Rais wa Guatemala Otto Perez Molina amejiuzulu baada ya bunge kumuondolea kinga ya kutoshitakiwa kufuatia tuhuma za kujihusisha na masuala ya rushwa.
Duru nchini humo zinaarifu kuwa Molina aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwake hapo jana usiku baada ya Jaji nchini humo kutoa amri ya kukamatwa kwake kuhusiana na tuhuma hizo za rushwa ambazo tayari zimesababisha kutiwa jela kwa makamu wake na kujiuzulu kwa baadhi ya mawaziri wake.
Hatua hiyo ya Jaji wa nchi hiyo ni ya kipekee katika kushughulikia tuhuma za rushwa zinazowakabili wanasiasa katika taifa hilo la Amerika ya kati.
Rais huyo wa Guatemala sasa atatakiwa kujibu tuhuma hizo zilizohusiana na kupokea fedha kwa njia ya rushwa .
Molina asema hana hatia katika kashifa ya rushwa
Hata hivyo Perez Molina mwenye umri wa miaka 64 amesisitiza kuwa yeye hana hatia na yuko tayari kukabiliana na hatua zote za kisheria zitakazofuata kuhusiana na kashfa hiyo.
Hakuna mashitaka kamili ambayo tayari yamewekwa wazi ingawa mwanasheria mkuu wa serikali Thelma Aldana amesema kuwa tayari uchunguzi wa awali unaendelea kuhusiana na Rais Molina kuhusika na kashfa hiyo.
Naye wakili wa Rais huyo Cezar Calderon aliliambia shirika la habari la Associated Press ya kuwa Rais huyo wa Guatemala yuko tayari kwenda mahakamani kwa hiari yake kujibu tuhuma hizo mara tu zitakapotolewa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais wa Guatemala aliyeko madarakani kushitakiwa, ingawa baadhi yao wamekwishakabiliwa na hali ya aina hiyo lakini baada ya kuondoka madarakani.
Mtandao wa uhalifu
Kashifa hiyo ya rushwa ilifichuliwa na waendesha mashitaka na kamisheni ya umoja wa mataifa iliyokuwa inachunguza mtandao wa uhalifu nchini Guatemala ambapo wafanyabiashara nchini humo walitoa rushwa katika mamlaka za juu ili waweze kukwepa kulipa kodi ya uingizaji bidhaa nchini humo mtandao ambao unadaiwa kuligharimu taifa hilo mamilioni ya fedha.
Kashifa hiyo pia tayari imemgharimu kazi yake makamu wa Rais wa nchi hiyo Roxina Baldetti ambaye katibu muhtasi wake wa zamani anadaiwa kuwa kiongozi wa mtandao huo wa rushwa.
Makamu huyo wa Rais ambaye alijiuzulu wadhifa wake Mei 8 , mwaka huu tayari yuko jela akisubiri kujibu mashitaka ya kupokea rushwa ya mamilioni ya dola. Hata hivyo na yeye pia amesema hana hatia katika sakata hilo.
Waandamanaji nchini humo wamekuwa wakiijaza mitaa nchini humo karibu kila siku wakishinikiza sio kujiuzulu tu kwa Rais Molina bali pia uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika jumapili wiki hii uahirishwe.
Katiba ya nchi hiyo inamkataza Perez Molina kuwania muhula mwingine wa uongozi na yeyote atakayechukua nafasi yake katika uchaguzi huo ataanza rasmi kazi hiyo mwezi January.
Mwandishi: Isaac Gamba/APE/AFPE/EAP
Mhariri: Gakuba Daniel
Recent Comments