WANANCHI wengi wanakiri kuona mabadiliko makubwa katika sekta ya miundombinu.
Mwandishi wa makala haya, STELLA NYEMENOHI, anaeleza shuhuda mbalimbali jinsi maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete katika sekta ya miundombinu yanavyochochea maendeleo ya ustawi wa taifa kiuchumi na kijamii. Wananchi wanakumbuka sana adha ya usafiri iliyokuwa ikiwakabili. Wapo wanaosimulia jinsi walivyolazimika kusafiri kwa mabasi wakipita nchi jirani za Uganda na Kenya, kwa ajili ya kukwepa ubovu wa barabara nchini.
Usafiri wa kutoka Bukoba, mkoani Kagera kwenda Dar es Salaam kwa njia ya barabara, ulikuwa ni wa adha kubwa kiasi cha kuwachukua takribani siku mbili njiani. Ndiyo maana, waliokuwa na uwezo kiuchumi, walilazimika kupitia Kampala (Uganda), Nairobi (Kenya) wakisaka kusafiri wa uhakika kwenye barabara nzuri. Adha hiyo haikuwa kwa wanaotoka mkoani Kagera pekee, bali pia waliokuwa wakitoka Mwanza, kulikuwa na mabasi yaliyokuwa yakizunguka hadi Nairobi kwa ajili ya kwenda Dar es Salaam.
Hivyo, safari ya kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam, ambayo kwa sasa inachukua takribani saa 18, kipindi kabla ya barabara kuboreshwa, ilichukua takribani siku mbili kufika. Baadhi ya watu, wanajaribu kufikiria maisha kabla ya Serikali ya awamu ya nne kuendeleza ujenzi wa barabara. Wanaona siyo tu waliathirika kijamii, bali hata kiuchumi. Mfanyabiashara Gaudence Kalisa mkazi wa wilayani Muleba, mkoa wa Kagera, anasimulia.
âMimi ni mfanyabiashara wa ndizi tangu mwaka 1997. Kipindi hicho tegemeo letu kubwa la usafirishaji ilikuwa ni kwa meli. Njia ya barabara ilikuwa inasumbua sana,â anasema Kalisa. Kalisa anasimulia, âKwa waliokuwa wakisafirisha ndizi kwenye malori wakitumia barabara, walilazimika kulala njiani kutokana na jinsi ambavyo ilikuwa mbovuâ¦lakini sasa, ni ajabu kuona tunatumia saa nane pekee kutoka Muleba hadi Mwanza.â
Damacen Stanslaus ni shuhuda mwingine wa mafanikio ya awamu ya nne katika ujenzi wa miundombinu hususani barabara na madaraja. Stanslaus, ambaye ni mkazi wa wilayani Iramba na mzaliwa wa Wilaya ya Muleba, anakumbua jinsi ambavyo alikuwa akihangaika kuunganisha usafiri kutoka kijijini kwake mkoani Kagera hadi kufika Iramba, mkoani Singida. âIlikuwa lazima upande basi kutoka Muleba, uende Bukoba Mjini kupanda meli kwenda Mwanza.
Ukifika Mwanza, ndipo upande basi la kwenda Singida, ambalo pia tulikuwa tukikaa njiani muda mrefu kutokana na ubovu wa barabara,â anasema Stanslaus. Anaendelea kusema, âLakini sasa mambo yamebadilika. Ukitoka Muleba unapanda basi moja kwa moja kwenye barabara ya lami na unafika siku hiyo hiyo Singidaâ¦haya ni maendeleo makubwa,â anasema. Mkazi huyo anaeleza pia furaha yake kutokana na kujengwa kwa kipande cha barabara katika mlima Msingi wilayani Mkalama na Iramba na kusema kimerahisisha sana usafiri kati ya wilaya hizo.
Mwingine ambaye anazungumzia mabadiliko chanya ya sekta ya miundombinu, ni Kennedy Jagaji ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu mkoani Ruvuma. Anasema ujenzi wa barabara ya lami kutoka Dodoma kwenda Iringa kupitia Mtera, umewarahisishia sana usafiri kwani awali, walilazimika kwenda ama hadi Morogoro. Kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma pia wanaeleza nafuu wanayoiona katika sekta ya miundombinu kutokana na ujenzi wa daraja la Mto Malagarasi wilayani Uvinza.
Mfano, wakazi wa Nguruka katika kueleza faraja ya daraja hilo la Kikwete, wanasema kwamba, magari yalilazimika kuzunguka kupitia barabara ya Nyakanazi na kupitia mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga na Tabora kuingia kwenye tafara ya Nguruka umbali wa zaidi ya kilometa 600. Mabasi ya abiria yalilazimika kupokezana abiria kwa kila basi kusimama upande mmoja wa barabara na abiria kulazimika kupitia kwa miguu kwa kutumia njia ya reli.
Hali hiyo inatajwa kwamba, siyo tu iliathiri abiria, bali pia kwa upande wa wafanyabiashara, iliwawia vigumu kusafirisha bidhaa zao. Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, pia wanaeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na hata madaraja. Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (BRT) chini ya Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ni miongoni mwa mambo yanayofanya serikali ya awamu ya nne iendelee kungâara katika historia ya ujenzi wa miundombinu.
Licha ya mradi wa BRT unaotekelezwa katika Barabara ya Morogoro ukilenga kukabili kero ya msongamano jijini Dar es Salaam, pia ujenzi wa daraja la Kigamboni, ni sehemu ya mambo ambayo serikali inajivunia kuchangia mabadiliko makubwa kiuchumi na kijamii. Kwa ujumla, hizi ni shuhuda chache kati ya nyingi kutoka maeneo mbalimbali nchini, zinazoweka wazi kuhusu mafanikio katika sekta ya miundombinu katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Wananchi wengi wanakiri kwamba, Serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wa Rais Kikwete, miongoni mwa mambo ambayo itakumbukwa sana kutokana na kufanya vizuri, ni pamoja na eneo la miundombinu. Hata Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaonesha Serikali imevuka malengo ya ujenzi wa barabara. Katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010- 2015, CCM iliahidi kukamilisha ukarabati wa barabara 29. Lakini sasa, imevuka malengo kwa kujenga barabara 33.
Miongoni mwa barabara hizo ni barabara ya kutoka Mto wa Mbu kwenda Loliondo, Mugumu, Nata, na Makutano yenye urefu wa kilometa 452 ambayo bado ujenzi wake unaendelea na Daraja la mto Malagarasi na barabara zake yenye urefu wa kilometa 48 ambayo ujenzi wake umekamilika. Pia kuna barabara ya Tunduru hadi Namtumbo yenye urefu wa kilometa 194, lakini ikajengwa kilometa 70 na barabara ya Sumbawanga hadi Kanyani, Nyakanazi yenye umbali wa kilometa 562 ambayo ujenzi wake unaendelea.
Barabara nyingine ni ya Tunduma hadi Sumbawanga yenye urefu wa kilometa 230 na barabara ya Makambako hadi Songea ambayo urefu wake ni kilometa 295. Ilani inasema nchi imepiga hatua kubwa katika sekta ya miondombinu kiasi cha kuifanya kuwa moja ya nchi zenye mtandao mzuri wa miundombinu ya barabara katika Afrika. Taarifa inaonesha, nchi ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 35,000 zinazojumuisha kilometa 12,786 za barabara kuu na kilometa 22,214 za barabara za mikoa.
Katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa Serikali ya awamu ya nne, barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,358 zimeendelea kujengwa katika kiwango. Barabara nyingine zenye urefu wa kilometa 3,419 zimefanyiwa umbembuzi na usanifu kwa ajili ya kuanza kujengwa. âKatika kipindi cha miaka kumi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 13,753 zimekuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi,â inasema sehemu ya ilani.
Inaeleza kwamba, jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 4,691 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,358 zimeendelea kujengwa katika kiwango cha lami. Katika kutambua kazi iliyofanywa na serikali ya awamu ya nne, inaelezwa kupitia ilani ya chama kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, CCM kitaielekeza Serikali ya awamu ya tano, kuendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja, vivuko, nyumba na majengo ya Serikali kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na huduma za kijamii.
Kipaumbele cha sasa, kwa mujibu wa ilani hiyo, katika ujenzi wa barabara kitazingatia barabara zinazounganisha Tanzania na nchi jirani; barabara zinazounganisha mikoa; na zinazokwenda kwenye maeneo yenye fursa za kiuchumi kama vile Liganga na Mchuchuma. Ili kutimiza azma hiyo, Mfuko wa Barabara utaimarishwa, vitabuniwa vyanzo vipya na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Kutaanzishwa pia wakala au taasisi itakayosimamia kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara za miji na majiji na Halmashauri ambazo ziko chini ya Tamisemi. Lakini pia, ili kupunguza umasikini, kuwezesha wananchi kiuchumi na kuongeza kasi ya maendeleo, Serikali itaunganisha makao makuu ya mikoa ambayo haijaunganishwa kwa barabara za lami na kujenga barabara kuu zote zinazounganisha Tanzania na nchi jirani kwa kiwango cha lami.
Matarajio mengine ni kuhakikisha kuwa makao makuu ya wilaya ambazo bado barabara zake hazipitiki majira yote , zinafanyiwa ukarabati angalau kwa kiwango cha changarawe na kuzifanya zipitike majira yote ya mwaka. Ni ukweli usiopingika kwamba, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji umechochea kukua kwa shughuli za kiuchumi ambazo zimewezesha pia kuongeza ajira nchini kupitia usafirishaji abiria, bidhaa mbalimbali zikiwamo za mashambani.
Hata ilani ya CCM inakiri kwamba, kulingana na jinsi ambavyo Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara, reli, madaraja, vivuko na viwanja vya ndege, umekuwa msingi mkuu wa kukua kwa uchumi na shughuli nyingine za kijamii. Uwapo wa miundombinu bora, kigezo sahihi cha ustawi wa nchi kiuchumi, kijamii kutokana na kuongeza fursa za uzalishaji, ajira na usafirishaji.
Recent Comments