Juma Issihaka, Mchambuzi.
Tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini Tanzania, uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka huu, unatajwa kuwa wa sita kufanyika, kukadiriwa kuwa na mvutano wa kipekee kufuatia aina ya wagombea kutoka chama tawala CCM na chama kikuu cha Upinzani CHADEMA.
Kabla ya kuanza kwa vuguvugu la kuelekea uchaguzi huo, iliaminiwa kwamba, chama tawala kingelishinda kwa kishindo katika nafasi zote zinazowaniwa, hiyo ni kutokana na kile kinachotajwa kuwa serikali iliyoundwa na chama hicho imetekeleza vyema ilani yake katika kipindi cha miaka mitano ya duru ya kwanza ya utawala.
Imani hiyo ilitawala zaidi hususan kwa wafuasi wa CCM, ambao mara kadhaa wamedhihirika wakijipambanua kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati uliofanywa na Rais Dk. John Magufuli, katika duru yake ya kwanza ya uongozi.
Kadhalika kilichoaminisha zaidi ni umati wa watu wanaojitokeza kwenye misafara ya Rais Dk. Magufuli, kwa kiasi kikubwa ulijenga imani kuwa anapendwa kuliko yeyote nchini humo, kufuatia utendaji wake kudhaniwa umekidhi haja za wananchi wote.
Mtazamo huo ulibadilika baada ya vuguvugu la uchaguzi kupamba moto na CHADEMA kuanza kukaribisha watia nia kwa nafasi za Urais ambapo miongoni mwa wengi waliojitokeza alikwepo mwanasiasa mashuhuri ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Tundu Lissu.
Baada ya Lissu, kutangaza nia ya kuwania urais Tanzania kwa tiketi ya CHADEMA, zilishududiwa shangwe za aina yake kwa wananchi, kupitia mitandao ya kijamii wakionyesha uhitaji wa huduma yake katika nafasi hiyo.
Kadhalika shangwe hizo zilinoga zaidi baada ya mwanasiasa huyo mashuhuri kutangaza uamuzi wake wa kurejea nchini humo, tangu miaka mitatu iliyopita ambapo alikuwa nchini Ubelgiji kwa matibabu, kufuatia kushambuliwa na wasiojulikana Septemba 7, mwaka 2017.
Nguvu ya Lissu
Tangu kuingia kwa serikali ya Dk. Magufuli, madarakani Lissu, amepata umaarufu mkubwa katika siasa za nchi hiyo kwa kutosita kuikosoa serikali wakati wote.
Lissu, ndiye mwanasiasa wa upinzani aliyezua gumzo na kuonekana kuitikisa serikali kufuatia matamko mbalimbali ambayo amekuwa akiyatoa kukosoa utendaji wa Dk. Magufuli.
Pamoja na mambo mengine mwanasiasa huyo, amekuwa akilaani utendaji wa serikali hiyo, kwa kile anachokiita inaminya misingi ya Demokrasia kwa kutoruhusu vyama vya upinzani kutumia nafasi zao kutekeleza haki yao ya kufanya mikutano ya kisiasa.
Kwa mujibu wa Lissu, serikali ya Dk. Magufuli pia, imekuwa kaburi la vyombo vya habari kwa maana havipewi nafasi ya kutekeleza wajibu wao kama sauti kwa yale yaliyofichikana na badala yake anavitumia kumnadi kwa sifa za utendaji bora.
Mwenendo huo wa Lissu, umempa umaarufu na imani kubwa kwa miongoni mwa wafuasi wa vyama vya upinzani nchini humo, hata wasiopenda utendaji wa serikali iliyopo madarakani.
Katika kipindi hicho Lissu, amekuwa akikumbwa na shuruba kadhaa ikiwemo kushikiliwa na Vyombo vya Usalama nchini humo, akidaiwa kuwa ni chanzo cha uchochezi na mihemko inayoweza kusababisha vurugu kwa wananchi.
Kadhalika mwanasiasa na mwanasheria huyo nguli, alijizolea umaarufu na wafuasi zaidi baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana eneo lililo karibu na lilipo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo inaaminiwa kuwa limezungukwa na ulinzi wa kutosha.
Mitazamo ya wapinzani nchini humo na hata kauli za Lissu, mwenyewe zimekuwa zikielekeza tafsiri kuwa shambulio hilo dhidi yake limetekelezwa na serikali ya Dk. Magufuli baada ya kumuona machachari kuikosoa.
Pia Lissu, anatajwa kuwa na ukaribu na Mataifa mengi Duniani ukilinganisha na Magufuli, tangu alipoingia madarakani kuiongoza nchi hiyo.
Nguvu ya Dk. Magufuli
Katika kipindi cha miaka hiyo, Dk. Magufuli, pamoja na mambo mengine amefanikiwa kutekeleza miradi mingi ikiwemo uboreshaji wa huduma za jamii kama afya, elimu bure, kusimamia nidhamu ya watumishi wa serikali.
Pia amefanikiwa kujenga miradi ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Bwala la kuzalisha Megawati 2,115 za umeme, usambazaji wa umeme vijijini kwa zaidi ya vijiji 9,000 na huduma za maji safi na salama, ambayo yalianishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM, mwaka 2015.
Kadhalika Dk. Magufuli, anayo nguvu zaidi ya kutumia dola kuendelea kubaki madarakani kwani anayo nafasi kubwa ya kunadi sera zake kabla hata ya mchakato huo kutangazwa rasmi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Imedhihirika katika ziara na mikutano yake mbalimbali amekuwa akiweka bayana yale mazuri yaliyofanywa na serikali yake kwa kipindi cha miaka mitano.
Pia mwanasiasa huyo ambaye ni Mtaalamu wa Kemia, amejizolea wafuasi kutokana na kuzichanga vyema karata zake kuelekea uchaguzi mkuu, kwani amefanikisha kukuza uchumi wa nchi hiyo na kutajwa kuwa na uchumi wa kati daraja la chini kwa kipindi cha miaka mitano lengo ambalo lilitarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 10.
Pia mbinu alizotumia kukabiliana na janga la Covid 19, ambapo kwa mujibu wa mamlaka za nchi hiyo, ugonjwa huo haupo tena na kwamba wako salama, hata Watalii wameanza kupokelewa huku shule, vyuo na shughuli mbalimbali zikiendelea.
Hata wakati wa mapambano dhidi ya corona Dk. Magufuli, aliruhusu wananchi kutoka nje kujitafutia ridhiki zao, jambo ambalo ndio iliyokuwa kiu ya Watzania wengi hivyo walimsifu na pia kuishinda vita hiyo kwa kumshirikisha Mungu.
Hofu ya Wapinzani nchini Tanzania
Mara kadhaa vyama vya upinzani vimekuwa vikieleza hofu yao ya kupata ushindi kwa nafasi ya urais kutokana na kile wanachodai kuwa utendaji wa tume hauzingatii haki.
Kinachozusha hofu zaidi ni kwamba, uongozi wa NEC unaundwa na Rais aliyepo madarakani ambaye ni Dk. Magufuli, Je, tume hiyo itakuwa tayari kumuangusha aliyewapa nafasi za kuiendesha na pengine kama Magufuli, ndiye aliyemteua kiongozi wa tume atashindwa kumuagiza kufanya figisu kumpa ushindi hata kura zisipotosha?
Kwa misingi wa hoja hizo wanasiasa wa vyama vya upinzani nchini humo, ndio maana wamekuwa wakidai uwepo wa tume huru na ya haki ili kuondoa malalamiko yote wakati wa uchaguzi.
Kadhalika wamekuwa wakilalamika juu ya utendaji wa vyombo vya habari nchini humo, kutojihusisha zaidi na habari zao na vimejikita kuandika mazuri kuhusu CCM.
Kwa mujibu wa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Mchungaji Peter Msigwa, vyombo vya habari nchini humo vimekuwa vikiandika zaidi masuala ya CCM, na kuonekana kuhofu kuandika kuhusu vyama vya upinzani.
Hata hivyo madai hayo ya Mchungaji Msingwa, yalijibiwa na Baraza la Wahariri nchini humo (TEF), kwamba watatekeleza wajibu wao kwa kufuata misingi ya sheria, miiko na maadili ya taaluma zao na hawatajihusisha na kuandika siasa za matusi na kejeli kwani zinachochea vurugu na uvunjifu wa amani nchini humo.
Hali ya kisiasa kuelekea uchaguzi Tanzania
Kuelekea mchakato wa uchaguzi mkuu, nchini humo Tanzania imekuwa ikilalamikiwa kutokuwa na Demokrasia na uhuru wa kujieleza hali inayosababisha kuibuka kwa joto kali linaloweza kuchafua amani ya nchi hiyo.
Mmoja wa wanahabari wakongwe nchini humo, amebainisha kuwa kuzuka kwa Watanzania wengi wanaoituhumu serikali kufanya ubepari kupitia mitandao ya kijamii, kumetokana na kuminywa kwa uhuru wa wenye wajibu wa kulisemea hilo.
Anaeleza âukimnyima mwenye wajibu kutekeleza majukumu yake mfano vyombo vya habari, wataibuka wengine watakaoutekeleza wajibu huo bila taaluma hivyo kuvunja sheria, kanuni na maadili ya kazi hiyo, ndio maana mitandao ya kijamii kwa sasa inatumika kama jukwaa la kukosoa na matusi,â alifafanua mwanahabari huyo.
Hata hivyo hali ya siasa nchini humo, pia inakadiwiwa kuwa tulivu kutokana na serikali kuwa kimya dhidi ya Lissu, ambaye iliaminiwa kuwa angeshikwa na Vyombo vya Usalama mara baada ya kurejea nchini humo Julai 27, mwaka huu.
Kilichobeba imani za kukamatwa kwa Lissu, kinatokana na kwamba mwanasiasa huyo amekuwa akiituhumu serikali, kumshambulia na kuitaja kuwa inaongozwa kwa mfumo wa kibepari jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi hiyo kwani inaweza kuchochea vurugu kwa wananchi.
Mmoja wa Wahadhiri wa Masuala ya Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini jijini Dar es Salaam (TUDARCO), Dk. Lazzaro Swai, amechambua ukimya huo wa serikali kuwa ni mbinu za kutozua taharuki kuelekea uchaguzi.
Anafafanua kinachofanywa na serikali ya Tanzania ni kama kuizichanga vyema karata zake kuelekea uchaguzi kwani ingelishafa lolote kwa Lissu, ingetonesha kidonda kilicho kwa Watanzania na pengine kusababisha vurugu.
âKwa sababu mwanasiasa huyu alishambuliwa na tukio hilo lina utata mkubwa, endapo serikali ingefanya lolote wakati wa kurejea kwake ingetonesha kidonda cha wananchi na kuzua vurugu,â anaeleza Dk. Swai.
Nani atashinda uchaguzi huo, CCM/CHADEMA?
Licha ya vyama vya upinzani nchini humo kudhaniwa kufifia lakini mwamko uliojitokeza tangu kurejea kwa Lissu, vinakipa mashaka CCM kuwa uchaguzi huo hautakuwa rahisi kama kilivyoamini awali.
Kinachotarajiwa kutokea ni mgawanyo wa kura wa aina yake kwani pamoja na vyama hivyo pia ACT Wazalendo, kinatajwa kuchipuka na wafuasi wengi tangu kuungwa mkono na Maalim Seif Sharrif Hammad na Benard Membe, wawili hao wote ni zao la CCM.
Seif Sharrif Hammad, alikuwa mwanasiasa kutoka chama cha Wananchi (CUF), aliyewania urais wa Zanzibar na kuzua upinzani mkali dhidi ya Dk. Ally Mohammed Shein, katika uchaguzi wa mwaka 2015, na ameapa kurejea kuwania nafasi hiyo tena kwa tiketi cha chama chake kipya ACT Wazalendo.
Kadhalika Membe, ambaye ni mwanasiasa mashuhuri na Mwanadiplomasia aliyefutwa uwanachama wa CCM, baada ya kutuhumiwa kuingilia taratibu na miiko ya chama hicho, anawania kiti cha urais wa bara na ameapa kupata ushindi.
Pia chama kingine kinachotajwa kuchipuka kwa kasi ni NCCR Mageuzi, ambacho kimepata wanachama wengi hivi karibuni waliovihama vyama mbalimbali lakini chenyewe kinahofiwa zaidi Majimboni.
Kufuatia mgawanyo wa kura katika uchaguzi wa mwaka huu, unasababisha kuzuka kwa mashaka juu ya ushindi wa chama chochote, tofauti na ilivyoaminiwa kuwa CCM ingeshinda kwa urahisi.
Pamoja na mambo mengine CCM, ina nafasi kubwa ya ushindi kutokana na ukubwa wake, pia kujipanga na matumizi ya dola kubaki madarakani.
Katika ulimwengu wa siasa haikuwahi kushuhudiwa ushindani mkubwa katika uchaguzi unaohusisha wagombea wengi wa nafasi ya urais wakipambana na chama tawala, siku zote kitashinda tu.
Kungelikuwa na ushindani mkubwa zaidi endapo vyama vya upinzni nchini Tanzania vingeamua kukusanya nguvu, kwa maana kuungana kisha kumsimamisha mgombea mmoja wa urais atakayeshindana na mgombea wa CCM.
Kwanini upinzani haukuungana kama 2015?
Uchaguzi wa mwaka 2015, ulishuhudiwa upinzani mkali baina ya CCM na Vyama vya upinzani vilivyoungana na kuunda UKAWA, lakini havikufua dafu huku sababu inatajwa kuwa uwepo wa makachero wengi wa chama tawala ndani ya muungano huo.
Katika uchaguzi huo, waliibuka wanasiasa wengi wa chama tawala nchini humo, waliojiunga nao na wengine kupewa nafasi za kugombea Urais akiwemo Edward Lowassa.
Hadi sasa bado muungano huo, unadhani kwamba kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 kulitokana na baadhi ya waliowaamini, hawakuwa pamoja nao badala yake walijiunga nao kufanya figisu za kuwazubaisha.
Dhana hiyo inaaminiwa hadi sasa kwani takribani wanasiasa hao wote wa CCM walioungana na UKAWA mwa 2015, wamerudi katrika chama chao cha CCM.
Hivyo kilichopo sasa ni hofu kwamba huenda wakiungana na ukizingatia ACT Wazalendo tayari kimeamua kumsimamisha Benard Membe aliyefutwa uanachama wa CCM, kugombea Urais huenda akasababisha yaliyotokea 2015.
Mmoja wa viongozi wa juu wa CHADEMA, aliwahi kusema hawapo tayari yaliyotokea mwaka 2015, yatokee tena mwaka huu, hivyo uamuzi wao wa kupata mgombea Urais utafanywa nao kwa kuzingatia uwanachama wa mgombea huyo.
Kadhalika ingekuwa vugumu kwa NCCR Mageuzi, kuungana na umoja huo kwani baada ya kuvunjika ndicho chama kilicholalamika zaidi kuathiriwa na muungano uliotokea mwaka 2015, hivyo kwa namna yoyote isingewezekana kuungana.
Vivyo hivyo kwa CUF ambapo iliamini kuwa muungano huo, unaipa nguvu CHADEMA pekee na kiviua vyama vingine.
Chama pekee kilichokuwa kikishinikiza muungano ni ACT Wazalendo pekee, kutoka kwa mgombea wake Benard Membe, ambaye aliuaminisha umma kuwa ushindi wa upinzani utapatikana endapo vyama hivyo vya upinzani vitaunda nguvu ya pamoja, lakini hadi sasa jaribio lake linaonekana kupuuzwa.
Recent Comments