SERIKALI imefuta hati miliki ya mashamba makubwa manne ya wawekezaji mkoani Arusha.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa kunyangâanya viwanja, kama ilivyojitokeza wiki iliyopita katika mikoa ya Morogoro na Pwani. Kutokana na uamuzi huo, sasa mashamba hayo yatagawiwa kwa wananchi wenye uhaba wa ardhi, waliojiorodhesha kutokana na migogoro hiyo.
Zaidi ya watu 2,000 wanatarajiwa kupata maeneo ya makazi na kilimo mkoani Arusha. Katika mkoa wa Arusha, mashamba yaliyofutiwa hatimiliki ni Tanzania Plantations Limited iliyokuwa na mashamba matatu na Shamba la Noors lililopo kijiji cha Laroi na Kisima cha Mungu, Oljoro mkoani hapa.
Kufutwa kwa mashamba hayo na serikali kutaondoa mgogoro wa muda mrefu, uliokuwa unasababisha mapigano ya mara kwa mara na uvamizi wa mashamba na wananchi hao, kwa kudai ardhi iliyokuwa inamilikiwa na wawekezaji hao bila kuendelezwa.
Akizungumza jijini hapa, jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema serikali imeamua kufuta miliki ya mashamba hayo ili kuwapa wananchi waweze kugawiwa kihalali na kupimiwa maeneo yao kwa watu, ambao hawana ardhi ambao waliainishwa hapo awali.
Alisema mashamba yaliyofutiwa hati hizo na Rais ni Tanzania Plantations lenye hati NP 305, NP 304 na C.T.No 5189 yenye ukubwa wa ekari 6,396 na ni mali ya serikali na stahili ya mwekezaji huyo ni fidia. Lakini pia katika ufutaji wa mashamba hayo, mwekezaji ameachiwa shamba lenye namba N.371 ambalo analimiliki kihalali.
Alisema serikali imeamua kutoa ekari 100 kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wenye uhaba wa ardhi na kilimo katika Halmashauri ya Meru. Alisema baada ya ubatilishaji wa mashamba ya Tanzania Plantations Ltd na ardhi aliyoitoa mwekezaji huyo kwa hiyari yake, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha imepata jumla ya ekari 6176.5 na Halmashauri ya Meru ekari 925 .
Alisema zaidi ya wananchi 2,000, watapata maeneo ya kujenga (makazi) na kilimo. Alisema kazi hiyo itasimamiwa na timu ya wataalamu, iliyoundwa kwa ajili ya kusimamia ugawaji wa maeneo hayo kwa wananchi wenye uhaba wa ardhi.
Lukuvi pia alisema idadi ya watu wanaohitaji ardhi ni kubwa, lakini wahusika watajua ni kina nani wana mahitaji ya ardhi kwani Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wananchi wanaohitaji ardhi kwa ajili ya makazi na mashamba ni 2000 na Halmashauri ya Meru wananchi wanaohitaji ardhi kwa ajili ya makazi na mashamba ni 2,891.
Alisema katika shamba la Noors ambalo linahusisha wananchi wa kijiji cha Laroi na Kisima cha Mungu, awali mwekezaji aliridhia kutoa ekari 696 kutoka shamba lake lenye ekari 2,296. Alisema shamba hilo mpaka hivi sasa linamilikiwa na mwekezaji kwa hati namba 14,294 ikiwa miliki ya miaka 90 na miezi kumi kuanzia 1/7/1959, hivyo hati yake itaisha mwaka 2050.
âKumbukeni huu ni utekelezaji wa ahadi za Rais. Kulikuwa na migogoro mingi ya ardhi na hivi sasa mingi tumeshaitatuaâ alisema.â Aliongeza kuwa, wiki iliyopita mashamba zaidi ya 7 wilayani Mvomero, yalifutiwa umiliki wa ardhi, 10 wilayani Kibaha mkoani Pwani na hivi mashamba ya watu wakubwa 10 yaliyopo Kilombero mkoani Morogoro yatafutwa hati miliki zake.
Alisisitiza kuwa haiwezekani matajiri kula maisha mazuri wakiwa mijini na kuyatelekeza au kuyakodisha kwa wazawa wasio na ardhi. Alipotafutwa baada ya mkutano ili kufafanua vigogo waliohusika na umiliki wa mashamba hayo, Lukuvi hakupatikana.
Wakati huo huo, serikali imefuta hati miliki za mashamba 48 yaliyokuwa yanamilikiwa na wawekezaji wilayani Monduli. Kwa mkoa wa Manyara, Rais amefuta hati miliki ya shamba la Ufyomi Gallapo Estate, lenye ukubwa wa ekari 120 ili kufidia wananchi 340 waliohamishwa kupisha Hifadhi ya Tarangire.
Recent Comments