Wazalishaji wa Mbolea nchini wametakiwa kuzingatia ubora na kushirikiana na taasisi za utafiti ili kuzalisha mbolea zenye viwango vitakavyoendana na uhalisia wa udongo wa eneo zitakapotumika.
Pia wameelezwa kuwa ni marufuku kupeleka mbolea kwenye matumizi kabla haijapewa leseni kutoka Mamalaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (NFRA).
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, wakati wa kikao cha wadau cha kujadili mbolea ya Minjingu Chai kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Amesema ni muhimu kwa watengenezaji wa mbolea nchini kuzingatia maelekezo ya kitaalamu ili kuzalisha mbolea bora yenye viwango vitakavyoendana na mahitaji ya udongo wa eneo husika.
âWatengenezaji wa mbolea pia wanao wajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakulima na ziuzwe kwa bei rafiki kutokana na hali ya kipato cha wakulima nchini,â amesema.
Amesema ni budi kwa wazalishaji hao pia kuzingatia matakwa ya kisheria ikiwemo usajili wa mbolea hizo.
Kusaya amesema ili kuzalisha mbolea yenye viwango vya ubora unaotakiwa kulingana na udongo wa eneo itakapotumika ni muhimu kwa wazalishaji hao kushirikiana na taasisi za utafiti ambazo zina uelewa wa kina juu ya utaalamu huo.
âKatika hili kila mmoja anao wajibu wake hata Maofisa ugani pia wanatakiwa kutoa elimu kwa wakulima juu ya kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea,â amesema.
Amesema serikali imekuwa ikihamasisha matumizi ya mbolea katika shughuli za kilimo kutokana na kwamba uzalishaji katika sekta hiyo hutegemea zaidi mbolea.
Kusaya amesema kwa sasa kuna ongezeko kubwa la watu ambapo imesababisha kuwepo kwa mabadiliko ya tabianchi hivyo shughuli za kilimo zinahitaji mbolea ili kuzalisha.
Ameitaka TFRA kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uzalishaji mbolea Pamoja na kusimamia utengenezaji na uingizwaji wa bidhaa hiyo unaokidhi matakwa ya sharia na kanuni.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuendelea kuwekeza katika uzlaishaji wa mbolea nchini.
Amezitaja changamoto wanazokutana nazo wawekezaji katika sekta hiyo kuwa ni gharama kubwa za uwekezaji zinazopelea mbolea kuwa ghali, kuwepo kwa mifumo ya kisheria yenye utata na kukosekana kwa ushirikiano na watengenezaji wa bidhaa saidizi kama vifungashio.
âSerikali ipo makini kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa na kama mnavyofahamu kuwa awamu hii imejikita katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo utafika wakati mambo yatakaa vyema zaidi,â amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Dk. Stephan Ngilo, amewahakikishia wakulima upatikanaji wa mbolea kwa msimu wa mwaka 2020/2021 ambapo hadi sasa tayari walishaanza mipango ya upatikanaji wa mbolea ya kupandia inayotarajiwa kupatikana katikati ya mwezi huu.
Amesema mwaka jana mbolea iliyozalishwa ilikidhi mahitaji ambayo yalikuwa ni tani 586,604 na ziada ambapo ilipelekwa nje ya nchi.
Recent Comments