KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio kadhaa ya ujambazi katika baadhi ya maeneo nchini, ambapo majambazi wamekuwa wakivamia watu na makazi na mara nyingine vituo vya polisi. Vitendo hivyo vimekuwa vikileta hofu na kuchafua amani na utulivu, ambayo imekuwepo tangu nchi ilipopata Uhuru miaka ya 1960.
Hata hivyo, mara zote jeshi la Polisi limejitahidi kupambana na hali hiyo na linaendelea kuchukua hatua mbalimbali. Kwa mfano, hivi karibuni polisi katika mkoa wa Kagera, walikamata bunduki moja ya kivita aina ya G3 na silaha zingine, ambazo majambazi walikuwa wakiitumia kufanyia uhalifu.
Silaha hizo zilikamatwa katika kijiji cha Masheshe Kata Nyabionza wilayani Karagwe, ambapo pia polisi walifanikiwa kuua majambazi wanne. Tunatoa pongezi kwa Polisi wote kwa jitihada kubwa, wanazofanya kupambana na ujambazi na uhalifu mwingine katika mkoa huo, uliopo mpakani mwa Tanzania na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda.
Pia, tunapongeza wananchi kwa kusaidia juhudi za jeshi hilo katika kutokomeza ujambazi. Tuna uhakika ushirikiano huo ndiyo uliowezesha polisi kupata taarifa za silaha hizo zilizokamatwa.
Aidha, ushirikiano huo wa wananchi ndio uliowezesha polisi kupata taarifa za majambazi hao, walioingia katika kijiji hicho kufanya uhalifu. Ni dhahiri kama wananchi wasingetoa ushirikiano mkubwa, kazi ya kufuatilia majambazi hao ingekuwa ngumu, au isingefanikiwa. Ni wazi pia kuwa polisi peke yao, hawawezi kupambana na wimbi la uhalifu nchini.
Tunahimiza ushirikiano na wananchi, uongezwe maradufu na pia polisi wafanye doria na misako ya mara kwa mara ya majambazi katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kudumisha hali ya amani. Kuna haja ya polisi na wananchi kutambua kuwa majambazi, hubadilisha mbinu zao kila siku.
Kwa mfano, kuna wakati majambazi hutumia mbinu ya kutoa chakula na wakati mwingine hugawa vinywaji. Mahali pengine hutumia ulaghai tu. Kwa mfano katika tukio moja la karibuni huko Kagera, majambazi walifika katika duka la mfanyabiashara mmoja na kujifanya wanataka kununua vocha za simu za mitandao mbalimbali.
Baadaye walimfunga kamba mwenye duka na kuanza kupora dukani na maduka ya jirani na kisha kutokomea porini. Katika tukio lingine mkoani humo, majambazi walipofika katika duka moja kubwa, waliwapatia vinywaji walinzi wawili na kusababisha wasinzie bila kujitambua.
Ndipo walivunja na kuingia ndani ya duka na kupora fedha na vitu vya thamani kadhaa na kutokomea. Tuchukue tahadhari kubwa juu ya mbinu mbalimbali za wahalifu na majambazi, zinazobadilika kila siku kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia duniani hivi sasa.
Tukumbuke kuwa ujambazi na uhalifu mwingine utapungua, kama tutalisaidia jeshi la Polisi kupambana na vitendo hivyo.
Recent Comments