LEO Watanzania wanatarajiwa kufanya uamuzi wa kihistoria wa kuchagua Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge wa majimbo na madiwani wa kata wanakoishi, katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchi nzima.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya kukamilika kwa siku zaidi ya 60 za kupiga kampeni jana, ambapo vyama vyote vilivyosimamisha wagombea wa urais, ubunge na udiwani vilikamilisha kampeni zao.
Tangu kampeni zilipoanza, viongozi mbalimbali wa kiserikali, kijamii na kisiasa pamoja na wagombea wote, walihamasisha wananchi kuhakikisha leo wanajitokeza kupiga kura baada ya kusikiliza sera na ahadi za wagombea mbalimbali na kuwapima.
Miongoni mwa viongozi hao ni Rais Jakaya Kikwete, ambaye kwa nafasi yake ya Mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, amewahakikishia Watanzania kuwa usalama na ulinzi wao utakuwa wa hali ya juu kuanzia leo wakati wa kwenda kupiga kura, wakati wa kupiga kura, kuhesabu na kutangaza washindi.
NEC Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, aliwataka Watanzania waliojiandikisha kupiga kura kuchagua viongozi wao bila hofu.
âKwanza niwapongeze wote pamoja na vyama vya siasa kwa kufanya kampeni kwa utulivu, niwaombe kesho (leo), jitokezeni kwa wingi mliojiandikisha kupiga kura kuchagua viongozi mnaowataka, msihofu, ulinzi upo,â alisema Jaji Lubuva.
Jaji Lubuva alisema vifaa vyote vya uchaguzi vimeshawasili kwenye maeneo ya uchaguzi na kazi iliyobaki ni leo wapiga kura kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi wao na vituo vitakuwa wazi kuanzia saa moja asubuhi hadi saa kumi jioni.
Idadi, matokeo Amesema idadi kamili ya wapigakura wanaotarajiwa kupiga kura leo ni Watanzania 23, 254, 485 na watapiga kura kwenye vituo 63,156 vya Tanzania Bara na vituo 1,580 vya Zanzibar.
Akizungumzia ni lini matokeo ya urais yatatangazwa baada ya kupiga kura, Jaji Lubuva alisema wanatarajia matokeo hayo yatangazwe ndani ya siku tatu hadi nne baada ya kazi ya kupiga kura kumalizika.
OP Habari Leo
Recent Comments