SERIKALI imeelezea imani yake kwamba Mkataba mpya baina ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), ili shirika hilo liweze kutoa Dola za Marekani milioni 472.8 (karibu Sh trilioni moja) za kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, utatekelezwa.
Kauli hiyo ya Serikali iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue (pichani), Dar es Salaam jana, inafuatia hatua ya Bodi ya MCC kueleza wasiwasi wake kuhusu hali ya rushwa nchini Tanzania na kukubaliana kwamba ni lazima kwanza Tanzania ifaulu kufikia kigezo cha udhibiti wa rushwa kabla ya kupewa msaada huo.
Fedha hizo pia zimelenga katika uimarishaji wa taasisi zinazohusika na usambazaji wa nishati hiyo na usimamizi wake, kusaidia utekelezaji wa mipango ya mageuzi katika Sekta ya Nishati na kuchochea uwekezaji wa Sekta Binafsi.
Balozi Sefue akielezea hatua hiyo, alisema Tanzania inayo mategemeo makubwa ya kupata fedha hizo kutokana na ukweli kwamba imefanikiwa kukidhi vigezo vingine vyote vinavyohitajika na kwamba hata katika kigezo cha rushwa zipo jitihada zilizochukuliwa katika kukabiliana nalo.
Alisema kimsingi, MCC ambayo ipo chini ya Serikali ya Marekani, hutoa vigezo mbalimbali ili kuziwezesha nchi kufaidika na fedha hizo na kwamba Tanzania imeweza kupiga hatua kubwa katika kufikia Malengo ya Milenia, hatua ambayo Bodi ya MCC imepongeza.
âTumechukua hatua katika kukabili rushwa kubwa nchini. Mambo mengi yamefanyika ikiwemo kuboresha vyombo vinavyohusika na upambanaji wa rushwa nchini. Rushwa hii inayotajwa ipo katika dhana tu na si uhalisiaâ alisema.
Akizungumzia hatua zaidi zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete katika kukabili rushwa; Balozi Sefue alitaja uboreshaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo sasa ina uwezo wa Kukamata, Kuchunguza na Kupeleka Mahakamani masuala yote yenye harufu ya rushwa.
Aliitaja pia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa umma, ambayo pia imekuwa inafanya kazi kubwa ya kukabiliana na vitendo vya rushwa kwa viongozi wa umma na pia Idara ya Mahakama, ambayo sasa imekuwa inasikiliza mashauri yote yanayohusiana na rushwa kwa haraka na kutolea maamuzi.
Kuhusu imani ya serikali juu ya upatikanaji wa fedha hizo; Balozi Sefue alisema serikali ina amini kwamba kikao kijacho cha Bodi ya MCC kitakachokutana baadaye mwaka huu, kitaliangalia suala hilo kwa kina na bila shaka wataridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na rushwa.
âTuna uhakika tutafanikiwa kupata fedha hizi. Imekuwa ni bahati mbaya kwamba kikao cha Bodi cha Septemba ndicho kilichoonesha wasiwasi juu ya mapambano haya ya rushwa.
Kwa vile hatua za kupambana na rushwa bado zinaendelea kuchukuliwa; tuna imani kwamba hadi Desemba wenzetu hawa wataona na kuridhishwa na jitihada zetu na hivyo watatuona kuwa tumefikia vigezo vyote, na tunastahili kupewa,â alisema Balozi Sefue.
Recent Comments