Kasi ya ustawi wa uchumi wa China imekuwa inapungua na masoko ya hisa yanaanguka duniani kote.
Jee pana hatari ya kuzuka mgogoro mwingine wa uchumi wa dunia? Mwandishi wetu Henrik Böhme anasema kinachotokea ni kuirekebisha kasi ya uchumi huo.
Mpaka sasa hakuna kikubwa kilichotokea .Mpaka sasa bado ni masoko ya hisa yaliyotikiswa. Ni kweli Bilioni zinateketea hapa na pale katika kila dakika moja kwenye masoko ya hisa duniani.
Lakini kutokana na vurumai iliyopo ambapo masoko ya hisa yametikiswa katika wiki za hivi karibuni, kuanguka kwa masoko ya hisa siyo jambo la kushangaza.
Ni kweli kwamba pamekuwapo habari mbaya kutoka China ambazo masoko ya fedha yamepaswa kuhimili mnamo wiki za hivi karibuni. Ikiwa China, yaani taifa kuu la pili kwa nguvu za kiuchumi duniani litatetereka,wawekaji vitega uchumi nao watagwaya. Lakini hiyo siyo sababu ya pekee ya kutokea vurumai tunazozishuhudia sasa.
Wasiwasi hautoki China tu
Zipo nchi nyingine zinazoinukia kiuchumi, zinazowatia watu wasi wasi.
Chukua mfano wa Urusi.Uchumi wa nchi hiyo umedhoofika kutokana na vikwazo vilivyowekwa na nchi za magharibi na pia kutokana na matatizo ya ndani. Au chukua mfano wa Brazil ambayo kama Urusi inategemea kuuza hasa bidhaa ambazo siyo za viwanda ili kuendesha uchumi wake. Na sasa kutokana na kupungua kwa mahitaji ya bidhaa hizo uchumi wake umeshuka.
Ni rahisi kuzilaumu nchi zinazoinukia kiuchumi. Sababu ni kwamba unomi wa kwenye soko la hisa ambao umekuwapo kwa muda wa miaka saba ilyopita umekuwa kimsingi unadumishwa na benki kuu za nchi.
Tokea mgogoro mkubwa wa kiuchumi uliosababishwa na kuanguka kwa benki ya Lehman Brothers ya Marekani, Benki Kuu ya Marekani na Benki Kuu ya Ulaya, ECB zimekuwa zinaingiza mabilioni ya Dola na Euro kwenye masoko kwa kuziweka riba katika viwango vya chini.
Lakini swali ni wapi fedha hizo zinapaswa kwenda?
Fedha hizo zinapaswa kuekezwa mahali fulani ili zilete faida na hasa ikiwa bima za pensheni na kampuni nyingine za bima zinataka kuona faida. Fedha hizo ziliekezewa katika kila aina ya hisa.
Ni ikiwa pana jambo moja la uhakika juu ya hisa ni kwamba wakati wote zinaweza kuathirika na ugeugeu wa soko. Na wakati mwingine ugeugeu huo unaweza kusababisha thamani ya hisa iteketee. Hivyo ndivyo mambo yalivyo.
Lakini kinachotokea sasa siyo muanguiko wa kwanza mnamo miaka ya hivi karibuni. Masoko wakati wote yanakuwamo katika hatari ya kukumbwa na vurumai kutokana na fedha za riba za chini sana.
Mwaka jana Soko la hisa la Ujerumani lilpoteza hadi pointi 8400 kutokana na hali ya wasi wasi juu ya uchumi. Lakini wasi wasi huo kwa kweli haukuwapo.
Soko la hisa la Ujerumani liliinuka tena.Kwa nini watu hawajiulizi, ila pale tu mambo yanapotekea katika nchi za kusini mwa dunia? Huu ni wakati wa kuyatafakari mambo vizuri.
Ujerumani yaani bingwa wa uuzaji wa bidhaa nje inauza asilimia 7 tu ya bidhaa zake kwa China. Ni kweli sekta ya viwanda vya magari imo katika hali ya wasiwasi nchini Ujerumani. Lakini wachunguzi wengine hawakubaliani na tathmini hiyo.
Nchi nyigine zimeathirika na kuanguka kwa bei ya mafuta na bidhaa ghafi.Lakini hiyo ni furaha kwa nchi nyingine.
Marekani ndiyo yenye suluhisho.
Ikiwa pana uvumi tu kwamba Benki kuu ya nchi hiyo inataka kupandisha kiwango cha riba,uvumi kama huo utatosha kusababisha wasi wasi katika nchi zinazoinukia kiuchumi.Sababu ni kwamba wawekaji vitega uchumi wanaiondoa mitaji yao kwa matumaini ya kupata faida kubwa zaidi nchini Marekani baada ya viwango vya riba kupunguzwa.
Lakini ikiwa mgogoro wa China utaukumbuka uchumi wa dunia, nchi za magharibi hazitakuwa tena na zana za kuziwezesha kujihami.
Recent Comments