VIONGOZI wa dini wametakiwa kutoegemea upande wowote wa vyama vya siasa ili kuepusha mpasuko unaoweza kutokea, huku wanasiasa wakiaswa kukubaliana na matokeo kwa kuwa ndiyo mwisho wa ubishi.
Ushiriki wa viongozi wa dini katika vyama vya siasa imeelezwa kwamba kuna hatari ya kusababisha mgawanyiko kwa wananchi kutokana na kuwa na imani na viongozi wao wa dini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Pentekoste nchini (PCT), Askofu Dk David Mwasota wakati akizungumza kwenye kongamano la majumuisho ya makongamano 19 yaliyofanyika katika mikoa mbalimbali nchini.
Alifafanua kwamba viongozi wa dini hawatakiwi kuwa na vyama vya siasa kwani wanaongoza waumini wenye vyama, hivyo viongozi hao kujiingiza katika siasa ni kuleta mpasuko mkubwa.
âMakanisa au misikiti ina waumini tofauti na wenye vyama tofauti, kwa hiyo sisi viongozi wa dini hatupaswi kuwa wabaguzi kwa kuegemea katika upande mmoja, mfano ni Kenya. Hii kitu ilitokea na ndio maana vurugu zilipoanza watu walichoma makanisa,â alisema Dk Mwasota.
Alisema hata katika Biblia imeandikwa kura huondoa ubishani, hivyo hata viongozi wa kisiasa wajiandae kukubaliana na matokeo ya aina yoyote kwani maamuzi yatakuwa yametolewa na wananchi kwa njia ya kura.
âKura huondoa ubishani, kwa hiyo tuwahamasishe wananchi kujitokeza kupiga kura kwa wingi ili tumalize ubishi kwa kumpata Rais mmoja atakayeamuliwa na kura,â alisema.
Aidha, aliwataka viongozi wa kisiasa kuacha kutoa kauli zenye vitisho kwa wananchi ili kuepusha kuwapa hofu na kupiga kura kwa woga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa Pentekoste Tanzania, Askofu Pius Ikongo alipongeza hatua ya viongozi wa kisiasa kufanya kampeni zao kwa njia alizoziita za kisayansi, kwani mpaka sasa hakuna matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza.
Alisema kikubwa kinachotakiwa kuangaliwa na viongozi hao ni amani ya nchi ambapo aliwasihi kuendelea kutumia njia hizo alizoziita za kisayansi ili kuhakikisha uchaguzi unapita na kumalizika salama bila kuwepo kwa uvunjifu wa amani ya nchi.
OP Habari Leo
Recent Comments