GAZETI hili jana lilichapisha habari yenye kichwa cha habari âTume ya Utawala Bora yaonya wanasiasa.â
Onyo hilo lilitolewa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga juzi alipokuwa anazindua Ilani ya Uchaguzi ya asasi za kiraia kuelekea na baada ya Uchaguzi Mkuu.
Nyanduga alihadharisha kwamba baadhi ya kauli zinazotolewa na wanansiasa zinaweza kuwa chanzo cha kuhatarisha amani ya nchi. Katika hili alitoa mifano ya kauli hizo kuwa ni pamoja na ââSerikali tukiibiwa kura patachimbika,ââ Ushindi ni lazima,ââ Serikali haitolewi kwa vikaratasi,ââ Goli la mkono au ushindi saa nne asubuhi.ââ
Alifafanua zaidi kwa kusema kwamba kauli kama hizo zinaweza kudumaza mchakato mzima wa uchaguzi, licha ya uwezekano wa kuwa chanzo cha kuhatarisha amani. Tunapenda kuunga mkono tahadhari hiyo kwa kuwa imekuja wakati muafaka kwa vyama, huku kampeni za uchaguzi zikizidi kupamba moto kwa vyama vilivyoko katika kinyangâanyiro cha uchaguzi katika ngazi za udiwani, ubunge na urais.
Ni vizuri tukakumbushana kwamba hii ni mara ya tano katika historia ya Tanzania kuendesha uchaguzi katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa. Tulianza mfumo wa vyama vingi vya siasa katika serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa na ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete ambao, kila mmoja wao aliongoza kwa vipindi viwili vya miaka mitano.
Katika historia ya taifa hili, chaguzi zote hizi katika mfumo wa vyama vingi Watanzania walikuwa wanapambana kwa nguvu ya hoja na siyo hoja ya nguvu na kuleta mafarakano. Kampeni zilikuwa zinafanyika kwa ustaarabu wa kustahimiliana na kuvumiliana bila ushabiki wa kutaka kuwagawa wananchi kwa misingi ya dini, ukabila, itikadi na rangi.
Aina ya kauli ambazo zimebainishwa wazi na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwamba hazitutakii mema kama taifa hazina budi kuachwa kutokana na ukweli kwamba huo siyo utamaduni wa Mtanzania.
Utamaduni wa Mtanzania ni kuendesha masuala yake ya kisiasa kwa njia ya demokrasia, kwa kufuata misingi ya amani, utulivu, mshiakamo na umoja bila kubaguana. Kutokana na ukweli huu, basi tusitayarishe mazingira ambayo yatatulazimisha hapo baadaye baadhi yetu kupelekwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi kama alivyohadharisha Nyanduga.
Kila mmoja wetu awe mlinzi wa mwenzake kuepuka uwezekano wa kutumbukia katika vurugu zisizo na tija katika kusaka wenzetu watakaoliongoza taifa letu. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.
Recent Comments