Uongo, Dhihaka, Kejeli kwa wana Ngara

By Baraka Bitariho Dec 8, 2023
Kinachoendelea sio kilichotarajiwa na mwaka 2023 ndio unakatika, tulitegemea faraja, twarushiwa matusi na misengenyo.
Kinachoendelea sio kilichotarajiwa na mwaka 2023 ndio unakatika, tulitegemea faraja, twarushiwa matusi na misengenyo.
Na Mwandishi wetu, Ngaratv.com
– Imeletwa kwenu na Kamera Nene
*NI NANI YUKO NYUMA YA UONGO DHIDI YA CHAMA NA SERIKALI, DHIHAKA NA KEJELI KWA WANA NGARA ZINAZOFANYWA NA MBUNGE NDAISABA RUHORO? JINAMIZI LA UCHAGUZI MKUU 2025 LINAMTESA?*
Uongozi ndio hubeba hatima ya ustawi wa jamii yoyote. Mageuzi na mabadiliko chanya ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni yanaanzia kwenye fikra, mitazamo, maono, hulka na haiba za Viongozi. Kama Kiongozi atakuwa na kiwango chini ya wastani kwa mambo tajwa hapo juu, hatima njema itakuwa kitendawili na mustakabali mwema wa jamii anayoingoza itakuwa ni mashaka makubwa.
Wanazuoni wana mjadala mpana na mkubwa usio na mwafaka wa pamoja ikiwa Viongozi huzaliwa au hutengenezwa *(Long lasting debate on whether Leaders are born or made)*. Kwa wale wenye mtazamo kuwa Viongozi huzaliwa; pamoja na mambo mengine huamini kuwa Uongozi ni karama ambayo Mtu huzaliwa nayo na ni kipaji kama zilivyo talanta nyingine kutoka kwa Mwenyezi Mungu: Na kwa wale wenye mtazamo kuwa Viongozi hutengenezwa wanaamini kuwa Kiongozi lazima apitie mchakato wa lazima wa malezi, makuzi na mafunzo yanayomuandaa kuwa Kiongozi bora.
Nimefuatilia mijadala katika vijiwe vya kidijitali hasa makundi sogozi (Whatsapp groups) nikaona uongo mkubwa anaofanya Mbunge Ndaisaba Ruhoro na wafuasi wake dhidi ya Chama na Serikali, sambamba na dhihaka na kejeli kwa watangulizi wake na Wana Ngara anaoamini hawamuungi mkono kuelekea uchaguzi Mkuu 2025 nikapata mashaka makubwa na wasiwasi usiomithilika ikiwa mwakilishi huyu wa Wananchi yuko katika kundi lipi la Viongozi.
Kwa fikra, hulka na mitazamo yake kwa maendeleo ya Wilaya ya Ngara, kwa Watangulizi wake na kwa wale anaoamini kuwa ni wapinzani wake sidhani kama amezaliwa au ametengenezwa kuwa Kiongozi. Kwa namna anavyojikweza na kujipa utukufu na utakatifu asiostahili, ninashindwa kujua yuko kundi lipi kati ya hayo makundi mawili yanayozua mjadala.
Mbunge anayejiona kuwa yeye ndiye Serikali Kuu, yeye ndiye Halmashauri, yeye ndiye TANROADS, yeye ndiye RUWASA, yeye ndiye TARURA, yeye ndiye TANESCO, yeye ndiye Idara ya Kilimo. Yaani kiufupi yeye ndiye mpangaji, mtekelezaji na msimamizi wa shughuli za Serikali na miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Ngara ana maadili na miiko ya uongozi kweli? Amezaliwa au ametengenezwa kuwa Kiongozi kweli?
Ina maana Ngara hakuna Serikali mpaka ionekane kila kitu kinafanywa na Mbunge? Hizo fedha za kutekeleza miradi anatoa mfukoni kwake au pesa za Serikali? Chama hakijaelekeza Serikali kutekeleza miradi hiyo mpaka ionekane kila mradi ni maelekezo, pesa na jitihada za Mbunge? Anasema huko nyuma kabla yake hakikufanyika kitu na kwamba Ngara ilikuwa imetelekezwa, ina maana CCM na Serikali yake walikuwa likizo? Ni nani anampa kiburi na jeuri ya kuzibagaza Serikali za awamu zilizopita?
Moja ya ujumbe wake kwenye group la Jimbo anasema kuna mtu anashawishi watu cha kuandika kwenye magroup, lakini anaenda mbali zaidi anamtweza kuwa kazi pekee anayoiweza ni kuuza bisukuti na dompo tu; je wauza bisukuti na dompo si walipa kodi wa Nchi hii? Kuuza bisukuti na dompo ni kosa la jinai? Mshahara na posho zake hazitokani na kodi za Watanzania wakiwemo hao Wafanyabiashara  anaowakejeli mitandaoni? Ninasubiri kuona kama umoja wa Wafanyabiashara Ngara watakaa kimya kwa shambulio hilo la aibu dhidi ya mwenzao na shughuli zao zinazowapatia kipato.
Ni bahati mbaya sana kwa Ngara kuwa na Mbunge jeuri, fedhuli na mwenye kiburi cha pesa kwa kiwango cha kudhani anaweze kumnunua kila mtu. Ninasikia yeye na wapambe wake wanatamba mtaani kuwa kuelekea siku kuu za Christmass na Mwaka mpya kuna package kambambe kwa Viongozi wa  dini na madhehebu mbali mbali ili wamuunge mkono katika kampeni yake ya kuvunja mwiko 2025. Ndugu zangu Wakristo na Waislamu msikubali udhalilishaji huo utokee kwa Viongozi wetu, tunao wajibu mkubwa wa kuwalinda na kuwatunza Viongozi wetu wa dini, tunao wajibu wa kuhudumia nyumba zetu za ibada na Watumishi wake, tujitoe vya kutosha kwa zaka na sadaka ili Viongozi wetu wa kiroho wasitwezwe na kubagazwa na mtu yeyote hasa Wanasiasa uchwara wenye uroho na uchu wa madaraka.
Akhsanteni sana, ninawatakia kazi na afya njema.
Tunawashukuru kwa kuendelea kutuamini na kutufatilia Ngaratv.com tukishirikiana na Simamia.com