BAADHI ya wachambuzi wa masuala ya siasa nchini, wamesema hali ya siasa ya sasa ya wanasiasa wakongwe kuhamia vyama vingine, ni dalili ya kansa ya siasa na ujasiriamali wa siasa, ikiwemo uchu wa madaraka.
Aidha, wachambuzi hao wamewataka wananchi kutorubuniwa na hali ya hiyo na badala yake watumie fursa iliyopo ya kampeni kuwachambua wagombea na kuchagua kiongozi mwenye malengo na misingi ya utaifa.
Akizungumza na HabariLeo Dar es Salaam jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kwa hali ilivyo sasa ni vyema wananchi wakachagua kiongozi mwenye maono ya kujenga taifa, badala ya vyama vyenye uchu wa madaraka.
âLazima tutofautishe kati ya vyama vya siasa tulivyo navyo ambavyo vingi lengo lake ni kuchukua madaraka hata kwa muda mfupi tu na utaifa wetu ambao ni wa kudumu,â alisisitiza.
Alisema kwa hali inavyokwenda hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, vyama vingi vya siasa malengo yake ni kupata madaraka angalau hata miaka mitano kwa gharama yoyote ile.
âRai yangu wananchi wapime vyama hivi kwa malengo yake, wajiulize je, chama husika kina sifa ya kujenga utaifa au kupata madaraka. Hatma ya taifa hili iko mikononi mwa wananchi na si wanasiasa au vyama, vyama hivi vinakuja na kuondoka, lakini taifa liko palepale,â alisisitiza.
Alisema kwa sasa Tanzania ina takribani miaka 20 tangu ianze kutekeleza sera ya vyama vingi, lakini haijapiga hatua katika eneo hilo, kwani vyama vingi vinatekeleza siasa uchwara.
âHuu ni mwaka wa tano tangu siasa ya vyama vingi ianze kutekelezwa lakini ukiangalia hali ya siasa hii ni siasa uchwara tu, vyama hivi badala ya kuongelea masuala mazito ya taifa hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, wanachojadili ni kuchafuana ili kuvuta wanachama,â alisema.
Alisema wengi wa wanasiasa waliohama vyama vyao, wameonesha wazi kuwa hawana misimamo na kile wanachoamini na kipaumbele chao ni kupata madaraka.
âYupo mwanasiasa amehama vyama vitatu ndani ya wiki moja, sasa huku si ndio kutafuta madaraka kwenyewe? Alisema anasikitishwa na madai ya watu wengi kuwa kinachoendelea sasa nchini katika medani ya siasa ni ukuaji wa demokrasia na kusisitiza kuwa kamwe siasa si uongozi, bali ni ukombozi wa taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisema wanachama wote wa CCM waliohama chama hicho, wamedhihirisha kuwa hawakubaliani na misingi ya hekima na usawa ambayo chama hicho kimejijengea na kukimbilia mahali ambako fedha ndio msingi wa maendeleo.
Alisema sera ya CCM ni elimu, fursa, huduma za afya na matumizi ya rasilimali za nchi kwa wote mambo ambayo wote waliohama yamewakasirisha na kuamua kuhamia kwingine kunakoendana na matakwa yao.
Alisisitiza kuwa CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi, ambapo juhudi zinafanyika kuboresha maisha ya wananchi wote na si utajiri ubaki mikononi mwa wachache.
âInachukua watu kama akina Sumaye (Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye), ambao wamejipambanua na matajiri, walikuwa wanatafuta upenyo wa kutoka CCM,â alisisitiza.
Alisema kamwe umasikini hautoki kwa kumwaga fedha mitaani ili watanzania wauokote barabarani, bali kama alivyosema Mwalimu Nyerere umasikini huondoka kutokana na juhudi na maarifa binafsi ya mtu katika matumizi bora ya ardhi, mifugo na rasilimali nyingine.
âBwana Sumaye ametoka ndani ya chama akishikilia ngazi ya juu ya Uwaziri Mkuu kwa miaka 10, sasa anapolalamika juu ya madhaifu ya chama anamlalamikia nani? Alihoji Butiku.
Alisema yeye binafsi amefurahi kuwa watu hao wameondoka ndani ya chama na kuwafuata wenzao katika chama walichokuwa wakikitamani kwa miaka mingi.âNgoja waende tubakie very clean.â
Kwa upande wake, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Humphrey Polepole, alisema kuhama chama cha siasa ni sawa na kuhama dini kwa kuwa siku zote chama huongozwa na imani na mawazo fulani.
Alisema endapo mtu atahama chama hicho ina maana atakuwa ameshindwa kukubaliana na misingi iliyopo na anakoenda amekubaliana na misingi na mawazo ya huko. Hata hivyo, alibainisha kuwa kitendo cha mtu kuhama chama kipindi cha uchaguzi husababisha mashaka juu ya anachokiamini na msimamo wake.
âKwa mfano huyu aliyeondoka jana (Sumaye), alikuwa akinukuliwa alipokuwa CCM akisema kuwa anachukia ufisadi, na endapo chama hicho kitakumbatia mafisadi atakihama.Sasa CCM imejitahidi imechagua mtu asiye na nasaba za ufisadi, anayetuhumiwa akahamia kwingine, yeye ndio kaondoka huko kunakotuhumiwa kuwa na nasaba za ufisadi, msimamo wake sasa ni upi?â Alihoji.
Alisema kwa sasa Watanzania watashuhudia vituko vingi vya siasa, wanasiasa watajipambanua kwa mengi, lakini jambo la msingi ni kutambua Watanzania wanataka nini. Alisema siku zote vijana wanawatizama viongozi wa kisiasa kama mfano, huku akitolea mfano Yesu Kristo ambaye watu wengi wamemuani na ndio maana wanaamini katika Ukristo au Mtume (S.A.W) na mitume hao hawakuondoka ndio maana hadi leo wanaaminiwa.
âUkiwa kiongozi unayesimamia imani au itikadi fulani ujue vijana wanakutazama, sasa unapogeuka wanashindwa kukuelewa,â alisisitiza.
Juzi Waziri Mkuu mstaafu Sumaye, alitangaza rasmi kuhama CCM na kuhamia upinzani huku akidai amefanya hivyo ili kukiimarisha chama hicho. Pamoja na Sumaye pia Waziri Mkuu mwingine wa zamani, Edward Lowassa, naye alihamia Chadema mwezi mmoja uliopita na viongozi wengine kadhaa wa chama hicho.
Recent Comments