Kundi la waadamanaji wanaounga mkono mapinduzi Burkina Faso wamevamia hoteli ya Laico mjini Ouagadougo Jumapili (20.09.2015) ambayo ilikuwa iandae mazungumzo yenye lengo la kurudisha serikali ya mpito ya kiraia.
Baadhi ya waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye kuashiria kuunga mkobo utawala wa kijeshi unaongozwa na kikosi maalum cha ulinzi wa rais RSP ambacho kiliingia kwa nguvu kwenye mkutano wa baraza la mawaziri hapo Jumatano na kutibua kipindi cha utawala wa mpito ambacho kilikuwa kimalizikie kwa uchaguzi hapo tarehe 11 mwezi wa Oktoba.
Shuhuda mmoja wa shirika la habari la Uingereza Reuters amekaririwa akisema walivamia hoteli hiyo kwa matumizi ya nguvu ambapo “waliwashambulia wanachama wa zamani wa upinzani wakati walipokuwa wanawasili ” ameongeza kusema kwamba ” mmoja wao ilibidi aokolewe na vikosi vya usalama kutoka umma wa watu.”
Balozi wa Ufaransa nchini Burkina Faso Gilles Thilbault ameandika katika mtandao wake wa Twitter ” Nilikuwa na wenzangu.Tuko salama. Hatukushikiliwa mateka.Tuko huru.”Ubalozi wa Marekani mjini Ouagadougou umekanusha taarifa kwamba balozi wake Tulinabo Salama Mushingi amejeruhiwa katika vurugu hizo.
Vurugu kwenye hoteli
Rais Macky Sall wa Senegal mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS ambaye anaongoza juhudi hizo za upatanishi baadae aliondoka kwenye hoteli hiyo.
Haikuweza kujulikana iwapo mazungumzo hayo ambayo yalipangwa kuhudhuriwa miongoni mwa makundi mengine mashirika ya kiraia, vyama vya kisiasa na jeshi yangeliweza kuendelea licha ya vurugu hizo.
Waandamanaji wanaopinga mapinduzi wamekuwa wakijikusanya barabara ya pili kutoka hoteli hiyo Jumapili asubuhi kabla ya kuanza kwa mkutano huo wakati wanajeshi wa kikosi maalum cha ulinzi wa rais RSP kilipowasili na kuanza kuwapiga.
Waandamanaji hao walikimbilia kujificha kwenye viwanja vya hoteli hiyo lakini wanajeshi zaidi wa kikosi hicho waliwasili baadhi yao wakificha nyuso zao kwa vifuniko na kufyetuwa risasi hewani kuwatawanya waandamanaji hao Wanajeshi hao walisindikizwa na waandamanaji wanaounga mkono mapinduzi ambao baadae waliuvamia ukumbi wa hoteli hiyo.
Kisa cha mapinduzi
Mashuhuda waliwatambuwa waandamanaji kadhaa wanaounga mkono mapinduzi kuwa ni wanamgambo kutoka chama cha Maendeleo na Demokrasia CDP ambacho ni chama tawala cha zamani wakati wa utawala wa Rais Blaise Compaore.
Compaore alipinduliwa mwaka jana na uasi wa umma wa wale waliokuwa wakipinga jaribio lake la kutaka kubadili katiba na kurefusha utawala wake wa miaka 27.Tokea wakati huo nchi hiyo imekuwa ikiongozwa na serikali ya mpito iliokuwa na majukumu ya kuandaa uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Generali Gilbert Diendere mkuu wa upelelezi wa zamani wa utawala wa Compaore na msaidizi wake mkuu amesema amefanya mapinduzi hayo kutokana na mipango ya kukivunja kikosi hicho cha ulinzi wa rais na kwa sababu washirika kadhaa wa rais wa zamani wamepigwa marufuku kushiriki katika uchaguzi huo.
Kurudishwa serikali ya mpito
Rais Thomas Boni Yayi wa Benin ambaye yeye na Rais Macky Sall wa Senegal wanasuluhisha mzozo huo amesema hapo Jumamosi usiku kwamba baraza la kijeshi lililotwaa madaraka nchini Burkina Faso liko tayari kuruhusu kurudishwa kwa serikali ya mpito.
Rais wa muda wa Burkina Faso Michel Kafando ambaye alikamatwa na kikosi cha ulinzi wa rais hapo Jumatano kabla ya kuachiliwa siku mbili baadae alikuwa pembeni mwa rais huyo wa Benin wakati akitowa tangazo hilo.
Mkutano na waandishi wa habari uliokuwa umepangwa kufanyika Jumapili umefutwa wakati hali ya mvutano ikionekana kuyumbisha juhudi za kidiplomasia kutatuwa mzozo huo.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters/dpa
Mhariri : Oumilkheir Hamidou
OP The East African
Recent Comments