Recent Comments

Uchaguzi Marekani 2020:Biden kuchuana na Rais Trump kinyang’anyiro cha urais mwezi Novemba

By ObyMack David Aug 19, 2020
Joe Biden ameidhinishwa kuwa kiongozi wa mbio za kuelekea Ikulu dhidi ya Donald Trump

Joe Biden ameidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais atakayepeperusha bendera ya chama cha Democratic katika mkutano wa chama hicho huku kukiwa na hotuba za kusisimua kutoka kwa waliokuwa viongozi wa taifa hilo.

Wawili waliokuwa marais wa Marekani kupitia chama cha Democratic, Bill Clinton na Jimmy Carter, pamoja na aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje Colin Powell, wa chama cha Republican, wamemuidhinisha rasmi Bwana Biden.

Bwana Clinton amesema ofisi ya Rais Donald Trump imesababisha vurugu katika Ikulu.

Bwana Trump anamuongoza Bwana Biden katika kura ya maoni kabla ya uchaguzi wa Novemba.

Hii ni mara ya tatu kwa Biden kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais huku mwakilishi huyo wa chama cha Democratic akionekana kuwa katika kipindi cha madiliko makubwa ikizingatiwa kwamba kampeni yake ilionekana kuwa katika hatari ya kudidimia mnamo mwezi Februari.

Usiku wa pili wa mkutano wa chama hicho Jumanne, mada ikiwa ni masuala ya uongozi, Bwana Clinton alitoa hotuba ya kilele.

“Donald Trump anasema tunaongoza duniani,” Bwana Clinton alisema katika hotuba yake ya dakika tano iliyorekodiwa akiwa nyumbani kwake Chappaqua, New York. “Sisi ndio nchi pekee iliyostawi kiuchumi ambayo kiwango cha waliokosa ajira imeongezeka mara tatu.

“Wakati kama huu, Ikulu inatakiwa kuwa kitovu cha kila kitu. Badala yake ni kituo cha dhoruba. Kinachopatikana huko ni fujo na ghasia pekee.”

Kufuatia hotuba ya aliyekuwa mama wa kwanza wa taifa hilo Michelle Obama na Seneta Bernie Sanders Jumatatu, hotuba za Jumanne zililenga kuonesha wapiga kura vile chama cha Democratic ndio kilicho katika nafasi nzuri zaidi ya kurekebisha matatizo yaliyopo nyumbani na nje ya nchi.

Michelle Obama ameukosoa waziwazi utawala wa Trump akisema si rais anayewafaa Wamarekani

Bwana Powell alisema Bwana Biden ana maadili “niliyojifunza wakati ninakua huko South Bronn na nikiwa mwanajeshi”.

Alisema kwamba anamuunga mkono kama rais kwasababu “tunahitajika kurejesha maadili hayo katika Ikulu”.

Mwezi Juni, Bwana Powell – ambaye alihudumu chini ya uongozi wa Rais George W Bush – alimtaja rais Trump kama muongo na kumuidhinisha Bwana Biden.

Bwana Powell anajiunga na wanachama wengine wa Republican ambao wamemuidhinisha Bwana Biden. Usiku wa kwanza wa mkutano wa chama hicho, aliyekuwa gavana wa Ohio John Kasich ni mmoja kati watu kadhaa waliojitolea kuunga mkono chama cha Democrats.

Cindy McCain, mjane wa seneta wa chama cha Republican John McCain, pia alitarajiwa kuzungumza kuhusu urafiki kati ya marehemu mume wake na Bwana Biden.

Aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje John Kerry pia alihudhuria mkutano huo kwa njia ya video na kukosoa ungozi wa Bwana Trump.

Bwana Kerry aligusia uelewa wa Bwana Trump wa masuala ya kidunia akisema anafahamu kwamba “hakuna kinachoweza kutatuliwa bila kuunganisha taifa”.

Rais wa Marekani Donald Trump

Bwana Trump alikuwa na haraka sana ya kujibu wafuasi wenzake wa Republican wanaomkosoa na amekuwa akiendelea kumuonesha Bwana Biden kama kibaraka wa watu wa mrengo wa kushoto wenye msimamo mkali.

Sasa hivi rais yuko eneo la Arizona, alikosimama hivi karibuni akiwa katika ziara ya kampeni ya wiki moja ya majimbo muhimu sana katika kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu.

Kura nyingi za maoni zinaonesha kwamba Bwana Biden anaongoza, ingawa wiki za hivi karibuni, Bwana Trump amejitahidi kuziba pengo kati yao na uchaguzi pia bado una miezi kadhaa kabla ya kufanyika.

Mkutano wa chama cha Democtaric utaendelea Jumatato na Alhamisi, huku hotuba za kilele zikiwa ni kutoka kwa makamu wa rais Seneta Kamala Harris, mgombea urais wa chama cha Democratic 2016 Hillary Clinton na aliyekuwa rais wa Marekani, Barack Obama.

Mikutano ya chama hicho kwa usiku wa nne itakamilika kwa hotuba ya kukubali kuwa mpeperushaji wa bendera ya chama hicho kutoka kwa Bwana Biden.

Mkutano wa mwaka huu unafanyika kwa njia ya mtandao wenye hotuba zinazotolewa ama kwa njia ya moja kwa moja au iliyorekodiwa kutoka kila pembe ya Marekani kwasababu ya janga la corona.