MKOA wa Dodoma una fursa nyingi za kiuchumi na kijamii na fursa ya kwanza inatokana na jiografia yake ya kuwa katikati ya nchi.
Hali hiyo inawezesha mkoa huo kufikika kwa urahisi kutoka maeneo yote ya Tanzania, hivyo kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi ndani ya mkoa, mikoa jirani na nje ya nchi. Umbali wa kufika Dodoma kutoka Dar es Salaam ni maili 304, hadi Bukoba maili 616, hadi Musoma maili 579, hadi Kigoma maili 693, hadi Mtwara maili 674, hadi Songea maili 485, hadi Mwanza ni maili 442, hadi Mbeya maili 402, hadi Musoma 579, na hadi Sumbawanga maili 946.
UMWAGILIAJI
Fursa nyingine ya Dodoma ni kiwango cha maji ardhini kiko juu. Hali hii inawezesha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na umwagiliaji kuwa rahisi. Kilimo cha umwagiliaji kinafanyika vijijini na yapo mabonde kadhaa yanayotumika kwa kilimo cha umwagiliaji wa mazao mbalimbali, mfano mabonde ya Kikore wilaya ya Kondoa na Lumuma na Malolo wilayani Mpwapwa.
Katika maeneo hayo, wakulima hulima mpunga, maharage, mbaazi, kunde, mahindi, migomba na mbogamboga. Kilimo cha umwagiliaji pia kinafanyika pembezoni mwa mji wa Dodoma, ambako wananchi wanalima mboga mboga, matunda na majani ya mifugo na kuwauzia wakazi wa mjini Dodoma.
UFUGAJI WA MIFUGO
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma, Deogratias Yinza anafafanua kuwa fursa nyingine iliyopo Dodoma ni kuwepo kwa mifugo ya kutosha, kama vile ngâombe, mbuzi, kondoo na kuku. Lakini, mifugo hiyo haijatumika kikamilifu kuzalisha nyama na bidhaa mbalimbali kwa matumizi ya nyumbani na kwa kupeleka sokoni. Maendeleo ya kweli yatapatikana kwa kutumia kikamilifu mifugo hiyo.
Yinza anaeleza kuwa ufugaji wa kunenepesha mifugo, umekuwa ukifanyika katika wilaya za Bahi na Chamwino, ambako wafugaji wamekuwa wakihimizwa kuuza mifugo yao. Kwa mfano akiwa na ngâombe 2000, anahimizwa auze zibakie ngâombe 100. Aidha, Yinza anasema mbuzi kutoka mkoa wa Dodoma, wamekuwa wakinunuliwa kwa wingi na wafanyabiashara na kupelekwa Comoro na nchi za Arabuni, kama vile Dubai na Abu Dhabi.
UCHIMBAJI WA MADINI
Kwa upande wake, Afisa Maliasili wa Mkoa, Halifa Msangi anataja fursa nyingine iliyopo Dodoma kuwa ni madini. Kuna madini ya aina mbalimbali kama dhahabu, jiwe jeusi, shaba na rubi katika wilaya za Mpwawa, Kondoa, Bahi na Chamwino. Katika wilaya ya Mpwapwa, uchimbaji mdogo wa madini upo katika eneo la Winza. Winza ni moja ya maeneo 18 nchini ambako kisheria wachimbaji wadogo wana viwanja vya kuchimba madini.
Wanaohitaji madini katika eneo hilo, huenda ofisi ya madini ili kuelekezwa maeneo hayo yalipo na taratibu za kisheria. Aidha, hivi karibuni, madini ya urani yamegunduliwa katika eneo la Bahi. Hayajaanza kuchimbwa. Urani ni madini ya asili yenye kawaida ya kutoa mionzi. Hupatikana ndani ya udongo juu ya uso wa dunia, kwenye miamba na ndani ya maji ya ardhini na baharini.
Zamani urani ilikuwa inatumika duniani kwa ajili ya kutengeneza silaha tu, lakini hivi sasa yanatumika kwa ajili ya kuzalisha umeme na maji. Pia, hivi sasa urani hutumika hospitalini kwa ajili ya matibabu kupitia mionzi yake.
MISITU, WANYAMAPORI
Msangi anasema sehemu kubwa ya mkoa huu ni nyika tambarare. Hata hivyo, kuna misitu katika baadhi ya maeneo. Kwa mfano, kuna misitu minene inayosimamiwa na serikali kuu katika wilaya ya Mpwapwa katika maeneo ya Kiboriani, Mangâaliza, Mafwemelo na Wotta. Fursa nyingine iliyopo ni wanyamapori. Serikali inaendelea kuhifadhi wanyamapori. Kuna mapori makubwa mawili yanayohifadhiwa na serikali kwa ajili ya utalii, ambayo ni Swaga Swaga wilayani Chemba na Mkungunelo wilaya ya Kondoa, mpakani na wilaya ya Kiteto.
Lipo pia Pori la Akiba la Rudi wilayani Mpwapwa. Pori la Rudi halijahifadhiwa kisheria na watu wamekuwa wakivamia mara kwa mara na kufanya makazi, kulisha mifugo na kuchimba madini. Fursa nyingine ni viwanda. Afisa Biashara wa Mkoa wa Dodoma, Prisca Dugilo anasema kuna viwanda vikubwa mjini Dodoma katika maeneo ya Nala na Kizota, kama vile, kiwanda kikubwa cha kuchinja nyama Kizota. Pia, kuna viwanda vikubwa na vidogo vya kukamua alizeti katika maeneo ya Nala, Kilimani, Kondoa, Kongwa, Kibaigwa na Mpwapwa.
BANDARI KAVU
Fursa nyingine iliyopo Dodoma ni bandari kavu. Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wenye Viwanda, Biashara na Kilimo (TCCIA), Fred Azaria anasema kuna uwezekano mkubwa wa kuwekeza katika bandari kavu mjini Dodoma, kutokana na Dodoma kuunganishwa vizuri na mikoa mingine nchini.
Anasema endapo serikali itaanzisha bandari kavu Dodoma, itapunguza foleni nyingi zilizopo Dar es Salaam hivi sasa na pia hatua hiyo itawezesha taratibu nyingi za kupokea na kusafirisha mizigo kutoka bandarini Dar es Salaam, kufanyikia Dodoma badala ya Dar es Salaam, hivyo kuokoa muda na fedha nyingi wanazotumia wateja bandarini.
Azaria anafafanua kuwa bandari kavu ni eneo maalum ndani na nchi ambalo hutengwa kwa ajili ya kupokea mizigo kutoka bandarini na kuihifadhi. Bandari hizi husaidia kupunguza msongamano bandarini na kupunguza muda wa kutoa mizigo bandarini.
Anasema mambo yanayotakiwa kufanyika Dodoma, endapo serikali itaamua kuanzisha bandari kavu ni iiagize Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) itenge eneo maalum la bandari kavu; na pili taasisi zinazohusika na masuala ya bandari, kama vile Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TRA), zikutane na kuanzisha kwa pamoja bandari hiyo kavu Dodoma.
âHadi sasa TCCIA katika mkoa wa Dodoma ina wanachama 890 na wilaya ya Kondoa kuna wanachama 120, Mpwapwa 89, Kongwa/Kibaigwa wanachama 59 na waliosalia ni wa Dodoma Mjini. Viongozi wa TCCIA wa mkoa huu ni Mwenyekiti ni Faustine Mwakalinga na Makamu Mwenyekiti ni watatu, ambao ni Peter Olomi anayeshughulikia Sekta ya Biashara, Onesmo Ngowi wa Sekta ya Viwanda na Dk. Samson Mniko wa Sekta ya Kilimoâ anasema Azaria.
Nishati siyo tatizo katika mkoa wa Dodoma. Mkoa umeunganishwa vizuri katika gridi ya taifa. Bwawa kubwa kuliko yote nchini la kuzalisha umeme, lipo mkoani humu katika eneo la Mtera, mpakani na mkoa wa Iringa. Bwawa la Mtera huzalisha megawati 80 zinazounganishwa katika gridi. Pia, bwawa hilo huzalisha samaki wa aina mbalimbali na uvuvi ni shughuli kuu ya maeneo hayo.
UFUGAJI WA NYUKI
Fursa nyingine iliyopo Dodoma ni ufugaji wa nyuki. Ufugaji wa nyuki hufanyika katika wilaya zote na nje kidogo ya mji wa Dodoma katika eneo la Zuzu. Ufugaji hufanywa na vikundi na wafugaji binafsi. Nyuki hufugwa katika mizinga na zipo bustani za kuzalisha nyuki katika eneo la Zuzu. Kituo kikubwa cha kuzalisha nyuki kipo katika wilaya jirani ya Manyoni mkoani Singida. Mmoja wa wafugaji wakubwa wa nyuki mkoani Dodoma ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye ana shamba katika eneo lake la Zuzu.
Wananchi, wageni na viongozi mbalimbali wa serikali, taasisi na makampuni, wamekuwa wakitembelea shamba hilo la Pinda huko Zuzu, kujifunza juu ya ufugaji huo wa nyuki, unaotajirisha watu kwa haraka. Ufugaji huu umenufaisha watu wengi kutokana na asali na nta inayozalishwa. Asali nyingi kutoka Dodoma hupelekwa Kibaha mkoa wa Pwani, ambako husindikwa katika kiwanda binafsi, kisha kufungashwa vizuri na kusafirishwa nje ya nchi kuuzwa.
SEKTA YA BARABARA
Kwa upande wake, Mhandisi wa Barabara wa Mkoa, Mkwata M., anasema mkoa wa Dodoma una mtandao mzuri wa barabara wa kilometa 7,474.65, ambapo zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) ni kilometa 1,696.68 na halmashauri za wilaya na Manispaa kilometa 5,777.97 Serikali katika mkoa huu imejitahidi kuboresha barabara vijijini. Nao wabia wa maendeleo kupitia programua za MIVARF (ADB), uondoaji vikwazo (DFID) na Improvement of Rural Accessibility and Livelihood (USAID) wameweza kufungua barabara za vijijini katika halmashauri za Kondoa na Kongwa, zenye urefu wa kilometa 282.8 kwa kutumia Sh milioni 5,709.7.
Programu hizi zimewezesha maeneo yaliyo katika barabara zilizofanyiwa matengenezo kufikika wakati wote wa mwaka. Wabia wengine ni ADB, JICA, WB, DFID,USAID na ADB Aidha, serikali imejitahidi kuboresha mindombinu ya barabara mijini. Mkwata anasema kupitia Program ya TSCP jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 42.17 zimeweza kuboreshwa kwa kiwango cha lami katika mji wa Dodoma kwa kutumia Sh. bilioni 31.32 kutoka Benki ya Dunia .
Kiasi hiki cha fedha kinahusisha pia ujenzi wa mitaro ya mvua ya jumla ya kilometa 7.64. Program hii imeongeza mtandao wa barabara wa tabaka la lami kutoka kilometa 32.3.hadi kufikia kilometa 74.5 katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Yinza anasisitiza kuwa âMkoa wa Dodoma una fursa nyingi, hivyo lazima viongozi tuone tunawapeleka wapi wananchi kuhusu fursa hizo ambazo hazijatumika vizuriâ.
CHANGAMOTO ZILIZOPO
Uongozi wa mkoa wa Dodoma unakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake. Changamoto ya kwanza ni upungufu wa watumishi. Sekretarieti ya mkoa ina watumishi wachache katika seksheni na vitengo vyake. Kwa mfano katika seksheni ya miundombinu, kuna wahandsi watatu wakati shughuli ni nyingi mno na mkoa una eneo kubwa. Tatizo lingine ni ukosefu wa vitendea kazi kama magari na mafuta.
Kuna magari matatu tu katika sekretarieti ya mkoa. Hali hiyo inaathiri ufuatiliaji wa miradi na shughuli mbalimbali za serikali wilayani. Changamoto nyingine ni ukosefu wa ofisi ya mkoa. Jengo la mkuu wa mkoa wa Dodoma, liliungua moto mwaka 2010, lakini kwa miaka sita hadi leo viongozi wa mkoa huu hawana ofisi. Kwa sasa watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, wamejibanza katika jengo lililokuwa likitumiwa na Wizara ya Kilimo na Ushirika, jirani na ukumbi wa White House wa makao makuu ya CCM.
Kutokana na hali hiyo katika baadhi ya ofisi unaweza kukuta maafisa watano hadi sita wamebanana katika âkachumba kamojaâ. Hali hiyo inafanya wafanyakazi hao, wasifanye kazi vizuri, kwa ufanisi na kwa wakati. Hata hivyo, serikali kuu inajenga ofisi mpya ya mkuu wa mkoa wa Dodoma katika eneo la kuelekea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Jengo hilo lilianza kujengwa miaka mitano iliyopita, lakini halijaisha kutokana na fedha kidogo zinazotolewa na serikali kuu. Mpango wa kuhamisha makao makuu, umeleta changamoto nyingine kwa mji huu, kwani umekua haraka na ongezeko la watu ni kubwa hivi sasa wakati huduma nyingi ziko pale pale. Kwa mfano, wakazi wa mji huu walikuwa 50,000 mwaka 1975, mwaka 1980 walikuwa 91,500, mwaka 1985 walikuwa 170,000 na sasa kuna watu 410,956.
Recent Comments