SALVATORY NTANDU
KAHAMA
17/4/2021
Katika jitihada za kukabiliana na tatizo la uhaba wa madawati katika shule ya sekondari Ubagwe wilayani Kahama mkoani Shinyanga wadau wa maendeleo wametoa msaada wa madawati 92 yenye thamani ya shilingi milioni 5.5 ili kuboresha mazingira ya wanafunzi kujifunzia.
Msaada huo umekabidhiwa jana kwa mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha na mkurugenzi wa mikopo wa benki ya Posta Tanzania (TPB) Henri Bwogi ambapo alisema wametoa madawati hayo ili kutatua shida ya wanafunzi kukaa kwa kubanana hali ambayo inachangia wengi wao kutofanya vizuri katika mitihani yao ya kitaifa.
Alisema kuwa benki hiyo ilipokea ombi maalumu kutoka kwa uongozi wa shule hiyo kupitia ofisi ya mbunge wa jimbo la Ushetu,kuhusiana na ukosefu wa madawati  ambapo wamefanikiwa kuiunga mkono serikali kwa kuchangia madawati hayo 92 ambayo yamegaharimu zaidi ya milioni 5.
âTumekuwa tukirudisha fadhila kwa wananchi ambao benki yetu inawahudumia kwa kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo katika sekta za elimu na afya,tutaendelea kushirikiana na serikali na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza,âalisema Bwogi
Akipokea madawati hayo kwa niaba ya serikali mkuu wa wilaya hiyo,Anamringi Macha aliishukuru benki ya TPB kwa kurudisha fadhila kwa jamii kupitia faida wanayoipata na kuwaomba wawekezaji wengine kujitokeza kuchangia sekta ya elimu ili kuwajengea wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunzia.
âNiwahakikishe madawati haya yatatunzwa vizuri ili kuleta tija kama ilivyokusudiwa,kupitia hadhara hii niombe wadau wengine wa maendeleo kutuchangia katika sekta hii ya elimu ambayo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali hususani ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari,âalisema Macha.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Ushetu Michael Matomora alisema kuwa shule hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati 51 lakini kupita msaada huo utakuwa umemaliza tatizo hilo ambalo lilikuwa linawakabili kwa muda mrefu.
âHali ya taaluma itapanda kutokana na wanafunzi kuwa na mazingira mazuri ya kujifunzi,shule hii ni mpya inakidato cha kwanza na cha pili na msisitizo wetu ni kuhakikisha tunatatua kero zao,niwaombe wananchi kuendelea kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa ili vikikamilika serikali iweze kuvikamilisha,âalisema Matomora.
Mwisho.
Recent Comments