RAIS Jakaya Kikwete ameeleza ndoto yake baada ya muda wake wa urais kumalizika, kuwa ataanzisha taasisi ya maendeleo, itakayosimamia midahalo, semina na kongamano kwa maendeleo ya taifa.
Pia, ameeleza kuwa anatamani kukabidhi urais kwa mrithi wake wiki moja baada ya matokeo kutangazwa.
Kikwete amesema atakapostaafu ataishi kijijini kwao Msoga, Chalinze mkoani Pwani, kuendeleza ufugaji na kilimo cha nanasi na hatapenda kujishughulisha kwa kiwango kikubwa na masuala ya serikali.
Alisema hayo Ikulu, Dar es Salaam jana, alipopokea Shahada ya Heshima kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Ndoto zake
Rais Kikwete alisisitiza ndoto yake ni kuanzisha taasisi hiyo ya maendeleo, ambayo kazi yake kubwa itakuwa kujadili, kupokea, kutafuta wadhamini na kushauri juu ya masuala yatakayoiletea maendeleo nchi.
âKuna watu wamenishauri nianzishe taasisi ya kushughulikia migogoro, sitaki kabisa kuitwa mchawi na wala taasisi hiyo siitaki kabisa, ila mgogoro ukitokea na nikahitajika, basi nitachangia; Ila dhamira yangu ni kushughulikia masuala ya maendeleo,â alisema.
Alitaja baadhi ya masuala ya maendeleo yakayopewa kipaumbele na taasisi hiyo kuwa ni pamoja na afya, afya ya akinamama na watoto, kilimo, maendeleo ya sayansi na teknolojia na viwanda.
Maisha kijijini
Alisema atakapokabidhi madaraka kwa Serikali ya Awamu ya Tano, ataachana na shughuli za kiserikali na badala yake ataenda kuishi kijijini, ambako ataendeleza shughuli zake za ufugaji na kilimo.
âKusema ukweli nitakapostaafu sitopenda kujishughulisha sana na masuala ya kiserikali, kwa sababu atakuwepo Rais mwingine lakini pia nitapenda nijishughulishe na shughuli zangu nilime mananasi na kufuga. Ila nitajaribu kuchangia kwa kadri ya uwezo wangu,â alisisitiza.
Rais Kikwete alisema dhamira yake ni kukabidhi madaraka kwa Rais ajaye wiki moja baada ya matokeo ya uchaguzi kutoka aweze kufungasha virago vyake na kwenda kijijini.
Wosia wake
Aidha, Rais Kikwete alisisitiza juu ya umuhimu wa nchi kuendelea kusimamia na kukumbatia maendeleo ya sayansi na teknolojia, nchi iweze kupiga hatua za maendeleo.
Akizungumzia maendeleo ya Taasisi ya Nelson Mandela, alisema wazo la uanzishwaji wake katika nchi za Afrika lilitokana na Benki ya Dunia kuziwezesha kupata maendeleo ya haraka katika eneo la sayansi na teknolojia.
Alisema benki hiyo ilihamasisha vyuo hivyo vianzishwe katika kanda nne ambazo ni za Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi. Katika Kanda ya Kaskazini, Nigeria imeanzisha chuo hicho Abuja na kwa Kanda ya Mashariki, kimeanzishwa Arusha.
âTulipoanza, tulikuwa hatuna fedha za kutosha, Benki ya Dunia ilihamasisha uanzishwaji wa vyuo hivi, lakini haikufadhili uanzishwaji wake, lakini pia sisi tulitarajia wenzetu wa jirani hasa wa Afrika Mashariki wanegtusaidia lakini walituachia wenyewe,â alisema.
Alisema Tanzania ilianzisha chuo hicho kutokana na umuhimu wake katika masuala ya maendeleo. Alisema kwa sasa, tofauti ya maendeleo ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea kimaendeleo huonekana kutokana na hatua kubwa ambayo nchi zilizoendelea imepiga katika sayansi na teknolojia.
Aliahidi kushughulikia changamoto zinazokabili chuo hicho ikiwemo uhaba wa fedha. Alisisitiza kwamba, Serikali kwa sasa kutokana na kukabiliwa na masuala makubwa ikiwemo uchaguzi, ilishindwa kutoa kiasi cha fedha ilichoahidi kwa chuo hicho.
âKuhusu ombi lenu la kuandaa chakula kwa ajili ya wafadhili mliowaalika katika harambee ya kuchagia mfuko wenu maalumu kuendeshea chuo, muda mliopanga nitakuwa nimeshastaafu, hivyo nitawaandikia barua hao wafadhili na baadaye kulikabidhi jambo hili kwa Rais ajaye,â alisema.
Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Nelson Maendela cha Sayansi na Teknolojia, Profesa David Mwakyusa, alisema wamemtunuku Kikwete shahada hiyo, kutokana na kutambua mchango wake katika masuala ya elimu hasa eneo la sayansi na teknolojia.
âTulipanga Shahada ya Kwanza tumpatie Rais Kikwete kutokana na kujitoa kwake katika mambo ya sayansi na teknolojia,â alisema.
Alisema pamoja na chuo hicho kuanzishwa na kuanza kufanya vizuri, bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali za kukiendeleza ikiwemo uhaba wa fedha.
Kwa mujibu wa Profesa Mwakyusa, Serikali iliahidi kuipatia taasisi Sh bilioni 7.2 lakini hadi sasa kimepatiwa Sh bilioni mbili.
Alisema kwa sasa umeanzishwa mfumo maalumu wa kuendesha chuo hicho na imeandaliwa harambee kwa ajili ya wafadhili.
âTunakuomba mheshimwia Rais utusaidie kuwaalika wale wafadhili, ambao sisi tumewabaini na tunaona wataweza kutusaidia angalau tupate hasa dola za Marekani milioni 10,â alisema.
Recent Comments