TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimedai hakitakabidhi madaraka kwa upinzani hata ikishindwa katika uchaguzi mkuu kuwa ni potofu.
Tume hiyo ilifafanua kuwa, Mbowe aliitafsiri vibaya kauli ya CCM iliyowataka wananchi wakipigie chama hicho kura nyingi ili kiwashinde wapinzani wake. Akitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema, âTume imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo, kauli na sheria mbalimbali za uchaguzi katika kipindi hiki cha kampeniâ.
Alisema wapo makini na kazi yao na wanafuatilia mwenendo wa kila chama na wagombea wake kuona endapo sheria na taratibu za uchaguzi zinafuatwa, ikiwa ni pamoja na kuangalia iwapo kauli zinazotolewa na wagombea wa vyama mbalimbali hazihatarishi amani.
Jaji Lubuva alisema, Mbowe aliitaka tume hiyo itoe ufafanuzi kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo kuwa CCM haiko tayari kuachia madaraka upinzani hata kama watashindwa.
Lubuva alisema, walichelewa kutoa ufafanuzi huo kwani walikuwa wanafuatilia taarifa hiyo kwenye chombo cha habari kilichodaiwa kuirusha. Alisema, baada ya kufuatilia video na kuisikiliza, walibaini Bulembo kusema maneno haya, âJamani tumwogope Mungu, CCM kuna jambo hatujalifanya na hatutalifanya na wana haki ya kulalamika, mnalifahamu ni jambo gani hilo?â â…Hapana, hatuwezi kuwaruhusu kwenda Ikulu, mengine yote tunaruhusu, lakini kwenda Ikulu, hapana.â
Lubuva alisema, matamshi hayo ya Bulembo hayakuwa na maana kwamba CCM hata kama ikishindwa haitaruhusu upinzani kuingia Ikulu kama alivyodai Mbowe, bali yalikuwa ni maneno ya kisiasa yaliyohamasisha kupigwa kura nyingi kwa chama hicho.
Alisema, hata wagombea wa Chadema pia kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisikika wakisema, âHuu ndio muhula wa mwisho wa CCM kuongoza nchi, wakimaanisha kuwa wananchi wawapigie wao kura nyingi ili washinde vyama vingine vyote na kushika dolaâ.
Alisema kuwa anapenda kuwahakikishia wananchi kuwa tume ya uchaguzi ndio yenye mamlaka kamili ya kutangaza nani ameshinda na kwa kiasi gani cha kura, hivyo haoni sababu ya vyama kuendelea kuwahangaisha wananchi kwa kauli zisizofaa ambazo, hata hivyo alizikemea.
Kutokana na maelezo yake, hadi kufikia sasa, mara baada ya kazi ya kuhakiki majina katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, jumla ya wapiga kura milioni 23.7 wameandikishwa na watapiga kura katika uchaguzi huo wa Oktoba 25.
Recent Comments