SIKU moja baada ya Serikali kutangaza kuwa mahujaji 50 wa Tanzania waliokuwa katika Mji Mtakatifu wa Makka, Saudi Arabia, hawajulikani walipo tangu kutokea kwa tukio la kukanyagana na kusababisha vifo vya watu 769, imesema imepokea majina 18 ya watu ambao hawajulikani walipo.
Katika tukio lililotokea eneo la Mina, nje kidogo ya Makka, Alhamisi iliyopita ambayo ilikuwa ya maadhimisho ya Sikukuu ya Idd el Haji, mahujaji watano wa Tanzania waliripotiwa kufa, na wengine kujeruhiwa.
Taarifa ya Serikali kwa vyombo vya habari jana, iliwataja mahujaji wa Tanzania ambao hawajaonekana kuwa ni Abdul Iddi Hussein, Awadh Saleh Magram, Burhani Nzori Matata, Yussuf Ismail Yusuf, Saleh Mussa Said, Adam Abdul Adam na Archelaus Antory Rutayulungwa.
Wengine ni Farida Khatun Abdulghani, Rashida Adam Abdul, Hamida Ilyas Ibrahim, Rehema Ausi Rubaga, Faiza Ahmed Omar, Khadija Abdulkhalik Said, Shabinabanu Ismail Dinmohamed, Salama Rajabu Mwamba, Johari Mkesafiri Mwijage, Alwiya Sharrif Salehe Abdallah na Hafsa Sharrif Saleh Abdallah Aidha, ilisema mbali ya taarifa za kupatikana kwa majina hayo, Wizara imepokea taarifa ya kutambuliwa kwa mwili wa mmoja wa Tanzania anayeitwa Hadija Shekali Mohammed wa kikundi cha Ahlu Daawa.
âSerikali ya Saudi Arabia imetoa picha za maiti za mahujaji waliokufa Makkah ambao wamehifadhiwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti kwa ajili ya utambuzi. Hivyo, Ubalozi wa Tanzania nchini humo kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission pamoja na vikundi vya mahujaji unaendelea na zoezi la kuzihakiki picha hizo ili kubaini kama zinalingana na sura za mahujaji wetu waliopotea.
âPia Mamlaka ya Serikali ya Saudi Arabia imesema kuwa imechukua alama za vidole za mahujaji waliokufa ili wazilinganishe na zile walizozichukua Uwanja wa Ndege wakati mahujaji hao wakiingia nchini humo.
Wizara inaamini kuwa taarifa za alama za vidole zitakapotolewa zitasaidia sana kuwatambua mahujaji wetu,â ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. Waanza kurejea Wakati huohuo, kundi la mahujaji 90 kati ya zaidi ya 3,000 waliokwenda Makka kuhiji kwa lengo la kutimiza moja ya nguzo kuu za Uislamu, wanatarajiwa kuwasili nchini leo alfajiri.
Idadi hiyo ya mahujaji ni wale ambao walipelekwa huko kupitia Taasisi ya Haji Caravan, wakati wengine wanatarajiwa kurejea nchini kesho na keshokutwa. Juzi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma, ilieleza kuwa mahujaji wa Tanzania ambao wapo salama, walimaliza ibada yao ya Hija Jumamosi iliyopita na juzi walitarajiwa kuanza safari ya kurejea nyumbani.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya mtandao akiwa Saudia, aliyekuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage ambaye alishiriki ibada hiyo, alisema msafara huo wa watu 90 wa Taasisi ya Haji Caravan utafika leo alfajiri. âSisi ambao tuko salama tutarejea nchini kesho (leo) alfariji. Tuko 90, ni wa taasisi moja, Haji Caravan. Lakini wengine watarudi Alhamisi na Ijumaa,â alieleza Rage.
OP Habari Leo
Recent Comments