WAKATI dunia ikishuhudia athari zilizokithiri za mabadiliko ya tabianchi, wadau nchini wamependekeza utumiaji wa maarifa yanayoendana na uhalisia wa nchi husika kuwa miongoni mwa hatua muhimu zitakazofanikisha kuongoa mfumo Ikolojia wa eneo husika.
Wamesema kufanya hivyo haimaanishi kupuuza njia zinazopendekezwa na ulimwengu, lakini ni budi kuwepo mbinu za kitaifa kwa kuwa zitafanyika kulingana na hali ya nchi husika na hivyo kufikia mafanikio ya haraka.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mdau wa Mazingira, Barack Lenga, wakati wa warsha ya wadau kuhusu matumizi ya Nishati mbadala ili kuongoa mfumo Ikolojia iliyoandaliwa na Asasi ya Kiraia inayojihusisha na mabadiliko ya tabianchi (FORUMCC) na kufanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja na kuwepo kwa mbinu za ulimwengu katika kukabiliana na athari hizo, ni muhimu jamii ya Tanzania ikatumia ujuzi wake kuwa na mbinu inazoona zinaendana na uhalisia wa taifa katika kuongoa mfumo Ikolojia.
Kwa mujibu wa Lenga, inawezekana sababu za kuchelewa kufanikiwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika nchi zinazoendelea inatokana na kutumia mfumo usioendana na hali halisi ya taifa husika.
“Kweli tunapewa mapendekezo na Jumuiya ya kimataifa, lakini tunapaswa ‘ku-localize’ mifumo ya kukabiliana na athari hizi, hapa tutatengeneza njia rahisi na itakayoeleweka na watu wetu naamini tutafanikiwa,” alibainisha.
Msololo Onditi, ni Mtaalamu wa Maendeleo ya Maisha na Mabadiliko ya Tabianchi FORUMCC, alisema kitaalamu kuna namna mbili za kukabiliana na athari hizo.
Alizitaja namna hizo ni kuendana na athari hizo na nyingine ni kuzipunguza ambazo zote kimsingi zinapaswa kufanywa kwa pamoja.
Onditi alifafanua kuwa FORUMCC kwa kushirikiana na PACJA imekuwa ikifanya mikakati kuwajengea uwezo wadau wa sekta mbalimbali ili wakautumie katika shughuli zao na kuongoa mfumo Ikolojia.
Hata hivyo, alishauri serikali pamoja na juhudi inazofanya kukabiliana na athari hizo, izihusishe mamlaka husika kuunda sera au sheria kamili ya mabadiliko ya tabianchi ili kila mmoja awe na wajibu wa kuifuata.
Naye Ezekiel Dembele, Ofisa wa Taasisi inayojihusisha na ufanyaji tathmini za mazingira wakati wa utekelezwaji wa miradi, alisema sekta binafsi kuna mambo muhimu inahitaji ili kufanya shughuli zake kwa kuzingatia uongofu wa Ikolojia.
Alisema ni vyema serikali iendelee kufanya punguzo la tozo mbalimbali katika uwekezaji ili washiriki ipasavyo kuwekeza katika miradi ya nishati mbadala.
“Pamoja na yote pia serikali iangalie suala la kupunguza urasimu katika ufuatiliaji wa tathmini na athari za mazingira (EIA), ambapo shida hujitokeza wakati wa kupitisha na hata gharama zake ni kubwa,” alibainisha.
Recent Comments