RAIS Jakaya Kikwete amewataka majaji na mahakimu kufanya kazi kwa ufanisi, hususani kumaliza kesi kwa muda mfupi ili kutoa haki sitahiki kwa wananchi.
Mwito huo wa Rais Kikwete aliutoa juzi alipokuwa akifungua mkutano wa Chama cha Majaji, Afrika Mashariki uliomalizika jana mjini Mwanza.
Tunaamini, mwito huo uliolenga kuwakumbusha wajibu wao wa kila siku, lakini safari hii kwa msisitizo zaidi. Tunasema ni kwa msisitizo kwa kuwa Rais Kikwete tangu aingie madarakani miaka 10 iliyopita, kati ya sekta alizozipa kipaumbele ni pamoja na ya utoaji haki kwa wananchi ambapo katika muda huo, ameweza kuapisha majaji wengi ili kuleta ufanisi katika idara ya mahakama, mintarafu suala zima la kupunguza mlundikano wa kesi.
Rais alisema serikali imeweza kuongeza bajeti ya shughuli za kimahakama kutoka Sh bilioni 36.6 mwaka 2005 hadi kufikia Sh bilioni 90 kwa mwaka huu. Hii yote ni kuhakikisha utendaji wa mahakama unakuwa wa kifanisi zaidi.
Ni ukweli ulio wazi kwamba kumekuwepo na ucheleweshwaji wa kesi nyingi hasa zile zinazohitaji maamuzi ya majaji, na kwa kuliona hilo, Rais Kikwete akaongeza majaji wa kutosha ili kesi hizo ziweze kuamuliwa kwa haraka zaidi na kuwezesha haki kutendeka.
Kuna kesi za mauaji na za madai katika mahakama zetu ambazo zimekaa miaka mingi bila kufikiwa uamuzi kutokana na uchache majaji huku baadhi ya wahusika wakifariki dunia bila kupata haki zao.
Wanasheria wanasema: Suala si kutoa haki, bali ni kuona haki inatendeka kwa wakati. Haki haiwezi kutendeka kama watendaji ni wachache. Na ndio maana Rais anasisitiza ufanisi kwa majaji waliokutana juzi na jana kujadili mfumo mzima wa utoahi haki.
Kumekuwepo na lawama za muda mrefu kwamba mahakama hazitendi haki na kwamba zimekuwa ni kero kwa kuwa pale inapoonekana haki haitendeki, wananchi hulazimika kupeleka malalamiko ya kesi zao kwa viongozi wa Serikali ili wapate haki yao.
Na hii si kwamba wananchi hao hawajui mgawanyo wa kazi kati ya mihimili hii, yaani Serikali na Mahakama bali ni kwa vile wanataka haki hiyo itendeke na msimamizi mkuu ni serikali yao. Kikwete anasema, ni bora majaji na mahakimu wafanye kazi yao tena kwa ufanisi. Wakifanya hivyo, kila mwananchi ataheshimu mipaka ya utoaji wa haki na hataenda kusikostahili kwa kuwa atakuwa amepata kile anachokitarajia.
Kushinda au kushindwa kesi, yote hayo ni haki ya mlalamikaji na mlalamikiwa. Na huo ndio utawatala wa sheria. Wakati nchi ikiwa katika kipindi hiki cha kampeni ambapo wagombea wanajinadi ili wapate kura kutoka kwa wananchi bila shaka tutashuhudia pia ukiukwaji wa haki za raia.
Wapo watakaotumia matusi, kashfa na ukiukwaji wa taratibu zilizowekwa. Ni imani yetu kwamba majaji watafanyia kazi ushauri wa Rais kwa kujipanga ipasavyo katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwani wakati mwingine watu kutopata haki huwa ni mwanzo wa vurugu.
Recent Comments