TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa uamuzi wa rufaa sita kati ya 13 za wagombea ubunge zilizokuwa hazijafanyiwa maamuzi kutokana na vielelezo vyake kutokamilika na kuamua kuyatupa mapingamizi yote, hivyo wagombea wake kutakiwa kuendelea na mchakato wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Kati ya wagombea hao sita waliopata baraka za NEC jana ni pamoja na mawaziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, Profesa Jumanne Maghembe wa Wizara ya Maji na Dk Abdallah Kigoda anayeshughulikia Viwanda na Biashara. Mwingine ni Daniel Nsanzugwanko, mbunge na naibu waziri wa zamani.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, NEC imezikataa sababu za rufaa zote na kukubaliana na uamuzi wa wasimamizi wa Uchaguzi, hivyo maamuzi yaliyofikiwa awali ya kuwapitisha kuwa wagombea, wanapaswa kuheshimika.
Katika rufaa zilizotolewa uamuzi, katika Jimbo la Mwanga, John Kilewo wa Chadema ameshindwa rufani mbili alizokata dhidi ya Anderson Msuya wa NCCR-Mageuzi na Prof Maghembe wa CCM.
Aidha, katika jimbo la Handeni Mjini, Daudi Lisewa wa Chadema amekwama katika rufani yake ya kumpinga Dk Kigoda wa CCM huku katika Jimbo la Kasulu Mjini, Nsanzungwanko amepitishwa baada ya rufaa ya Boniface Bunyago wa NCCR-Mageuzi kukwama.
Wengine walioshinda rufani zao ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Gerson Lwenge wa Jimbo la Wangingâombe (CCM) ambaye awali alipingwa na Dismas Luhwago wa Chadema.
Khatan Ahmad Khatan wa CUF katika Jimbo la Tandahimba, naye alishinda rufani yake iliyokuwa imekatwa na Likumbo Shaibu wa CCM. Ilisema taarifa hiyo kuwa Tume imekataa rufaa na wagombea wote waendelee na kampeni za uchaguzi.
Aidha, NEC imesikiliza rufaa za madiwani 70 kati ya rufaa 118 zilizokuwa hazijafanyiwa maamuzi kutokana na vielelezo vyake kutokamilika, kati ya rufaa hizo zilizoamuliwa 14 zimekubaliwa na na wagombea waliokuwa wameenguliwa wamerudishwa kugombea.
âHii ina maana kuwa Tume imetengua uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi na kuwarejesha wagombea katika kinyangâanyiro cha udiwani katika kata zao,â ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Awali, NEC ilipokea jumla ya rufaa 55 za ubunge na 200 za madiwani, hivyo kufikia jana imetolea uamuzi rufaa 48 za ubunge na 152 za ubunge.
Recent Comments