Recent Comments

WANAWAKE WAWILI MBARONI KWA UNYANG’ANYI WA PIKIPIKI MOROGORO. 

By Mussa Mathias Aug 14, 2024
Pichani ni Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama.

WANAWAKE WAWILI MBARONI KWA UNYANG’ANYI WA PIKIPIKI MOROGORO.

Gairo, Morogoro.

WANAWAKE wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro kwa madai ya unyang’anyi wa Pikipiki na fedha kwa kutumia silaha ya jadi aina ya nondo pamoja na panga.

Wanawake hao ni Farida Msafiri Charles (26) Mkulima mkazi wa mtaa wa Uchagani Gairo na Grace Robert Chiduo (24) Mkulima mkazi wa kitongoji cha Sambweti Gairo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama mesema tukio hilo lilitokea Agosti 13, 2024 majira ya saa 12 jioni ambapo wanawake hao walimkodi muendesha pikipiki ya abiria (bodaboda)  Ndoni Ndumwa John (32) Mkazi wa kitongoji Kichangani Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara.

 

Pichani ni Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama.

Alisema John akiwa na pikipiki yake yenye namba MC 936 DRZ aina ya Houjue nyeusi, kutoka kijiweni kwake Sunya Kiteto Manyara wanawake hao walimtaka awapeleke Sambweti wilayani Gairo.

Alisema wakiwa njiani kuelekea Sambweti Gairo, wanawake hao walimvamia kwa ushirikiano na vijana wengine wakiume wawili ambao walitokea vichakani na kumshambulia kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumnyang’anya pikipiki sh. 4000.

Baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo Jeshi la Polisi Wilaya ya Gairo kwa kushirikiana na Kiteto lilifanya msako mkali wa Watuhumiwa hao na kuwakamata wanawake hao wakiwa na Pikipiki hiyo pamoja na fedha.

Aidha Watuhumiwa wanashikiliwa katika kituo cha Polisi Gairo kwa mahojiano na watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Mwisho.