Marekani kwa mara ya kwanza imefanikiwa kuufanya majaribio mfumo wake wa kudungua makombora ya masafa marefu ICBM kulingana na maafisa.
Mfumo huo wa ardhini uliwekwa katika kambi moja ya kijeshi mjini California na kudungua kombora la masafa marefu kulingana na kitengo cha ulinzi wa makombora MDA.
Pentagon imesema kuwa majaribio hayo yalikuwa yamepangwa muda mrefu uliopita, lakini yanajiri huku kukiwa na wasiwasi mkubwa na Korea Kaskazini.
Majaribio hayo yamefanyika baada ya Korea Kaskazini kufanyia majaribio kombora lake la tisa mwaka huu.
Mkurugenzi wa kitengo hicho cha ulinzi wa makombora Admirali Jim Syring amesema kuwa jaribio hilo ni hatua muhimu.
”Mfumo huu ni muhimu kwa ulinzi wa taifa letu na jaribio hili ni thibitisho kwamba tuna uwezo mkubwa dhidi ya tishio”, alisema siku ya Jumanne.
Lilikuwa jaribio la kwanza dhidi ya kombora la masafa marefu kwa mfumo huo wa ardhini GMD.
Mfumo huo ulirushwa kutoka Kwajalein Atoll katika kisiwa cha Marshal juu ya anga ya Pacific, kitengo hicho kilisema katika taarifa iliotolewa.
Tangazo hilo linajiri baada ya Korea Kaskazini kufanyia majaribio kombora lake la tatu katika kipindi cha wiki tatu.
Kombora hilo lilisafiri kwa urefu wa kilomita 450 kabla ya kuanguka katika maji ya Japan.
Recent Comments