WATU wawili, Said Abdallah (37) na Ally Mwishee (44), wameuawa kwa kupigwa risasi na kufa papo hapo katika uwanja wa mpira wa miguu wa shule ya Msingi Bonye, tarafa ya Bwakila, wilaya ya Morogoro jana.
Waliouawa walikuwa katika kikao cha kusuluhisha mgogoro wa mapenzi kati ya mume wa mke anayedai kufanya mapenzi na mtu mwingine chini ya Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Samata katika kijiji cha Bonye, Said Abdallah pamoja na watu wengine wawili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema tukio hilo la mauaji lilitokea juzi, majira ya saa mbili usiku katika eneo la kiwanja cha mpira cha shule ya msingi Bonye iliyopo katika tarafa ya Bwakila, wilayani Morogoro mkoani hapa.
Alisema kuwa kabla ya tukio hilo, kulikuwa na kikao cha watu hao watano ambao walikutana kusuluhisha mgogoro huo unaohusiana na masuala ya mahusiano ambapo Kamanda alimtaja Omary Ngaliwata alikuwa akimtuhumu Ally Mwishee kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wake aliyemtaja kwa jina la Zena ama Mama Shakira.
Kamanda huyo alisema kuwa, Mwishee ambaye kwa sasa ni marehemu alituhumiwa na Ngaliwata ya kwamba ana mahusiano ya kimapenzi na mkewe hali iliyosababisha Zena kutofautiana na mumewe Ngaliwata na kisha kuamua kuondoka nyumbani kwao.
Akielezea kwa kina tukio hilo, Kamanda Paulo alisema Agosti 27, mwaka huu kabla ya tukio hilo la mauaji, Mwishee alimpigia simu Ngaliwata na kumuomba wakutane ili waweze kusuluhisha mgogoro wao na kumaliza tofauti zao na inadaiwa awali Ngaliwata alitoa taarifa ya kwamba hatokuwepo, lakini baadaye alipatikana na kukubali kukutana na Mwishee ili wasuluhishwe tofauti zao.
Kamanda Paulo alisema kabla ya kukubali, Ngaliwata alitoa sharti ya kwamba usuluhisho huo ufanyike kwenye uwanja wa mpira wa shule ya msingi Bonye iliyopo kijijini hapo. Alisema ilipofikia majira ya saa mbili usiku waliwasili Mwishee na Abdallah pamoja na watu wengine wawili na walimkuta Ngaliwata tayari alishafika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda Paulo, kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Ngaliwata alitoa udhuru kuwa tumbo linamsumbua na hivyo aliondoka kwenye kikao na kwenda karibu na kichaka na muda kidogo alirudi kuungana nao, lakini ghafla watu wengine wawili wakiwa na pikipiki walifika eneo hilo na kuanza kuwashambulia kwa kuwafyatulia risasi.
Alisema katika mashambulizi hayo ya risasi, Mwishee alipigwa risasi upande wa mkono wa kulia na kutokea ubavuni upande wa kushoto ambapo Abdallah, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Samata alipigwa risasi begani na sikioni na hivyo kusababisha vifo vyao papo hapo.
Kamanda huyo alisema baada ya tukio hilo, Ngaliwata alikimbia mbio na kwenda kupora pikipiki yenye namba za usajili MC 775 AUG aina ya Sunlg iliyokuwa mali ya marehemu Mwishee na kisha kufuatana na wauaji hao na kukimbia kusikojulikana.
Alisema Polisi inawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni askari wa Wanyamapori, Haruni Salehe (36) pamoja na Athuman Salehe (45) na wanaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine akiwemo Ngaliwata ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Hilo ni tukio la pili katika kipindi cha siku nane mwezi huu yanahusisha wivu wa mapenzi na kusababisha vifo na madhara ya uharibifu wa mali. Katika tukio la kwanza lililotokea Agosti 20, mwaka huu, mkazi wa kijiji cha Mpofu, Tarafa ya Mngeta, wilaya ya Kilombero Bashiri Kadugula (25) anatuhumiwa kumuua mkewe Veronica Chabula (21) kwa kumkata na mapanga sehemu mbalimbali za mwili kwa wivu wa mapenzi.
Kutokana na tukio hilo watu zaidi ya 100, walikwenda kuvamia kituo kidogo cha Polisi Mbingu alikokuwa amehifadhiwa mtuhumiwa na baadaye kukichoma moto kituo hicho pamoja na ofisi ya Serikali ya kijiji cha Mpofu na polisi walifanikiwa kuwakamata watu 11.
Recent Comments