WAKATI leo zimesalia siku 12 tu kufanyika kwa uchaguzi mkuu katika nchi ya Tanzania iliyoko Afrika Mashariki, vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani vinazidi kushamiri. Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, unatarajia kufanyika nchini kote Okboba 25 mwaka huu.
Vitendo vinavyoendelea kushamiri ni pamoja na lugha chafu, matusi, kauli za kudhalilisha pamoja na matamshi yanayochochea chuki, vurugu, mafarakano, udini na ubaguzi wa aina mbalimbali.
Wakiongea kwenye mdahalo unaorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, Jijini Dar es Salaam, baadhi ya Watanzania walioshiriki wanasema, makundi yayoongoza kwa kufanya vitendo hivyo ni pamoja na baadhi ya wanasiasa wanaogombea nafasi tofauti za uongozi, wapambe wao pamoja na waandishi wa habari vya vyombo mbalimbali vya hapa nchini.
Nani anatoa kauli za uchochezi?
Kwa mujibu wa wananchi hao, wanasiasa na wapambe wao wamekuwa wakitoa kauli hizo zinazochochea fujo wakati wa kampeni, kwenye mitandao ya kijamii na hata kwenye mikusanyiko isiyo rasmi.
Licha ya wanasiasa, washiriki wa mdahalo huo wanasema baadhi ya wana habari, wamekuwa wakichochea fujo kupitia habari wanazoandika.
Baadhi ya waandishi wanashabikia chama tawala CCM wakati wengine wanaunga mkono vyama vya upinzani na katika kuandika habari, wanaegemea zaidi upande wanaouunga mkono badala ya kuongozwa na maadili ya taaluma yao kusimama katikati, wanasema baadhi ya washiriki wa mdahalo huo.
Hiyo ni hatari, washiriki wa mdahaho huo wanaonya. Wanafafanua kuwa ushabiki wa aina hiyo huo unawafanya wananchi kuamini kila kinachosemwa kwenye magazeti, televisheni ama redio hata kama si cha kweli.
âBaadhi ya vyombo vya habari vimewafanya watu waamini kwamba wagombea wao watashinda uchaguzi, wakati wanajua fika, hawana uwezoâ¦itakapotokea wagombea hao wakashindwa, wananchi hawataridhika na wataingia msituni na kuwa mwanzo wa machafuko,ââ anasema mmoja wa washiriki hao.
Wengi wa wachangiaji katika mdahalo huo, wanaitupia lawama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo kisheria na kwa mujibu wa katiba ndiyo inaratibu taratibu zote za uchaguzi kwa madai kwamba imeshindwa kudhibiti ipasavyo viasharia vya uvunjifu wa amani.
âKauli za uchochezi zinatolewa kila siku na wanasiasa, NEC inakaa kimya, inashindwa kukemea kwa sababu haiko huru,ââ anasema mmoja wa wachangiaji hao.
Licha ya kufumbia macho vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani, NEC pia inatuhumiwa kupendelea wakati inapokemea wanasiasa wanaovunja kanuni.
NEC haitendi haki katika kukemea vikundi na watu wanaotoa kauli zinazochochea fujo, wanasema baadhi ya washiriki wa mdahalo huo kwa nyakati tofauti.
Wapo wanasiasa ambao wanavunja kanuni hadharani lakini hawakemewi hata kidogo, wakati wengine wakifanya hivyo, NEC hutoa taarifa ya kuwakemea haraka, anafafanua mshiriki mmoja wa mdahalo huo.
Washiriki hao kwa kauli moja wanasema wana mashaka kwamba NEC ina nguvu na uhuru wa kusimamia uchaguzi kwa haki na usawa. Na hilo wanasema linatokana na katiba ya nchi inayotumika hivi sasa ambayo ina mapungufu chungu nzima.
Nini kifanyike kulinda amani?
Wachangiaji wengi wanakiri kuwa ulinzi wa amani katika taifa si jukumu la taasisi ama kikundi kimoja na badala yake ni jukumu wananchi wote.
Kwa hali hiyo wanapendekeza kila Mtanzania kusimama katika nafasi yake kuhakikisha amani inaendelea kudumu badala ya kutegemea NEC na Jeshi la Polisi kufanya hivyo.
Kuwadhibiti na kuwachukulia hatua kali wanasiasa wanaotoa kauli zinazochochea uvunjifu wa amani, ni njia ya pili inayopendekezwa kutumiwa ili kudhibiti hali hiyo kabla haijaliingiza taifa kwenye machafuko.
Tukatae kauli za uchochezi. Wagombea wanaotoa kauli zinazoashirikia kuleta uvunjifu wa amani, tuwakatae, mmoja wa washiriki anashauri. Wananchi tujufunze kusema hapana kwa wanasiasa wanaotoa kauli zisizofaa.
Waandishi wa habari na wahariri wao wanatakiwa kuchuja kila taarifa inayoandikwa badala ya kubeba kauli za wanasiasa kama zilivyo na kuzipachika kwenye vyombo vyao vya habari.
NEC ifanye nini?
Wachangiaji katika mdahalo huo wanasema ili uchaguzi mkuu wa mwaka huu uwe huru na wa haki, ni lazima Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC), Jaji Damiani Lubuva, asimamie kidete kuhakikisha haki inatendeka.
Amani ni tunda la haki. Kama haki hakuna, amani haiwezi kuwepo, anaonya mmoja wa washiriki hao.
Mshiriki mwingine anasema ni vema NEC ikatangaza matokeo ndani ya muda uliopangwa ili kuondoa hisia za kuwepo kwa njama za kuiba kura.
Matokeo yanapocheleweshwa, wananchi wanapata wasiwasi kwamba kuna njama za kuiba kura. Hiyo inatokana na uzoefu katika chaguzi zilizopita, anasema mmoja wa washiriki hao.
Recent Comments