INGAWA vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja walikubaliana kuwa na uchaguzi huru, wa haki, uwazi, na wa kuaminika; mambo yanayotokea katika majukwaa halali na yasiyohalali yanaleta hisia tofauti na kauli za makubaliano ya wahusika katika mchakato wa uchaguzi.
Tunasema ni tofauti kwa kuwa kinachoendelea katika majukwaa hayo si majibu ya hoja ya matatizo ya Watanzania na tuhuma zinazowazunguka wenye kuwania mamlaka bali uoshaji wa nguo zao za ndani mbele ya hadhara.
Kama tunataka kuwa na amani, ustawi wa nchi, Usalama wa raia, uhuru wa vyama vya siasa na utii wa sheria ni dhahiri tunatakiwa kufuata kanuni na taratibu za uchaguzi na siyo kuibua hisia za kidini, kikabila na uzushi ambayo italeta shida kubwa.
Unapoona watu wenye ushawishi mkubwa katika makundi wanatumia nafasi zao za ushawishi kupandikiza mbegu ya uwongo ilhali wakijua ni uwongo, wakitumia nafasi zao hizo kugonganisha makundi mengine ni dhahiri tunajipeleka katika uwanda mkubwa wa mtafaruku usiokuwa na lazima.
Inafaa sana vyombo vinavyohusika kuangalia kwamba kuna utekelezaji wa makubaliano hayo, hivyo watu wakaacha kutumia ushawishi wao kuwamega Watanzania katika makundi na ni lazima watu hao waheshimu ukweli na kuacha kutayarisha matatizo.
Nchi hii ni yetu sote, wasiokuwa na nafasi hapa ni wachochezi wanaojifaragua katika mbawa mbalimbali za ushawishi wao. Kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 1985, (sura 343) kinachohusu maadili kinatakiwa kufuatwa kwa makini.
Na kila mmoja katika mchakato huo ajitahidi kuwa wazi kuhakikisha maadili haya yanajulikana kwa wafuasi na mashabiki wao na kuheshimiwa na wagombea na wanachama wote wa vyama vya siasa.
Katika ufuatiliaji wa maadili pia imeelezwa kuwa majengo wanayotumia kufanya kampeni sio ya ibada au sehemu zinazotumiwa kwa ajili ya ibada. Vile vile, vyama vya Siasa vihakikishe kuwa havitumii viongozi wa dini kupiga kampeni kwa ajili ya vyama vya siasa au wagombea wao.
Lengo kuu la maadili hayo ni kuzuia kutumika kwa ushawishi wa kidini katika kufanya maamuzi mazito ya kitaifa kwa kuwa wanaofanya hivyo wanatengeneza matabaka hatari yatakayoiingiza nchi hii katika mgogoro mkubwa wa kidini.
Maslahi ya taifa yanaweza kulindwa tu katika hili kama watu watapatiwa kiongozi anayejali taifa na wala si kuingia katika mamlaka kwa kupitia migongo ya kidini au ya umaarufu ambao utaleta songombingo katika taifa hili.
Athari ya watu wenye ushawishi kutumia ushawishi wao vibaya ni kuupasua umoja wa kitaifa uliojengeka katika misingi ya kuheshimiana na kutokuulizana dini wala kabila.
Tunaomba kwa heshima kubwa Watanzania tuache kufuatana na viongozi wanasiasa na hata wale watu wenye ushawishi kufanya mambo ambayo yataligawa taifa hili vipande viwili au zaidi kutokana na migongano ya maslahi binafsi ya watu.
Tuna haki ya kusema wazi kwamba hatupaswi kushabikia watu wa aina hii ambao mipango yao inaambatana na hila za kulitafutia balaa taifa hili. Mungu ibariki Tanzania.
Recent Comments