Wagombea 10 wanaoongoza katika kura za maoni za kumtafuta atakayewakilisha chama cha Republican katika uchaguzi mkuu wa Marekani wamenadi sera zao kwenye mdahalo wa kwanza ulioonyeshwa kwenye televisheni.
Miongoni mwa walioshiriki katika mdahalo uliorushwa na kituo cha televisheni cha Fox News ni bilionea Donald Trump ambaye kwa sasa ndiye mwenye nafasi nzuri zaidi ya kushinda, seneta Rand Paul wa jimbo la Kentucky, seneta wa Florida Marco Rubio na daktari Ben Carson. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wapiga kura walifuatilia kwa makini aliyoyasema mgombea Jeb Bush, ambaye ni kaka yake rais wa zamani George W. Bush na mwanae rais George H. W. Bush. Swali kubwa ni iwapo uongozi wake utakuwa na tofauti yoyote na uongozi wa baba yake na kaka yake.
Mdahalo wa jana usiku uliodumu kwa masaa mawili uliwapa nafasi wagombea kutoa maoni yao kuhusu sera mbali mbali kama vile uchumi wa nchi, siasa za mambo ya nje na usalama wa taifa. Pamoja na hayo, wananchi walipata fursa ya kutuma maswali yao kupitia mtandao wa Facebook.
Donald Trump aliombwa aelezee hoja yake, kwamba Mexico inatuma wabakaji na wahalifu wengine Marekani, na alishikilia msimamo wake. “Wanawatuma watu wabaya kwetu kwa sababu hawataki kuwalipia gharama za maisha yao wala hawataki kuwashughulikia,” alisema Trump. “Kwanini wahangaike wakati viongozi wajinga wa Marekani watawasaidia kufanya hivyo? Hicho ndicho kinachotokea kwa sasa, penda usipende.”
Nani kupambana na Hillary Clinton?
Wakati wapinzani wa Trump wamemkejeli mfanyabiashara huyo, wakisema yeye ni kama kichekesho ndani ya chama cha Republican, gavana wa jimbo la Ohio John Kasich, ambaye pia ni mgombea, amewataka wenzake wasipinge kila kitu ambacho Trump anasema, akiongezea kwamba Trump anathubutu kusema yale ambayo wengine hawayatamki. “Watu wamekasirika. Wamechoshwa. Hawaoni kwamba serikali yao inawatumikia,” alisema Kasich. “Kwa hiyo wale wanaotaka kumpuuzia Trump wanafanya kosa. Hata hivyo, yeye ana mapendekezo yake ya namna ya kutatua mamatizo, na wengine wana suluhu nyingine.”
Mbali na mada ya uhamiaji, wagombea waliwasilisha pia maoni yao juu ya makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani. Usalama wa ndani na mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi ni mada zilizozua mjadala mkubwa katika jukwaa la ukumbi wa Quicken Loans ulipofanyika mdahalo.
Atakayeteuliwa kugombea kwa tiketi ya Republican anatarajiwa kupambana na Hillary Clinton ambaye anapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda uteuzi wa chama chake cha Democrat.
Recent Comments