njiani walipigwa na dhoruba kali hadi wakaomba poo, Mungu saidia wakaibukia kwenye rasi na kuwakuta wakhoisan wakiishi hapo lakini Bartolomeu akapaita mahali pale Cape of Storm as if wenyeji hawakuwa na jina na kuitangazia dunia kwamba yeye ndo alivumbua nchi ya Afrika Kusini. Ndo yaleyale ati Ziwa Victoria liligunduliwa na wazungu na wakati liliitwa Nyanza. Baadaye Mfalme Mfalme John II, alibadilisha jina hilo na kuitwa Cape of Good Hope yaani Cape Town ya leo.

Mwaka 1647 wafanyakazi wa Dutch East India Company wakiwa kwenye safari zao za Asia walikwama pale Cape of Good Hope kwa miezi kadhaa, wakavutiwa na ardhi nzuri, ukarimu wa wenyeji, wingi wa misosi na kuwashawishi wakulima wa kizungu yaani makaburu kutoka uholanzi kuhamia Sauz. Mwaka 1652 makaburu wakahamia pale mazima na roho zaa za kibaguzi na kudai Cape ni nchi yao ya Ahadi waliyoahidiwa na Mungu. Wenyeji wakasema achani ukuda. Wakatwangana kishenzi. Kaburu na migobore yake, Mkhoikhoi na mikuki, upinde na mishale yenye sumu na mikuki. Hata hivyo wenyeji walishindwa vita kwa sababu makaburu yaliwapelekea magonjwa ya Surua na Ndui, wakafa. Wazungu sio kabisa. Hata Kigoma na Ngara walimwaga makontena ya funza ili watafune vidole vya vijana waliokuwa wanakimbia enzi za utumwa.Madhara yake yapo hadi leo. Wengi waliotafunwa na funza hawana kucha na miguu imepinda.

Baada ya kuona sasa hali imekuwa tete, wakhoisan waliamua kukimbilia  kwenye Jangwa la Kalahari kama Wangoni walivyokimbilia Songea baada ya kuchapwa makofi mawili matatu na Shaka Zulu kati ya 1820 and 1840. Waliingia Songea kwa mkwara mzito, waulize wandendeure. Kuna mshikaji mmoja aliitwa Mtepa Gama. Huyu bwana alikuwa kauzu zaidi ya dagaa.Kwanza aliwatandika wenyeji na kisha kuwateka na kujimilikisha watoto waliozaliwa. Wakaitwa kwa jina la ukoo wake, Gama. Leo hii ni ukoo mkubwa sana. Ila na wenyewe walitandikwa na Mjerumani mpaka huruma. Aliwanyonga kweli. Siku hizi Wangoni ni wapoleee kama maji mtungini. Halafu toka mwaka 93 Bambo ndo Super Star wa Wangoni.Loh!

Makaburu yakaendelea na maisha pale Cape of Good Hope wakitumia Bible kuhalalisha ushenzi wao. Sisi tunawaita makaburu lakini wao wanajiita Wana wa Israel maarufu kama Wayahudi ndo maana hata yule mchungaji wao alivyoulizwa kwa nini wasiondoke kwenye ardhi ya watu alisema umeandikwa katika Torati ya 32:8 kwamba, “Yeye aliye juu alipowapa mataifa urithi wao, alipowabagua wanadamu; aliweka mipaka ya watu kwa kadri ya hesabu ya wana wa Israeli”. Hata vile vinu vya nyuklia vilivyojengwa Sauz mwaka 1976 vilijengwa na serikali ya Israel na Sauz kuwa ya nchi ya kwanza Afrika kuzalisha silaha za nyuklia,lengo ilikuwa kulinda ardhi yao isivamiwe kwa sababu ardhi kwao ni ya pili baada ya Mungu kama ilivyo pombe kwa mlevi.

Leo Sauz ni kati ya nchi 12 duniani zenye wayahudi wengi. Hata lile jamaa lililokamata ndege yetu ni liyahudi la Sauz. Nitakupa ubuyu baadaye ngoja tumalize mambo ya msingi kwanza.

Hawa watu yaani Wayahudi ni wachache sana lakini ndo wanaotawala dunia. Wako milioni 14.5 tu lakini, fedha na vitu vyote vya thamani ni mali yao. Wanamiliki media na mabenki na teknolojia. Nusu ya wayahudi wote wanaishi Marekani. Wanajiita taifa teule la Mungu. Prince Katega anasema haya ni matapeli tu kama matapeli mengine, hakuna cha taifa teule wala nini. Lakini Prince Katega naye ni mtata, havumi lakini ana mengi kweli.

Prince anasema wayahudi  ni wazungu waliotokea huko Urusi karne ya 6 AD baada ya kuukataa ukristo na uislam maana dini hizo zilishambuliana kishenzi. Sasa ili kuwa salama wakajiunga na dini ya Kiyahudi ambayo ndo ilikuwa imeanza. Walivyoanza kusambaa walitua Ujerumanin ya Mashariki, wakaungana na Wazungu wengine walioitwa “The Ashkenaz” ambao nao walikataa Ukristo na Uislam wakaanza biashara ya vito, mabenki na vyombo vya habari na utengenezaji wa filamu. Hawa ndo walianzisha mifumo ya kodi inayotutoa jasho. Waliishauri Ujerumani ianze kuwatoza wananchi wake kodi na wao wakawa mawakala wa kuikusanya chini ya familia ya The Rothchild. Hapo ndo wakawa wametoka kimaisha, wakawa na jeuri ya pesa.

Wakajitungia historia katika vitabu vitakatifu vya Biblia na Kurani kwamba wao ni taifa teule la Mungu walioahidiwa Afrika kama nchi yao Ahadi. Mwaka 1917 wakaishinikiza Uingereza iwape eneo la Kaskazini-Mashariki ya Afrika, wakaliita eneo hilo Middle East, wakatua Palestina na mwaka 1948 likazaliwa taifa jipya la Israel. Mpango wao ni kuitawala Middle East yote na Afrika nzima. Kwa sasa wako Israel na Sauz. Wanachinja na kuua!

Jeuri, ubabe na ubaguzi ndo hulka ya wayahudi. Wanaamini kufanya hayo ni maagizo kutoka kwa Mungu mwenyewe. Kwa binadamu mwingine kudai ni sawa na ngedere kufanya ugaidi kwenye shamba la mahindi. Ndo maana kila aliyewapinga cha moto alikiona. Hawa ndo walimfunga Mandela miaka 27, wakamnyonga Steve Biko, mwaka 1976 waliua vitoto vya shule 600 kwa risasi za moto pale Soweto waliofanya maandamano ya amani kupinga ubaguzi, wakapuumzishwa kwa amani. Ajabu kweli!

Tabia zao za kishenzi ndo zimefanya ukatili kuwa jadi ya wasauzi wote, ndo maana masauz kukutoa roho mchana kweupe siyo issue. Yalimuua Baraka wa Kasulu hivi hivi. Ilikuwa tarehe 23 Februari 2018. Baraka ndo alikuwa anamalizia PhD yake pale Johannesburg University. Baraka alitoka familia ya kimaskini akapiga vibarua mpaka vya ulinzi kupata ada ya msingi mpaka university, akafaulu kwa kishindo, akaajiriwa kufundisha chuo kikuu cha SAUT pale Mwanza, akaenda Ubeligiji kwa masomo ya Masters, na baadaye Sauz kwa PhD, halafu akarudi kwao Kasulu na cheti cha kifo badala ya cheti cha PhD kwa sababu mbuzi wa maskini hazai. Moyo wangu ukaniuma kweli kwa sababu nilimfahamu Baraka kuanzia kwao Kasulu mpaka kazini SAUT. Pumzika kwa amani Comrade.

Ukiambiwa Sauz hapafai kama choo cha soko usifikiri masihara. Movie ya Sarafina inatosha kuielezea Sauz kwa kina, lakini tambua kila siku iendayo kwa Mungu sauzi wanauawa watu wasiopungua 57 kwa sime, mapanga, virungu, bastola na matairi ya gari. Ukiwa Sauz  uhakika wa kuuawa muda wowote ni mkubwa kuliko nchi yoyote Afrika. Wenye uhakika mdogo wa kufa kwa mapanga na mashoka ni familia zinazoishi kwenye mageti na ulinzi. Ni nchi inayoongoza kwa utitiri wa makampuni ya ulinzi Duniani. Idadi ya walinzi wa makampuni ni kubwa zaidi ya polisi na jeshi la nchi hiyo. Halafu walinzi wanaolipwa mishara ya kumudu makongoro na utumbo wa kuku. Yaani wanalalaliwa kama housegirl wa mwalimu na mkunga.

Lakini pia Sauz inaongoza kwa ubakaji duniani. Kila wanaume wanne, basi mmoja aliishawahi kubaka na wakati kila wanawake watatu, mmoja kaishabakwa. Vinabakwa mpaka vitoto vyenye miezi tisa kwa sababu wanaamini kubaka vitoto kunaondoa gundu. Ni nchi yenye waganga wengi wa jadi, wanaitwa Sangoma. Halafu kinachoniacha hoi karibu nchi nzima ni wakristo lakini zaidi ya nusu wanaamini katika ushirikina na ndumba kama huko kwenu tu kwenye watu wengi wenye Biblia kifuani, Korani mkononi, hirizi kiunoni na matunguli shingoni kwa maana wamechanganyikiwa.

Halafu ni nchi iliyotunga sheria ya ndoa za jinsia moja tangu mwaka 2006. Sauz ukizubaa mwanaume kuolewa kuko nje nje. Wamevurugwa kwelikweli.

Tabia za kishetani kwa Wasauz za kuuana wao kwa wao zilipamba moto enzi za utawala wa Shaka Zulu. Shaka, alikuwa shujaa mwenye bwegwe kwelikweli. Alishambulia vijiji,akaua watu kijiji kizima, akachoma mashamba na nyumba zao na kuondoka na mifugo kwa fahali ya kuwa na ardhi kubwa. Aliua mpaka nchi ikabaki ukiwa. Siku aliyofanya kufuri ni wakati wa kifo cha mama yake Nandi. Aliua wanajeshi wake 7000 kwa sababu tu hawakuonyesha huzuni kwa kifo cha mama yake. Aliamuru nchi nzima kufunga na kuomba kwa miezi 3 wakiomboleza msiba wa mama yake.Alipiga marufuku kulima kwa mwaka mmoja, wanawake kubeba mimba, na kuua wajawazito na wame zao wote. Alikuwa kauzu zaidi ya dagaa! Kaka zake Dingane na Mhlangalangana ilibidi wamnyonge na kumtupa shimoni kwa sababu walijua kachanganyikiwa.Hii Dunia ilikuwa na watu Shekhe!

Kwa muziki wa Shaka, wangoni wakaamua kulikimbia jij na kuja kuishi Songea kwa raha mustarehe. Kwahiyo kabla hujafikiria kuzamia Sauz kwa hoja ya kwamba tuliwasaidia kupigania uhuru, kawaulize kwanza wangoni. Lakini huo uhuru wenyewe waliupata? Unapataje uhuru bila ardhi? Kwa taarifa yako Wasauz hawana ardhi kabisa. Asilimia 87 ya ardhi yao ni mali ya Kaburu. Bora huku kwetu maisha yakigoma town unaweza kimbilia kijijini, ukajenga kijumba cha nyasi na tope ukapata na mke kabisa, mayanki wa Sauz hata kupata demu ni issue.

Mandela pamoja na kusifiwa huko Duniani alishindwa kuwanyanganya wazungu ardhi kama alivyofanya comrade Mugabe kwa sababu ndo waliompa Urais.

Prince Katega anakwambia Mandela ndo aliwaangusha Wasauz. Akiwa gerezani, Wasauz walikuwa wanaelekea kupata uhuru maana Dunia nzima ilikuwa upande wao. Makaburu chini ya De Klerk wakatumia akili kubwa sana, kubadilisha agenda. Wakamtoa Mandela Jela kwa masharti ya kumpa Urais na kweli alivyoingia Ikulu aliwasamehe wabaguzi na wauaji wote isipokuwa mke wake Winnie kwa sababu mapenzi hayana akili.

Jina la Mandela likatukuzwa Afrika na Duniani kote, wazungu wakamjengea hadi samu huko kwao, Mugabe akawambia hilo ni changa la macho, mwanaume Afrika ni Nyerere tu. Makaburu yakalitumia jina zuri la Mandela kupora ardhi nchi mbalimbali za Afrika ikiwembo, Msumbiji, Zambia, Malawina Congo.

Mandela akafika mpaka Tanzania, akateta na Mzee Mwinyi, milango ya Tanzania ikafunguka, Makaburu wakaingia nchini kwa mbwembwe za uwekezaji, wafungua shoprites kuuza mpaka pilipili na chapati kutoka Sauz, wakashika kuanzia ardhi, madini, mabenki, ndege mpaka umeme, tukavuna kashifa za Meremeta, Tangold, Majengo pacha ya BoT, TBL ikayumba, NMB akachacha, Viwanda vya Bia vikafa kifo cha mende, NBC ikawa kituko na ATCL ikaingia mushikeli, jina la Mandela likatutia kitanzini ingawa vijana haya hawayajui, wao wanachojua ni Mandela baba wa Afrika.

Mandela kaishaondoka, kawaachia Wasauzi majanga. Makaburu wanakula vizuri, wanaishi vizuri na kutibiwa kwenye hospitali ya tatu kwa ubora kabisa Duniani, iko pale Sauz, inaitwa Chris Hani Baragwanath Hospital, wenyeji wanachenza kwaito na kunywa ulanzi, wakilewa wanawaua ndugu zao, ati ni wahamiaji haramu na wakati Afrika ni moja. Huu ni ujinga ngangari. Wenyeji anaua huku wageni wakitafuna nyama choma huku wakicheki Manchesta ikimenyana na Man U kwa sababu vita vya panzi faida kwa kunguru.

Wasauz wanaua wahamiajia haramu Kaburu anaingiza mzigo mpya wa watumwa kutoka kila kona ya Afrika wanaozamia Sauz kila kukicha, anawatumikisha kuanzia migodini mpaka viwandani kwa malipo ya NA KESHO UJE, UKIUGUA USIKANYAGE HAPA kwa sababu maskini hana hoja, yeye anahaja ya mkono kwenda kinywani. Hili ndilo linawachefua Wasauz. Kwa nini wageni wakukubali ajira zisizo na tija? Katika hili Wasauz wanahoja ya msingi sana, sema tu wanakobugi ni njia wanazotumia kuondoa kero, kuwafukuza, kuwapiga na kuwaua ndugu zao.

Kimsingi aliyetakiwa kupigwa hadi achakae ni kaburu anayetumia njaa zao kuwagawa maana anajua hakuna umoja wa wenye njaa uliowahi kudumu kwa sababu akija mwenye chakula atawagawa tu. Tabia ya kuwatumikisha wenye njaa hakuianza leo. Nakumbuka mwaka 1904, serikali yao imewahi ingizi mzigo wa vibarua kutoka kutoka China.

Makaburu waliota mapembe siku mwingereza amewapa uhuru ile mwaka 1910. Tangu wapate uhuru huo wametunga sheria nyingi kuwakandamiza weusi maana hawaamini kabisa kama mweusi ni binadamu, hata Pieter Botha aliwahi kusema, “Ukweli kuwa weusi wanaofanana na binadamu na kutenda mambo kama binadamu hayawahalalishi kuwa wao ni watu wenye akili timamu au binadamu aliyetimia. Kanunguyeye si nungunungu na mijusi hawawezi kuwa mamba kwa sababu eti wanafanana”.

Pamoja na Mwingereza kuwaachia uhuru lakini aliwatoa jasho kweli mpaka wakaikimbia Cape Town  kuelekea Majimbo ya Orange na Transvaal, katia safari iliyoitwa The Great Trek. Ilikuwa mwaka 1836 na 1837.

Ubaguzi ulipamba moto pale Hendrik Verwoerd alipoingia madarakani kama Waziri Mkuu. Ilikuwa 1958. Utawala wake ulifanikisha ubaguzi mpaka kwenye mapenzi na ndoa dadaki. Nyani walioana kwa nyani, tumbili kwa tumbili na binadamu kwa binadamu. Sisi walituita Nyani. Ole wako Nyani upendwe na mtoto wa kizungu sasa, loh! Muziki wake, mwe! Sheria iliwagawa watu kwa rangi zao, weusi, machotara, wazungu na waasia. Mtoto chotara akatengana na wazazi wake. Kwa mweusi kuingia mjini haikuwa mpaka uoge tu, ulitakiwa kuwa na hati maalumu.

Hendrik alifanikiwa sana katika ubaguzi, naye kifo kikambagua, alikufa kwa kuchomwa kisu cha shingo na Kaburu mwenzake kwa sababu mshahara wa dhambi ni mauti. Ilikuwa 1966. Lakini mshikaji alikuwa kauzu kweli. Aliwafukuza weusi mijini na kuwapeleka Bantustans kumi, yaani makazi ya malofa, halafu akawanyang’anya uraia na haki ya kupiga kura. Wasauz walipiga kura kwa mara ya kwanza 1994 kumchagua Nelson Mandela akawaangusha. Mimi sitawaangusha.

Sasa ngoja nikupe ubuyu wa lile yahudi lililokamata ndege yetu. Linaitwa Herman Styn. Jamaa limezaliwa Vienna, likaishi S.Afrika, Libya, likaenda Kenya, likaja Bongo, likatuliza ardhi, kutoka Bongo likarudi Kenya, kutoka Kenya likaenda Sauz likitafuta fursa, mwenzangu hujawahi toka nje ya mkoa uliozaliwa halafu unajiita mjasiriamali.

Iko hivi:Miaka ya 80 Serikali ya Tanzania ilitaifisha mashamba ya Styne huko mkoani Arusha yenye wa heka laki mbili, sawa na nchi ya Rwanda. Steyn akatinga mahakamani, serikali yetu ikashindwa kama kawaida, tukatakiwa kumlipa fidia, lakini baadaye serikali ikashtukia dili na kuacha kulipa deni hilo na kumpiga marufuku Steyn kukanyaga Tanzania.

Yahudi akahamishia kesi yake Sauz na kuomba itekelezwe kwa kukamata mali za Tanzania. Alishauriwa hivyo na mawakili wake wa Kitanzania halafu sisi tukawashukia mawakili wetu kwamba hawana uzalendo na wakati kisheria wakili kumtetea mwizi hakumuondolei uzalendo. Kwamba anapofanya hivyo haina maana anaunga mkono uhalifu. Hizi sheria bwana.

Anyway kikubwa tusipoteze muda na mawakili wake badala yake tusikubali kulipa fidia kwenye ardhi yetu maana tukifanya hivyo wataibuka wale wote tuliotaifisha mali zao baada ya uhuru. Usishangae kuwaona vitukuu vya Car Peters vikija kudai chao. Ohoo!

Uzuri mahakama ya Guteng ya Afrika Kusini imemuamuru Styn atulipe fidia kwa sababu dawa ya kuondoa giza ni kuweka mwanga na sio kufumba macho. Herman Steyn atalipa gharama za usafiri, chakula, mawasiliano na malazi ya mawakili waliokwenda kuendesha kesi hiyo, usafiri wa mawakili wa serikali kwenda nchini Afrika Kusini ili iwe fundisho na kwa wazungu wengine wanaotuchezea kama midoli.

Yaani wazungu kila siku wanatafuta namna ya kuendelea kututawala maana wanajua tukiamka wamekwisha. Sasa hivi wamekuja na uongo wa viumbe vinaitwa aliens, ati ni viumbe vyenye akili sana kutoka sayari za mbali, ndo vinavumbua teknolojia zote kubwa kule Marekani, wajinga wameanza kuamini. Hivyo ndo watavitumia kuja kupiga nchi zetu na kuiba mali zetu na sisi kubaki tunasema kwamba ni viumbe vya ajabu. Hawa watu wanaakili sana katika kutengeneza ajenda.

Katega anakwambia hata Biblia ni ajenda yao ya muda mrefu ambayo sasa wanatekeleza na sisi kusema ati ilitabiriwa.

Tatizo la Sauz litamalizwa kwa Afrika yote kuungana. Na muungano wa Afrika lazima uanzie kichwani. Wazo la Kwame Nkrumah lilidunda kwa sababu lilianza kwa kushindwa. Tulipigania uhuru kulinda mipaka ya wazungu. Afrika ikapata uhuru kwa mafungu, walianza Ghana wakamalizia Afrika Kusini 1994. Huu siyo Uhuru. Ni mpishano wa wakalia viti Ikulu tu. Awali alikaa Mzungu na sasa anakaa Mweusi kuendesha nchi katika fikra za kikoloni, ndiyo maana bado tunafikri kikoloni, tunavaa kikoloni, tunaabudu kikoloni, tunakula kikoloni, tunasoma  kikoloni na kuishi kikoloni.

Tunazalisha madaktari kuwa mawakala wa viwanda vya dawa za wakoloni, watumishi wa Mungu kutukuza dini za wakoloni, wachumi kusimamia uchumi wakoloni, wanasheria wanatufunga kwa sheria kikoloni. Nasema kwa dhati kabisa hivi vinchi vyetu ni mali yao ndo maana wanaobligation ya kuziadhibu nchi ambazo haziendani na matakwa yao. Waliipiga Iraq, wakaipiga Libya na sasa wanamvutia kasi Kim Jun Un.

Wazungu wanahakikisha wabaki juu mawinguni kama Piere ili tuendelee kuwatukuza, leo mtu anaona fahali kupiga picha na mzungu, kuoa mzungu hata kama ni kikongwe,kuishi Ulaya hata kama ni kwa kuzibua mitaro, yaani hata ukimpa lift mzungu kwenye gari lako, watasema wewe ni dereva wake, ukijenga nyumba nzuri watasema unaishi uzunguni, tuna mpaka viaziulaya na mapera ya kizungu vijijini, yaani tulipigwa tukapigika.

We must learn to live together as brothers or perish together as fools alisema Martin Luther King, Jr.

Habari ndo hiyo!