LICHA ya serikali kutotamka ni lugha ipi itatumika kwa ajili ya kufundishia shuleni, kuna mijadala inayoendelea kuhusiana na jambo hilo. Hapa nchini lugha mbili zinatumika kufundishia shuleni ambazo ni Kiswahili na Kiingereza.
Katika shule za msingi masomo mengi yanafundishwa kwa lugha ya Kiswahili isipokuwa somo la Kiingereza. Katika shule za sekondari, masomo yote yanafundishwa kwa Kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili. Masomo shule ya msingi yanayofundishwa kwa lugha ya Kiswahili ni hayo hayo yanayofundishwa kwa lugha ya Kiingereza. Hivi karibuni, vijana kutoka shule za sekondari hadi vyuo wamefanya tamasha kupitisha ilani yao ya mwaka 2015 ambayo pamoja na mambo mengine, suala la lugha liliibuliwa.
Tamasha hilo linalojulikana kwa jina la Youth Manifesto, lina lengo la kujadili mambo yanayowahusu ili yapewe kipaumbele katika miaka mitano ijayo. Waandaaji wa tamasha hilo, Shirika la Restless Development wamewakutanisha vijana kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili. Mjadala kuhusu lugha ya kutumika kufundishia shuleni na vyuoni umeshika kasi huku kila upande ukitamka ni ipi inafaa ili kuboresha elimu kulingana na mahitaji ya sasa.
Katika ilani hiyo, kwenye kipengele cha elimu imebainisha wazi kuwa lugha ya Kiingereza itumike kufundishia kuanzia shule za awali. Baadhi ya vijana wanapinga kwa kusema kuwa lugha inayofaa kutumika kufundishia ni ya Kiswahili. Katibu wa Vijana wa Wanafunzi, Alfonce Msako anasema lugha ambayo serikali inapaswa kuifanyia kazi ni ya Kiswahili kwa kuwa inaonesha uzalendo kwa Watanzania.
Anasema Kiswahili ni lugha ya mama inayostahili kuenziwa nchini kupitia masomo yanayofundishwa katika shule za msingi na sekondari. ââLazima tuwe wabunifu katika masuala ya elimu. Lugha ya Kiswahili inatakiwa itumike kufundishia katika shule zote na sio lugha ya Kiingereza kwani tunakuwa hatuoneshi uzalendo,ââ anasema Msako. Astelia John anasema, hakuna mzazi anayependa mwanawe ahitimu bila ya kuelewa kujieleza kwa lugha ya Kiingereza.
Kijana huyo anaunga mkono suala la kutumika kwa lugha ya Kiingereza kufundisha kuanzia shule za awali hadi vyuoni. John anasema, suala la kutumia lugha ya Kiswahili kufundishia linasababisha mwanafunzi ashindwe katika mashindano ya kielimu. ââHakuna mzazi anayependa mtoto wake kushindwa kujieleza hata kwa Kiingereza. Hapo ulipo unatamani sana kumpeleka mtoto wako katika shule za Kiingereza kwa lengo la kumuweka katika mazingira mazuri,ââ anasema John.
ââNi vyema kutumia kwa lugha ambayo mataifa ya nje wanatumia kwa lengo la kutusaidia kushindania nafasi mbalimbali za elimu,ââanasema. John anasema, haiwezekani masomo yote ya sayansi yafundishwe kwa lugha ya Kiswahili kwa kuwa yatakuwepo mapungufu makubwa na kwamba wahitimu hawataweza kushindanishwa na mataifa mengine.
Nickson Simon maarufu kama Nikki wa Pili, ambaye ni msanii wa kizazi kipya , anasema kuwa suala la lugha ya kufundishia shuleni na vyuoni linapaswa kuangaliwa kwa umakini wake kwa kuwa lugha zote zina umuhimu. Anasema, wapo wanafunzi wanaohitimu hadi shule ya sekondari lakini hawajui kusoma, kuandika, na kuhesabu. Simon anahoji kwamba, je ni lugha ipi ambayo ikitumika katika kufundishia italeta unafuu kwa wanafunzi walengwa?
ââNi vyema lugha zote zitumike kwa ajili ya kufundishia kwani mfumo bora wa elimu ndio utakaosaidia katika kuimarisha masuala yote ya elimu ikiwa ni pamoja na miundombinu yake,ââ anasema Simon. Msanii huyo anasema, jambo muhimu la kuzingatiwa ni kuwahamasisha walimu kutumia nyenzo zao kuwafanya wanafunzi wote waweze kuelewa kinachofundishwa.
Simon anasema, endapo walimu watatimiza wajibu wao ipasavyo, vivyo hivyo kwa serikali, wazazi na wanafunzi, wataweza kufikia malengo yao bila ya kujali ni lugha ipi inafaa zaidi kuliko nyingine. ââKwa upande wangu kila mmoja anatakiwa kuchukua nafasi yake katika suala zima la elimu hivyo ukiangalia suala la lugha sio lazima uchague bali kuangalia uwezekano wa wanafunzi kuelewa kile wanachofundishwa na si vinginevyo,ââ anasema Simon.
Mshindi wa tuzo ya vijana nchini Adam Anthony anasema, suala la elimu kwa kila kijana ni muhimu endapo itapatikana kwa urahisi. Anasema vijana wengi wanaishia katika elimu ya msingi na sekondari na wachache sana ambao wanafika vyuo vikuu kwa sababu ya changamoto zilizopo nchini. Anthony anasema, ni vyema kila kijana kutambua lugha zote zinazofundishwa ili kuleta wepesi katika masuala ya biashara na kiuchumi.
Anasema wafanyabiashara wengi nchini wanafahamu lugha tofauti ili kurahisisha mawasiliano kati yao na wenzao au wateja wao. ââLazima tuwafundishe lugha zote ili kuhakikisha tunaweza kufikia malengo ya kuwapata wafanyabiashara wazuri na kuinua uchumi wetu kama vijana,ââ anasema Anthony. ââKwa ulimwengu wa sasa vijana tunatakiwa kujua lugha zote zinazofundishwa kwa ajili ya manufaa yetu binafsi na Taifa kwa ujumla,ââanasema.
Mtaalamu wa masuala ya mawasiliano na mwanzilishi wa mabadiliko ya vijana, Maria Sarungi Tsehai anasema, mjadala kuhusu lugha ipi itumike kufundishia ni lazima lizingatie maendeleo ya sayansi na teknolojia. Anasema, lugha zote ni bora kwa sababu kutumia Kiswahili kunaongeza uzalendo wa Watanzania kuipenda lugha yao lakini pia lugha ya Kiingereza ni kwa ajili ya kutengeneza mahusiano ya kimataifa.
ââNi bora kutumika kwa lugha zote isipokuwa ni lazima tuweke mkazo kwa wanafunzi waweze kuelewa nini wanataka na kipi wanafundishwa mashuleni ili kuboresha elimu tuliyonayo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo,ââ anasema Tsehai. Mkufunzi wa masuala ya sheria katika Chuo Kikuu cha Sheria Tanzania, Dk Ally Possi anasema, kila mwanafunzi anatakiwa kufahamu lugha zote na si Kiingereza au Kiswahili pekee. Anasema dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia, wanafunzi wote wanatakiwa kujua lugha zote duniani kwa lengo ni kuelewa soko la dunia linataka nini.
ââChuo ninachofundisha mimi unakuta mwanafunzi hajui hata Kiingereza lakini ukitaka kumuelekeza hataki. Sio wote ambao wanajua Kiingereza hivyo basi mtu akitaka kukuelekeza kubali kuelekezeka,ââ anasema Dk Possi. Anasema, wawekezaji wengi wanakuja nchini lakini hawajui Kiingereza hivyo tunatakiwa kujua lugha zote ili kumudu ushindani katika biashara na mambo mengine.
ââUkijua lugha ya Kiingereza, Kifaransa, Kichina na lugha zote duniani ni bora zaidi kuliko kusema tuchague lugha moja tu,ââ anasema Dk Possi. Mwanzilishi wa mtandao wa Jamii Forum, Mike Mushi anasema, ni bora kutumia lugha zote kuliko kuchagua kwa kuwa inaweza ikaathiri mfumo wa elimu baadaye. Anasema kila mmoja atambue nafasi yake katika elimu hivyo wanafunzi waelewe wanachofundishwa na kutoshabikia masuala ya lugha ya kufundishia shuleni.
Recent Comments