TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeshatangaza kuwa kampeni zitaanza rasmi Agosti 22 mwaka huu, tayari kwa wanasiasa kutangaza sera na kuwaeleza wananchi watawafanyia nini.
Bila shaka Watanzania watapenda kusikia namna maisha yao yatakavyoboreshwa baada ya kupata viongozi wapya, ikiwemo kuondokana na matatizo kama kupata maji ya uhakika, miundombinu ya barabara iliyo bora, umeme wa uhakika, kuondokana na matatizo ya ardhi na changamoto nyingine kadhaa.
Kwa uzoefu huu, ndio wakati wa wanasiasa kueleza ya ukweli na ya uongo. Ahadi zitatolewa nyingi sana tena wapo watakaothubutu kutoa na siku za kutekeleza ahadi zao. Kutokana na tabia ya wanasiasa kutoa ahadi hewa au za kwenye ndoto ni wakati wa wananchi kuhudhuria mikutano ya kampeni na kusikiliza kwa makini pamoja na kuuliza maswali, namna ya ahadi hizo zitakavyotekelezeka na si kwenda kushangilia bila kujua kilichozungumzwa.
Si wakati wa kwenda kwenye mikutano kufuata burudani za muziki na ngoma na kuangalia unavutiwa na mtu gani, bila kumtathmini vya kutosha na namna atakavyowavusha na kuwapeleka kwenye maendeleo ya kweli.
La kwanza kuangalia, wananchi watafute ilani za vyama vyote vya siasa na kuzisoma kwa makini na hasa katika maeneo yanayowahusu kuona jinsi ilani hizo zilivyoainisha jinsi ya kutatua matatizo yao.
Tunasema hivyo kutokana na kubaini wapo wanasiasa wasiofuata ilani za vyama vyao na kutoa ahadi za uongo, lakini pia vipo vyama vyenye kuandika ilani kama hadithi ambapo haielezi jinsi ahadi hizo zitakavyotekelezeka.
Unapoweza kusoma ilani za vyama vyote vya siasa itakuwa rahisi kuuliza maswali kwenye kampeni pamoja na kujua mipango ya chama husika katika kuwatatulia changamoto zinazowakabili na kupata maendeleo.
Huu si wakati wa kuwa na ushabiki wa kupenda mtu au chama fulani au kukubali kupandikizwa chuki ila hoja ndiyo iwe msingi wa kumchagua mtu. Si kila ahadi zinatekelezeka na baadaye wananchi ndiyo mnaoumia iwapo ahadi hizo hazitekelezeki.
Hivyo ni vema kuwa makini kuchambua ahadi hizo na kuona kama za kweli kwenye utekelezaji au ni sawa na ndoto za Abunuwasi. Sisi tunaamini msemo usemao âAkili za kuambiwa changanya na zakoâ hivyo si kila unachoambiwa unakubali bali tafakari, chambua kwa akili ulizopewa na Mungu na pale unapoona kuna uongo ni vema kuchukua hatua kwenye sanduku la kura.
Mnapaswa pia kutambua kuwa Tanzania inahitaji kuachana na wanasiasa wa kurudisha nyuma, wenye kuangalia maslahi yao binafsi na kukamua wananchi bali wapewe nafasi wale watakaoleta maendeleo na kuondokana na umasikini na si wale wa kujinufaisha.
Recent Comments