WATANZANIA wanatakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuimarisha biashara ndani na nje ya nchi na kuliwezesha Taifa kuingia kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.
Miaka sita iliyopita Tanzania ilisaini Mkataba wa Itifaki ya Soko la pamoja la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nchi hizo ni Kenya,Uganda, Rwanda, Burundi na wenyeji Tanzania. Utiaji saini huo wa soko la pamoja ulifanywa na wakuu wa nchi akiwamo Rais Jakaya Kikwete, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Kurunziza wa Burundi na Rais Mwai Kibaki wa Kenya ambaye alistaafu.
Lengo la utiaji saini wa itifaki la soko hilo la pamoja lilikuwa ni uimarishaji wa biashara ya bidhaa kwa kuondoa vikwazo vya kibiashara, kutoa fursa zaidi za ajira sanjari na kuwezesha watu wa nchi wanachama kupata uhuru wa kufanya biashara kwa nchi hizo. Dira kuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kukuza kipato, kuinua hali ya maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki, kukuza uchumi, na kujenga ushindani wa kanda katika ngazi ya kimataifa.
Katika utekelezaji wa mkataba huo, nchi wanachama zitanufaika kutokana na mahusiano mazuri ya kibiashara na uwekezaji, zitanufaika pia na uwepo wa program mbalimbali ikiwa na pamoja na kuendeleza mitandao ya barabara, reli, umeme, elimu, afya, usalama na utawala bora. Ili kufanikisha azma hiyo kamati ya kitaifa imeundwa kwa ajili ya hushughulikia vikwazo vya kibiashara (Non- Tariff Barriers) kwa nchi wanachama ambayo inakutanisha wadau kutoka sekta ya umma na sekta binafsi.
Mtu mwenye malalamiko katika biashara anatakiwa kutoa taarifa katika Kamati hiyo au katika Wizara. Aidha, kuna Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao husimamia upatikanaji wa ufumbuzi katika kuwasaidia wafanyabiashara ndani ya Jumuiya. Maamuzi hayo huwekwa katika mifumo ya mawasiliano hasa katika tovuti na kusambazwa kwenye vyombo vya habari ili kuwapa mwanya wafanyabiashara waweze kuwa na ufahamu mkubwa zaidi.
Utekelezaji wa soko huru la bidhaa kwa nchi za Afrika Mashariki utaiwezesha Tanzania na nchi nyingine wanachama kupata soko la uhakika kwa bidhaa za kilimo na viwanda katika jumuiya ya watu zaidi ya milioni 190. Ibara ya 10 ya itifaki hiyo inatoa nafasi kwa raia nchi wanachama uhuru wa kupata ajira katika nchi yoyote mwanachama na kutobaguliwa kwa misingi ya utaifa wa nchi anakotoka.
Ni dhahiri fursa hiyo itawawezesha Watanzania kuajiriwa katika sekta za kiuchumi za nchi wanachama na wakati huo huo kuongeza tija kwenye uzalishaji na ukuzaji wa uchumi. Fursa za soko hilo zitaiwezesha Tanzania katika kutekeleza kikamilifu umoja wa forodha kwa kuondoa ushuru wa forodha kwa biashara ya bidhaa kwa nchi wanachama. Kiuchumi vitu vinavyodhibiti fursa za soko ni pamoja na uzalishaji wa bidhaa za mazao ya biashara na chakula ambayo ndiyo hatua mojawapo ambayo inatumiwa na nchi wanachama katika kumiliki fursa za soko hilo.
Itifaki ya Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza kutekelezwa Januari mwaka 2005 kwa lengo la kukuza biashara, kuongeza ufanisi katika uzalishaji, kuongeza uwekezaji wa ndani baina ya nchi wanachama na kuendeleza viwanda. Katika kipindi chote cha utekelezaji wa Itifaki hiyo, Tanzania imepata mafanikio makubwa hususan katika eneo la biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Thamani ya bidhaa za Tanzania zilizouzwa katika Nchi Wanachama imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 142.0 mwaka 2005 hadi Dola za Marekani milioni 1,120.1 mwaka 2013 ikiwa ni ongezeko la Dola za Marekani milioni 978.10. Bidhaa zilizochangia katika ongezeko hilo ni pamoja na nafaka, karatasi, mbolea, vifaa vya umeme, mashine, bidhaa za mafuta na vimiminika, vyandarua, bidhaa za plastiki, na chai. Bidhaa nyingine ni saruji, matunda, chuma, samaki, ngano, sukari na nguo.
Aidha, thamani ya biashara ya jumla ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 317.9 mwaka 2005 hadi Dola za Marekani milioni 1,515.0 mwaka 2013. Ongezeko hilo limeongeza mgawo wa biashara ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka asilimia 15.2 mwaka 2005 na kufikia asilimia 26.1 mwaka 2013 ikiwa ni nafasi ya pili baada ya Kenya.
Utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki umechangia katika jitihada za Serikali za kuvutia na kukuza uwekezaji hapa Nchini. Utekelezaji wa Itifaki hiyo umewezesha idadi na thamani ya miradi ya uwekezaji kutoka Nchi Wanachama kuongezeka kutoka miradi 35 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 39.6 mwaka 2005 hadi kufikia miradi 244 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 676.5 mwaka 2013.
Katika kipindi hicho miradi hiyo imezalisha jumla ya ajira 15,721 kwa Watanzania. Ili kuendelea kufaidika na soko hilo wafanyabiashara wa Kitanzania wanapaswa kupanua wigo kwa kutumia vyema fursa zilizopo kwenye soko la pamoja ili kufikia lengo la kuingia katika kundi la uchumi wa kati na kuwa katika kundi la nchi zilizoendelea lenye kipato cha wastani wa Dola za Marekani 3,946 hadi 12,195.
Kwa mujibu wa dira ya Taifa, Tanzania inatarajia kuongoza pato la mtu kufikia Dola za Marekani 88,600 na kuwa na uchumi mkubwa katika kanda ya Afrika uliojengwa kwenye msingi imara wa viwanda vikubwa vinavyozalisha bidhaa zenye ubora na kwa kiwango kikubwa na kilimo cha kisasa. Pia inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2010 Tanzania itakuwa miongoni nchi yenye barabara kubwa zenye lami, mtandao wa reli ya kisasa unaoendeshwa kwa nishati ya umeme nchi nzima, utakaopunguza usafiri wa watu na mizigo kwa barabara na kutumia zaidi usafiri wa reli na anga.
Inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2010 Tanzania inakuwa na ongezeko la uzalishaji na matumizi ya nishati katika sekta zote za uchumi; kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika kufika takriban asilimia 100 na nguvu kazi ya Taifa kuwa yenye ujuzi wa hali ya juu. Mambo mengine yanakayowezesha Tanzania kuingia katika kundi la uchumi wa kati ni kuongezeka kwa muda wa wastani kwa Mtanzania kuishi ufikie miaka 70; Kiwango cha vifo vya watoto wachanga kuwa cha chini kabisa hadi kufikia ni 3 kwa kila watoto 1,000; na matumizi ya hali ya juu ya sayansi na teknolojia katika nyanja zote za uzalishaji na huduma.
Recent Comments