HALI ya taharuki imeibuka katika Halmashauri ya Moshi baada ya madiwani kugomea mafunzo ya utaratibu ulioboreshwa wa uendeshaji  ruzuku ya maendeleo kwenye mamlaka za Serikali za mitaa (LGDG), wakishinikiza kulipwa posho ya Sh 100,000 kila mmoja.
Mafunzo hayo yaliyokuwa yanasimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), yalihusisha madiwani wote na wakuu wa idara jana katika ofisi za Halmashauri.
Taharuki iliibuka baada ya madiwani hao kuingia ukumbini na kabla ya mafunzo kuanza, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Michael Kilawila aliwatangazia kuwa kutokana na mafunzo kutokuwa ya kisheria, Halmashauri itapaswa kutoa posho zao kupitia makusanyo ya ndani.
Kilawila alisema kutokana na hali hiyo na mapato kuwa madogo, kila diwani atalipwa Sh elfu 60,000 kama posho ya siku moja ambapo siku mbili za mafunzo hayo kila mmoja angepokea Sh 120,000.
Baada ya tamko hilo hali iligeuka baada ya madiwani hao kuonesha kutoridhishwa na kiwango hicho cha posho na kugonga meza wakishinikiza kulipwa Sh 100,000 kwa siku kama wanavyolipwa kwa vikao vingine vinavyotambulika.
Waliposhindwa kuelewana, madiwani hao walisusia mafunzo hayo na kuondoka hali iliyowalazimu wakufunzi kutoka Tamisemi kufundisha wakuu wa idara peke yao.
Akizungumzia sintofahamu hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Butamo Ndalahwa alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha madiwani kwa kushirikiana na wananchi, wanaibua miradi.
Ndalahwa alisema mafunzo hayo yanafanyika katika halmashauri zote nchini na kuwa madiwani hao waligoma wakitaka posho kubwa bila kujali kuwa mafunzo hayo yangenufaisha wananchia ambao ndio waliowachagua.
Mkurugenzi huyo akionesha masikitiko, alisema jambo hilo la kugomea mafunzo litasababisha maendeleo ya Halmashauri kurudi nyuma kwa kukosa elimu ya uibuaji miradi ambayo inakubalika.
âNimesikitishwa kwa kiasi kikubwa, madiwani wameonesha kutangulia mbele maslahi yao badala ya kutumikia wananchi waliowachagua, tumewaelimisha kuhusu posho, kwa nini tunawapa Sh 60,000 lakini hawakutaka kuelewa na badala yake waligonga meza ovyo na kutoka nje,â alisema Ndalahwa.
Kilawila alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia suala hilo na hatima yake, alisema hawezi kuzungumzia jambo lolote mpaka kikao cha madiwani kitakapokaa ili kutoa maazimio.
âNinachoweza kusema sasa ni kwamba siwezi kuzungumza lolote, Â mtafute Mkurugenzi, mimi nasubiri ni kikao cha madiwani ili kutoa maazimio ya kilichotokea leo,â alisema Kilawila.
Recent Comments