HARIBIFU wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji ni miongoni mwa changamoto kubwa katika maeneo mengi mkoani Dodoma hususan wilayani Kondoa.
Ukataji miti, upasuaji mbao, uchomaji moto misitu, uchomaji mkaa na kilimo cha uvamizi katika misitu na vyanzo vya maji ni sehemu tu ya uharibifu huo. Mwaka jana serikali mkoani Dodoma ilipiga marufuku ukataji miti, kilimo na uchungaji mifugo kwenye safu za milima ya vijiji vya Mafai, Haubi, Ntomoko na Kitongoji cha Mwisanga kuwa shughuli hizo zimesababisha uharibifu wa mazingira.
Kazi hizo zimehatarisha uhai wa chanzo cha maji cha kihistoria cha Ntomoko kinachohudumia vijiji takribani 17 vya wilaya za Kondoa na Chemba. Wananchi, viongozi na wadau wa mazingira wametakiwa kuhakikisha kata ya Haubi inarudisha sifa yake ya utunzaji mazingira na kunusuru chanzo cha maji cha Ntomoko. Serikali imetoa shilingi bilioni tatu kukikarabati chanzo hiko na miundombinu ya kusambazia maji kwenye vijiji hivyo 17. Chanzo hicho kimeasisiwa na Baba wa Taifa, Julius Nyerere miaka ya 1970.
Wakati huo Mwalimu Nyerere aliweka kambi katika eneo hilo na kushiriki kazi ya kuchimba mitaro ya kusambazia maji vijijini. Katika Wilaya ya Kondoa shughuli za kuhifadhi wa mazingira na usimamizi wa misitu zimeanza kwa kasi miaka ya 1973 baada ya kuanzishwa Hifadhi ya Ardhi Dodoma (HADO). HADO wamefanya kazi hadi mwaka 2006 mradi uliokuwa ukifadhiliwa na watu wa Sweden ulipokwisha muda wake. Baada ya mradi kwisha kazi hizo zimeendelea kufanywa na idara za serikali hadi sasa.
Kazi ambazo zimefanyika za kuwezesha uhifadhi wa mzingira kwa serikali na wadau katika wilaya hiyo ni pamoja na kuunda Kamati ya Hifadhi ya Mazingira ya Kijiji kwa serikali za vijiji 97 na serikali za mitaa 11.
Imeandaliwa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 17 kikiwemo cha Mnenia, Itundwi, Filimo, Masange, Kandaga, Mapinduzi, Kisese Sauna, Madege, Kikore, Mkurumuzi, Mitati, Puhi, Salanka, Masawi, Bukulu, Humai na Kwadimu, Yametengenezwa makingamaji ya kuzuia mmomonyoko wa udongo katika eneo la hifadhi ya ardhi Dodoma na vijiji vinavyozunguka milima.
Wataalamu wamewezeshwa kuelewa kuhusu namna ya kutekeleza usimamizi shirikishi wa misitu na hata Jumuiya ya Uhifadhi wa Misitu ya Salanga na Isabe (JUHIBEKO) imeundwa na inafanya kazi. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Isdory Mwalongo anasema, uharibifu wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji imekuwa kero kubwa kwenye maeneo mengi ya wilaya hiyo ikijumuisha ukataji miti, ufyekaji miti, upasuaji wa mbao, uchomaji moto misitu, uchomaji mkaa na kilimo cha uvamizi katika misitu na vyanzo vya maji.
Mwalongo anasema, Halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa ikifanya jitihada kupambana na uharibifu wa mazingira, lakini kuna changamoto kadhaa zinazokwamisha, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa utashi wa kisiasa katika kusimamia shughuli za uhifadhi wa mazingira na baadhi ya viongozi wa vijiji kutoa uchochezi kwa kutoa taarifa za uongo kwenye ngazi ya wilaya.
Anabainisha kuwa baadhi ya viongozi wanajihusisha na uharibifu wa mazingira kwa kushirikiana na waharibifu wengine, hivyo wanashindwa kusimamia sheria. Anakitaja kikwazo kingine ni urasimu katika uendeshaji kesi za uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kazi ya upelelezi kuchukua muda mrefu sanjari na waharibifu kupewa kifungo cha nje na kurudi maeneo yao kuendelea kuharibu.
âKuna urasimu katika uendeshaji wa kesi za uharibifu wa mazingira kwani zoezi la upelelezi huwa linachukua muda mrefu sana, matumizi ya sheria ambazo ni kama zimepitwa na wakati kwani zimekuwa ni za muda mrefu sana,â anasema Mwalongo. Anasema baadhi ya wananchi kwenye maeneo yenye uharibifu wamekuwa na tabia ya kuficha wahalifu kwa kutotoa taarifa za wanaoharibu kwa sababu za undugu.
Kwa mujibu wa Mwalongo, hali inakuwa ngumu zaidi wakati familia za wajumbe wa kamati za mazingira za vijiji zinapovamiwa baada ya kuchukulia hatua wahalifu. Anazitaja jitihada zinazofanyika kuhifadhi mazingira ni pamoja na kufanyika kwa doria katika misitu ya hifadhi na maeneo ya wazi, mapori ya akiba na wanyamapori ya Swagaswaga na Mkungunero. Anasema, elimu kwa njia ya vitendo imetolewa kuhusu matumizi bora ya nishati itokanayo na miti, kuni na mkaa kwa kufundisha jumla ya vikundi saba kutoka vijiji vya Kilo, Filimo, Puhi, Mnenia na Bukulu.
Askari 39 wa misitu wa vijiji kutoka katika vijiji 18 wamepata mafunzo kuhusu kuhifadhi wanyamapori na mazingira ngazi ya vijiji. Wataalamu wa wilaya na askari wamepata mafunzo na kununuliwa sare za kufanyia kazi.
Mwalongo anasema, makingamaji yamewekwa sehemu zenye miteremko mikali na mashamba katika kijiji cha Masange kuzuia mmomonyoko. âPamoja na jitihada ambazo wilaya imekuwa ikizichukua ili kuendeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira, bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma jitihada hizo ikiwemo upungufu wa rasilimali watu na rasilimali fedha,â anasema na kuongeza kuwa changamoto nyingine ni kukosekana kwa utashi wa kisiasa katika kusimamia shughuli za hifadhi ya mazingira.
Mwalongo anasema, mradi wa maji Ntomoko unakadiriwa kuhudumia watu 23,400 lakini kutokana na ongezeko la idadi ya watu kwa sasa inakadiriwa kuwa watu 60,000 wananufaishwa. Anasema, wakati mradi huo unaanzishwa vijiji 17 vilikuwa vinapata maji vikiwemo vya Kingkima, Mapango, Churuku, Igunga, Makirinya, Jinjo, Songolo Chandama, Mlongia na Jangalo.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewahi kutembelea mradi huo na kubainisha kuwa serikali itaipatia Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Sh bilioni 2.3 ili kuukarabati. Mradi huo umejengwa kuhudumia vijiji 17 vikiwemo viwili katika wilaya ya Kondoa na 15 wilayani Chemba. Mhandisi wa Maji Mkoa wa Dodoma, Bazil Mwiserya anasema mradi huo unaanza kufanyiwa ukarabati mkubwa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu.
Mwiserya anasema, zaidi ya wananchi 28,987 watanufaishwa na mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni tatu. Anasema sababu za kufa kwa mradi huo ambao umejengwa miaka ya 1970 ni uchakavu wa miundombinu pamoja na uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji miti unaosababisha uharibifu wa vyanzo vya maji. Kwa mujibu wa Mwiserya, baadhi ya wananchi kwenye maeneo kadhaa mkoani Dodoma wamekuwa wagumu kuchangia kutekeleza miradi ya maji hivyo kusababisha isiwe endelevu.
Recent Comments