Recent Comments

WAZIRI MKUU MSTAFU WA TANZANIA EDWARD LOWASSA AFARIKI DUNIA.

By Mwafrika Feb 10, 2024

NA, ANKO G.

Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania Edward Lowassa amefariki dunia, akiwa anapatiwa matibabu jijini Dar es Salaam.

Tangazo la kifo cha Lowassa kimetangazwa Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango.

Katika tangazo fupi alilolitoa kupitia televisheni ya taifa, Mpango amesema kuwa Lowassa amefikwa na umauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

”Amefariki leo akipatiwa matibabu kwa ugonjwa wa kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu. Hayati Ngoiyai Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu tangu tarehe 14 mwezi Januari mwaka 2022”. Alisema Dkt. Mpango.

Alikuwa akipatiwa matibabu katika taasisi hiyo ya moyo kisha kupelekwa Afrika Kusini na baadaye kurudishwa tena katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete.

Lowassa alihudumu kama Waziri Mkuu wa Tanzania chini ya Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kwa miaka mitatu, toka 2005 mpaka 2008 alipolazimika kujiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza siku tano za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia hii leo.

Mwaka 2015 Lowassa alikihama chama tawala cha CCM baada ya kukosa tiketi ya kuwania urais kupitia chama hicho.

Alitimkia chama kikuu cha upinzani cha Chadema ambapo aliungwa mkono kugombea urais na vyama vilivyounda umoja wa upinzani wa UKAWA kwa wakati huo.

Lowassa hata hivyo alishindwa katika uchaguzi huo na aliyekuwa mgombea wa CCM John Pombe Magufuli. Lowassa alirejea CCM mwaka 2019.

Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 amefariki akiwa na umri wa miaka 70 na anaacha alama kama moja ya miamba ya siasa za Tanzania.