Recent Comments

Twende na Prince Katega II katika kuufahamu ukuu wa mwafrika na uasi wa akili

By Denis Mpagaze Aug 2, 2019

Sijawahi kukutana na mtu anayeujua mkwamo wa Afrika kama Prince Katega II. Halafu anaipenda Afrika kwa dhati.Huyu nshomile havumi lakini ana mengi. Kwanza kabisa ni msomi wa PhD katika masaula ya historia ya Afrika, siunajua tena wahaya kwa kitabu? Kwa sasa anaishi nchini Uingereza akila na kunywa walivyoiba wazungu. Namchukulia Prince kama fikra Afrika. Unahitaji utulivu wa akili kumuelewa, vinginevyo unaweza kuchanganyikiwa. Mie siku aliposema “Yesu aliisharudi siku nyingi” nilishtuka lakini alivyofafanua nikasema hakika Neno la Mungu ni Fumbo la imani, kulifumbua unahitaji utulivu wa akili. Nitakwambia alivyosema ngoja kwanza nifanye kilichonileta hapa.

Kwanza kabisa biashara ya utumwa ilituvuruga tukavurugika Afrika, dini zikatugawa tukagawika Afrika, ujinga ukatupiga tukapigika, tukawa wajinga wa kuogopa kila ukweli unaosemwa kututoa utumwani na hivyo kuendelea kumuita aliyetusababishia mkwamo huu mfadhili, na wakati yeye anatuita washenzi. Prince Katega II anasema haya yanatokea kwa sababu tumeasi asili yetu na kudhani kila kitu kutoka nje ni bora. Matokeo yake tumekuwa kituko cha dunia. Tunamuomba Mungu kwa lugha tusiyoijua, tunamuabudu Mungu tusiyemjua, tunaitwa majina tusiyoyajua, tunavaa nguo tusizozijua, tunatibiwa na dawa tusizozijua, tunakula na kunywa tusivyovijua, tunasoma elimu tusiyoijua, tunaishi na watu tusio wajua, tumekuwa wazungu bandia, hata mtu mweusi kama mkaa anaitwa Mr. White badala ya kuitwa Rwegasira, Mwanamalundi na Kinjekitile.

Mimi huu nauita utumwa wa fikra, Prince anauita Mental Terrorism. Tunatembea kama watu waliokatwa vichwa. Hatuna ladha ya uafrika tena. Ile ladha ya kunywa mitishamba kutibu mvurugiko wa tumbo, ile ladha ya kunywa maji ya chemchem na kuoga mtoni wakati wa mbaramwezi, ile ladha ya kupiga magoti kwenye makaburi ya mizimu yetu kuomba mvua, amani na mavuno, ile ladha ya kupeleka dawa nchi za mbali kwa usafiri wa ungo, ile ladha ya kuomba ukitakacho kwa jina la mizimu, waganga na waganguzi, ile ladha ya kufanya uzazi wa mpango bila kumeza kemikali zenye sumu, ile ladha ya wanaume kukaa chini ya mti wakinywa ulanzi, mbege na komoni wakijadili issues, ile ladha ya kijana kutafutiwa mke bora na si bora mke, ile ladha ya kuwatuma nyuki na radi kuwashughulikia adui, ile ladha ya kuazimana chumvi, moto na mafuta ya kula, ile ladha ya mtoto kulelewa na kijiji kizima, ile ladha ya ngoma za mdundiko, ile ladha ya kutembeleana na kujuliana hali, ile ladha ya mtoto wa kike kuchumbiwa na si kuchumbia na ladha nyingine tamu kama asali ya bibi hakuna tena Afrika. Tumeambiwa kufanya hayo Mungu hapendi, ni ushenzi. Wakatupangia namna ya kubehave mbele ya Mungu na wakati Prince Katega II anasema sisi tumemjua Mungu kabla yao. Hivi kati ya Farao mwafrika na Ibrahimu mzungu nani alikuwa mshenzi? Anauliza Prince. Mwanaume mzima unadanganya hadharani kwamba mkeo Sarah ni dada yako ili abebwe na mwanaume mwenzako? Hivi ni Mungu gani anaweza kufanya hayo? Katega anasema Farao asingekuwa mtu wa Mungu asingeepushwa na dhambi ya kuzini na mke wa mtu.

Tumemuasi Mungu wetu tukaparamia Mungu wa kuja, tukavuna dhambi ya ubaguzi, tumeacha elimu yetu ya maarifa, tukaenda shule kupambana na mitihani badala ya kupambana na ujinga. Siku hizi fasheni ni kuwa na cheti kizuri hata kama huna ukakika wa kujilisha. Aliyesoma anamuita asiyesoma primitive, kwa jina la dini sasa tunaitana makafiri, wapagani, washirikina, machizi, wapotevu na mzungu kutuita sisi sote washenzi. Zamani waliwagawa wazee wetu kwa viboko, siku hizi tunabaguana kwa ridhaa na utashi kwa sababu hatuna akili.

Tumeaminishwa kwamba bila wazungu hatuwezi kuishi na kumbe wao ndo hawawezi kuishi bila sisi. Sisi tumeishi bila wao kwa zaidi ya miaka milioni nne iliyopita na tukafanya makubwa. Katega anakwambia ushahidi wa lile Fuvu la Olduvai George lenye umri wa miaka milioni 1.8, nyayo za pale Laitory Ngorongoro tangu miaka milioni 4 iliyopita na Dada Lucy aliyeishi pale Ethiopia miaka milioni 2.5 vinatosha kuthibitisha sisi ndo wazee wa dunia hii. Ukweli huu hawapendi ujulikane ndo maana wakatuaminisha kwamba binadamu wa kwanza aliishi Mashariki ya Kati, Bustani ya Edeni ambayo wanasema ni pale Iraq, ukiwaambia walete ushahidi wanaingia mitini.Katega anasema Eden ingekuwa Iraq dunia nzima tungeenda kutembelea.

Hivyo basi Katega anasema dunia inatakiwa ijue sisi ndo waanzilishi wa kila kitu, tumevumbua moto, tukavumbua chuma, tukavumbua kuandika, hata oparesheni za uzazi zimeanzia Afrika, kilimo na ufugaji ni sisi, hata teknolojia ya ujenzi tumevumbua sisi. Ujenzi wa Piramidi za Giza pale Misri bado zinawachanganya wazungu mpaka kesho. Mijengo imepandishwa zaidi ya miaka 5,000 iliyopita lakini hadi leo bado ni tishio la dunia. Piramidi moja lina urefu wa mita 147 kwenda juu sawa na jengo lenye ghorofa 48, jengo hilo limetumia mawe milioni 2 na laki 3, mawe yenye uzito wa wastani wa tani 2 mpaka tani 5 na lile la mwisho kama juu kama kifuniko ni tani 50. Unaambiwa mpaka leo mainjinia wa ujenzi duniani wameshindwa kuelewa ni tekinolojia gani walitumia hao Mafarao. Kuna waafrika tena wasomi wanaamini zilijengwa na waisrael wakiwa utumwani na wakati yamejengwa baba yao Ibrahimu hajazaliwa. Ibrahimu alizaliwa 1775 BC na wakati piramidi piramidi ya kwanza imejengwa 2250 BC.

Baadaye hao wazee wetu walianza kusafiri kutoka Afrika Mashariki na kuelekea kona zote za Afrika. Waliingia Congo, Kenya, Uganda, Ethiopia na kugota Misri, wenginine wakaelekea Zimbabwe, Ghana, Morocco, Mauritania, Afrika yote ikajaa waafrika. Wakakaa kwa miaka milioni nne wakiijenga Afrika. Wakati huo mabara mengine hayakuwa na watu. Wakaanza kutoka nje ya Afrika, wakaingia China, India, wakasambaa Asia na Ulaya yote. Bahati mbaya waliokwenda kwenye milima ya Cocasian huko Asia walinasa kwenye baridi kali na barafu kwa miaka 9000 bila kuona jua, na kupoteza melanini na kuwa wazungu. Kwahiyo mzungu ameanza kuonekana duniani miaka 7000 mpaka 8000 huo ndo umri wa Adam kwa mujibu wa thiolojia. Hivyo sisi tulikuwepo kabla ya Adam. Hata mtu wa kwanza kuishi Marekani ni mwafrika kutoka Morocco wala siyo mhindi mwekundu. Prince Katega II anasema Mungu asingekubali kuwaweka watu wake kwenye shida, aliwaweka Afrika kwenye kila kitu, ardhi yenye rutuba iko Afrika, madini ya kila aina yako Afrika, mafuta ya kila aina yako Afrika na siyo huko jangwani na kwenye baridi, matetemeko na vimbunga. Hata hilo jangwa la Sahara halikuwepo anasema Prince Katega II.

Sasa basi wazungu nao walivyofika Misri walishangazwa na ustaarabu walioukuta pale. Watafiti wa Ugiriki walioishi Misri kwa miaka 50 mpaka 60 akiwemo Aristotle na Pythogarus yule anayetamba kuvumbua hesabu na wakati ndizo zilitumika kujenga yale mapiramidi, walipeleka taarifa kwa mfalme wa Ugiriki kuhusu ustaarabu walioushuhudia huko Misri. Wakakiri kwamba hawa watu wana Mungu na pia wana mahusiano ya ukaribu na ndugu zao walioacha miili yaani mizimu ndo maana wana nguvu kubwa. Mfalme Ptolemy I Soter akaona dawa ni kuwatenganisha hawa watu hiyo asili, mwaka 320 BC aliingiza sanamu lake kwenye mahekalu yote ili wamuabudu yeye, walipogoma akayafunga yote na kubeba nyaraka zote na kuzipeleka kwenye maktaba ya Alexandria, ambayo baadaye ilichomwa moto na warumi enzi za utawala wa Julius Caesar. Na huo ndo ukawa mwisho wa ukuu wa mwafrika.

Prince Katega II anakwambia wasingetuvamia leo dunia ingekuwa juu sanaa,hizi simu nadhani tungeisha tengeneza toka miaka ya 1500 huko, maana hawa mizimu waliisha design mpaka ndege, kuna vitabu vimeandika maajabu yaliyofanywa na mizimu ya kale, hawataki vijulikane.

Lazima tumjue mzungu kama adui na si mfadhili anasema Prince Katega II anayeishi nchini Uingereza. Mtu aliyekupiga na kukutenganisha na Mungu wako kwamba ni mshenzi na kusema usimuite Ngai, Imana, Kyala, Nguluvi, Mulungu badala yake umuabudu Yahwe, Allah na God hawezi kuwa mfadhili, mtu aliyevunja ule ushirikiano wetu wa kumsaidia kijana aliyetaka kuoa kujenga nyumba kulipa mahari na sherehe ya kuoa, siku hizi tunachangia chakula na vinywaji tu na kuacha kijana kuolea kwenye nyumba ya kupanga hawezi kuwa mfadhili, mtu anayeziita nchi zetu third world countries na wakati Mungu aliumba dunia moja hawezi kukufadhili kitu, mtu aliyetupeleka mateka kwa miaka mia saba na kutufanyia ukatili wa kutisha hawezi kukufadhili kitu, mtu anayetudai kwa riba kubwa na wakati alitakiwa atulipe fidia kwa damage aliyotufanyia mpaka Afrika ikawa na umaskini wa kunuka ndani ya utajiri wa kutupwa hawezi kukufadhili kitu huyo. Huyo ni adui. Adui yako muombee njaa, adui yako mmalize ni maneno kuntu ya wahenga kuwaamsha waliolala.

Hata hao Freemansonry siyo wachawi kama tunavyofikiria. Katega anasema ni kikundi cha watawa 9 wa kifaransa kilichoanzishwa 1330 AD wakafungua kitabu cha maandiko ya siri kilichoandikwa na wataalam wa Misri wale waliojenga yale mapiramidi ya Misri. Walikuta siri zote kama wataalam walivyopunguza uzito wa jiwe la tani mbili na kulipandisha juu, maana ya michoro na maumbo, ndo maana leo wanatisha kwa utajiri.

Prince Katega II ananifurahisha sana kwa jinsi anavyofikiri tofauti kwa kila jambo. Hata kuhusu kifo, anasema binadamu hafi, anaacha mwili kwa sababu kilichoumbwa na Mungu hakifi. Lugha za, “Marehemu apumzike kwa amani,” “Kifo ni kazi ya Mungu,” “Sisi tulimpenda lakini Mungu kampenda zaidi,” “Aliyekupa wewe ndo kaninyima mimi,” hakubaliani nayo hata kidogo. Anasema kama kifo na kuugua ni kazi ya Mungu basi kumpa dawa mgonjwa ni kazi ya shetani. Mungu si mjinga kiasi hicho. Kwamba mtu anamchoma mke wake kwa magunia mawili ya mkaa mpaka kuwa majivu halafu waombolezaji wanasema ni kazi ya Mungu, loh! Mungu kweli aue kiumbe chake alichokiumba? Ni sawa na wewe ujenge nyumba yako nzuri halafu uibomoe. Hivi kweli inawezekana? Anayeweza kufanya hivyo ni serikali tu. Hata habari za Gharika Katega anasema ni za kiroho zaidi ya kihistoria. Tembo saba waingie kwenye Safina, wajisaidie humo miezi na miezi, hali itakuaje? Kwanza anakwambia ni Mungu gani anaweza kuua mpaka wanyama wasiokuwa na dhambi?

Prince Katega II anasema Mungu hana ubaguzi wa kumpa yule na kumnyima huyu kwa sababu yeye si muislamu, wala mkristo, wala mbudha, ndo maana habagui, hata Yesu hakuwa mkristo, alikuwa myahudi. Kumbe yeye ni Mungu wa utaratibu. Mungu ni sayansi na teknolojia yake ni asili. Kabla hujasema Mungu amekunyima unatakiwa ujiulize umetoa kafara ngapi? Je unamahusiano ya uhakoka na vitu vyote alivyoviumba Mungu kuanzia watu walioacha miili, wenye miili na wasiokuwa na mili, nyota, mwezi, madini, wanyama, ardhi, mawe, wadudu, mafuta na maji? Usione watu wanawasha mshumaa wakati wa maombi ukadhani wanacheza, ipo nguvu katika nta, usione watu wanafukiza ubani ukadhani ni ushirikina, kuna nguvu katika ubani, usione watu wanavaa pete ya dhahabu na almasi ukadhani ni urembo tu kuna nguvu katika madini, usione watu wanatoa kafara ukadhani ni wachawi kuna nguvu katika kafara, usione watu wanavunja nazi njia panda na mambo kutendeka ukadhani ni washirikina, kuna nguvu katika mimea, usione watu wanaangamia ukadhani wanapenda ni kwa sababu hawana maarifa. Fumbua macho! Usione mwezi kuandama ukachukulia poa, kuna nguvu katika muandamo wa mwezi, kama mwezi unasababisha kupwa na kujaa kwa bahari, unafikiri hauna kitu katika mwili wako ambao robo tatu umeumbwa kwa maji? Usiishie kusema tu jamaa kachanganyikiwa kwa sababu ya mwezi mchanga, nenda mbele, kuna jambo unatakiwa kufanya wakati wa mwezi mchanga, wazungu wanashindana kwenda mwezini kwa sababu wanaijua siri, waislamu hawafungi wala kufungua bila kuona mwezi, habari za kuzaliwa kwa Yesu zilifika dunini kupitia nyota.

Ibaada ya hija na kafara ni nyenzo muhimu katika kufanya maombi yenye nguvu ndio maana dini za kigeni zimetupiga pini. Tunaambiwa kutoa kafara ni ushetani na wakati baba yao wa Imani Ibrahimu alitoa kafara, kuwasiliana na mizimu yetu tukaambiwa ni dhambi na wakati wao mizimu yao wanawaita watakatifu, tumeambiwa kutumia mitishamba ni dhambi ili watuuzie dawa zenye kamikali za kutuua taratibu, wamesema kuoa wake wengi ni dhambi, mke mmoja mpaka afe na wakati baba yao wa hekima Suleman alikuwa na wake 700 na wa nje 300, tumeambiwa tukitaka kufanya hija basi twende Maka na Jerusalemu na wakati Prince Katega II anasema hija yenye nguvu hufanywa kwenye makaburi ya mizimu yenu na si mizimu ya wazungu na warabu. Hivyo anasema basi kabla ya kwenda Maka na Yerusalemu tuanzie kuhiji kwa wazee wetu, kwa sababu sisi ni wafrika kabla ya kuwa waislam ba wakristo.

Kuna mkushi mmoja anaitwa Kissendi Nyanda, yeye anasema dini ndo zimechangia watu kuwa wavivu kwa sababu imeandikwa ombeni chochote kwa jina langu nanyi mtapokea, matokeo yake mahekalu yamejaa kondoo wenye umaskini wa kunuka badala ya kwenda kupiga kazi. Ndiyo maana Prince Katega II anasema tuvisome hivi vitabu vitakatifu tukiwa na fikra nje ya box. Hapa napo kuna hoja. Ujumbe kama, “Ni rahisi ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuingia mbinguni” umewafanya kondoo wengi kuuchukia utajiri na kujifia maskini, ujumbe kama, “Samehe saba mara sabini” umepelekea kondoo wengi kutenda maovu wakiamini kusamehewa, ndiyo maana wezi wengi wana majina mazuri na waliapa kwa Biblia na Kurani, una jina zuri la kidini lakini mlevi sugu wewe, changudoa wa mji wewe, mtukanaji mashuhuri wewe, mwizi sugu wewe, mchepukaji maridadi wewe, msengenyaji shupavu wewe.

Hizi imani za kuwalinda wezi ndo Prince Katega II anazitilia mashaka kama kweli zimetoka kwa Mungu. Anasema ndo maana Hitler aliwanyosha wayahudi waliojifanya taifa teule la Mungu.Prince anakwambia hakuna watu washenzi kama wayahudi,hawa ndo walianzisha kodi duniani, hawa ndo wamiliki wa media duniani na wametumia media hizo kuendesha propaganda kwa sababu he who controls the printed page controls the thinking of the age, hawa ndo waanzilishi wa hizi video na picha za ngono, hawa ndo walisababisha Marekani kurusha mabomu ya nyuklia kule Nagasaki na Hiroshima Japan ambayo madhara yake yapo hadi leo
Prince Katega II anasema wayahudi walizamisha meli ya Marekani na kutumia media kudanyanya ulimwengu kipindi cha vita ya pili ya dunia kwamba Japan ndo imezamzisha meli. Revange ndo mabomi yale.

Mtu anayetuma nyuki kuwauma wazungu tu anaitwa mchawi, mtu anayetuma radi kumlamba adui bila kudhuru wengine anaitwa mchawi, mtu anatibu mfupa uliovunjika akiwa mbali anaitwa mshirikina, mtu anaruka angani kwa ungo kwenda kutibu mgonjwa anaitwa mchawi, hivi kati ya mtu aliyejifungia maabara na kutengeneza virusi vya ukimwi na hao niliowataja hapo juu nani mchawi? Vipi hao wanaorusha hizo ndege za kivita kuua mamilioni ya watu wasio na hatia? Wapi umeishasikia ungo umeua watu kumi kwa wakati mmoja? Wazungu wanaangalia future yetu wataimalizaje, ndo maana wakatengeneza ukimwi, ebola na sasa wameleta GMO.

Ni wakati wa Afrika kuamka anasema Prince Katega II. Nguvu ya asili, bado ipo, tunauwezo wa kurudi juu ni suala la kuamua tu. Leo hii China ni superpower kwa sababu hawakuruhusu dini yao kurufugwa, hakuna mchina anayeitwa Kalimanzira. Japan wako juu kwa sababu hawakuruhusu dini yao kuguswa. Hakuna kilichopotea, kama ni miti ni ileile, mizimu ipo, nyenzo zote tunazo, kakakuona ni wale wale, nyuki bado wapo na tuvitumie katika kurudisha ukuu wetu. Ni magonjwa mangapi yameshindikana hospitalini lakini yamepona kwa waganga wa jadi? Hatuhitaji kutumia hata senti tano kununua dawa za kizungu.

Prince Katega II ana mengi sana sema muda hautoshi kuyaeleza yote. Mtafute kwa Whatsapp +447404966955 muhojiane, yeye anasema, huki ni kipindi cha kuuliza maswali na kuhoji majibu, tumeingia katika acquarian age, new age. Lazima tufikiri kwa nini Yesu amefanywa mzungu na hali tunauhakika mahali pale panapoitwa Israel hakukuwa na wazungu? Hao akina Nyetanyau ni watu wamegawiwa tu ardhi hapo karne ya 19, hata Biblia inajieleza wazi watu wote walikuwa weusi, hata mke wa Musa alikuwa mweusi. Marco Angelo ndo alichora kila kitu kuwa cha kizungu kwa amri ya Pope Yudas wa 6, karne ya 16. Alimchora Yesu Mzungu na wanafunzi wote wazungu ndo tukaanza kuaminishwa mkombozi wetu ni mzungu. Mzungu si mkombozi, mzungu ni colonizer na stop adoring a white man anasisitiza Katega.

Hivi kweli Pilato angeweza kumhukumu mzungu mwenzie yaani afe? Thubutu. Hata moto wa milele haupo, Mungu hawezi kuumba moto kuteketeza viumbe vyake. Hata jehanam haipo jamani.

Huyo ndio Katega, mwana wa mfalme ambaye nilikwambia unatakiwa kuwa na utulivu wa akili kumuelewa. Unaweza kudhani ni mpinga dini la hasha, kwanza ni mkristo safi kabisa, amezaliwa katika familia ya kikatoliki, akasoma seminari na ameokoka mwaka 1993 katika kanisa la Mtikila Full Salvation Church ndo maana hata siku ya mazishi ya Mtikila yeye ndo alikuwa MC.

Katega anajiita mkristo anayejitambua, an African Christian. Anachokifanya ni kuwatahadharisha wakristo na waislamu na wengine wanaofuatilia maandiko wasichukulie zile hadithi ndani ya Biblia na Kurani kama matukio ya historia bali mafundisho ya kiroho kwa njia ya visasili, kwa hiyo ukisikia Mungu kateketeza Sodoma na Gomora si kwamba ni tukio halisi, kwamba Mungu akaleta Gharika siku 40 si kweli, kwamba Mungu akavuruga lugha za kule babeli as if aliwaogopa watu aliowaumba, kwamba Musa akapiga maji bahari ikagawanyika wakapita waisrael na kuwaua Wamisri wote, kwamba Mungu ameandaa moto wa milele, ateketeze watu wake? Mungu ni wa upendo bwana. Kuchukulia haya mambo literally Prince Katega II anasema ni kumdhalilisha Mungu. Eti Mungu alimuumba Adam peke yake na wakati kwa wanyama kaumba jike na dume, kwa hiyo anajuta, ooo si vyema huyu mtu awe peke yake, yaani kama vile Mungu alijisahau na kujuta baadaye halafu akamchomoa mwanamke kwenye ubavu wake, kwahiyo Mungu alisahau kumuumba mwanamke? Mungu hawezi kumdhalilisha mwanamke kiasi cha kumuwekea kwenye levo ya nyoka. Hata habari za Yesu kuhutubia wanaume elfu 5 bila kuhesabu watoto bila kipaza sauti inawezekanaje? Kwamba wana wa Israel walitembea Jangwani miaka 40 wakila nyama choma ya Kware na kachumbali bila mboga nyingine, halafu wako jangwani na mifugo je ilikula mchanga?

Nimalizie kwa ahadi niliyoitoa maana ahadi ni deni. Nilisema ntakupa jibu alililonipa Prince Katega II kuhusu Kurudi kwa Yesu. Prince Katega II alisema kwa mujibu wa Biblia ukiisoma vizuri, Yesu anasomeka akisema kwamba kizazi hiki hakitapita kabla sijarudi, lakini Prince Katega II anasema kiliishapita, Yesu anasema kabla hamjamaliza kuzunguka miji ya Israel ntakuwa nimeishafika lakini tayari wamefika mpaka Tanzania, alisema wapo ambao hawajaonja kifo kabla sijafika lakini wameisha kufa wote.

Haya yote niliyoandika kutoka kwa Katega ni sawa na tone la maji ndani ya bahari,ukitaka mengi zaidi mtafute.

Asanteni.