Hotuba ya Mwl. Mbelwa Petro, Mbunge wa wananchi jimbo la Biharamulo kwenye mkutano hadhara uliofanyika wilayani Biharamulo 11/03/2023.
________________________
Amani iwe nanyi nyote!
Naitwa Mwl. Mbelwa Petro, ndiye nilikuwa Mgombea wa kiti cha Ubunge kupitia CHADEMA katika jimbo letu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Naomba nisiache kuwashukuru wananchi wenzangu wote wa dini, kabila na vyama vyote vya siasa kwa kuhudhuria mkutano wetu CHADEMA kwani najua mmesitisha kwa muda shughuli za kutafuta unga na madaftari ya watoto ili mje kutusikia. Ninyi wageni wetu, siwashukuru tu bali nawapongeza pia kwa utume wenu kuzunguuka nchi nzima mkihubiri haki na Maendeleo ya kweli tunayoyataka Watanzania.
ILI NIWEKE VIZURI HOJA YA JINSI SERIKALI YA CCM INAVYOTUUMIZA NA KUKWAMISHA MAENDELEO YETU BIHARAMULO, NAOMBA NIELEZE KWA UFUPI KUHUSU JIOGRAFIA, UTAWALA NA MIPANGILIO YA KIUCHUMI YA WILAYA HII TANGU TUPATE UHURU 1961.
Biharamulo ni wilaya iliyoasisiwa mwaka 1961. Wilaya yetu ya Biharamulo ina Halmashauri moja iliyoanzishwa mwaka 1983 na kuanza kazi mwaka 1984. Wilaya ya Biharamulo ndiyo iliyoizaa wilaya changa ya Chato mnamo mwaka 2007. Baada ya kuondoa eneo lililokwenda kuunda wilaya mpya ya Chato, wilaya kongwe ya Biharamulo ilibakiwa na ukubwa wa 5627km², kati ya eneo hilo eneo lenye maji ni 10km² na eneo lenye Ardhi ni 5617km².
Kiutawala, wilaya yetu imegawanywa katika Tarafa mbili, Kata 17, Vijiji 79 na Vitongoji 379. Sensa ya mwaka 2012 idadi ya watu ilikuwa ni 323,486 na kabla ya matokeo rasmi ya sensa ya mwaka 2022 tunakadiriwa kuwa watu 390,000.
Kati yetu, 85% ya wananchi wa Biharamulo tunategemea shughuli za kilimo kujipatia kipato chetu na cha Taifa, 7% wakifanya ufugaji katika kulijenga Taifa, 5% hufanya shughuli za biashara, 1.6% ni watumishi wa sekta rasmi ikiwemo ya UMMA na Binasfi na 1.4% hufanya shughuli nyingine ikiwemo uselemala, usafirishaji, uchimbaji madini na uvuvi.
Kwa utangulizi huo, Ndugu wananchi na wageni wetu mtaona shughuli za kilimo, ufugaji na biashara ndio shughuli zinazochangia uchumi wa wananchi wa Biharamulo kwa 97%.
DHAMBI KUBWA ILIYOFANYWA NA SERIKALI YA CCM YA KUTUUMIZA NA KUTUFUKARISHA WANANCHI WA BIHARAMULOÂ NI:
Kuchukua 54% ya maeneo yetu sawa na 3033km² na kuyafanya yawe hifadhi hivyo haturuhusiwi kufanya shughuli yoyote huko iwe kilimo, ufugaji wala biashara. Wananchi tumebakiwa 46% tu sawa na 2583km² tu ambazo hazitutoshi kufanya kilimo kikubwa na cha kisasa kama tunavyotamani. Na sasa wafugaji wetu wameachwa bila maeneo ya malisho.
1. Vijana tukienda maeneo hayo kulima ili tujiajiri tunakamatwa, wengine tunakamatwa na kupotezwa, wapo ambao wanakamatwa na kukatwa unyayo wa miguu zao, wengine wanaosamehewa wanakamatwa na kufungwa jela miaka nyingi kama mvua.
2. Wafugaji wakimatiwa ng’ombe zao kwenye maeneo hayo hutozwa faini ya Tsh. 100,000 kwa kila ng’ombe mmoja bila huruma. Hii ina maana mfugaji mwenzetu akikamatiwa ng’ombe wake 10 atauza ng’ombe wake wawili apate Tsh. 1,000,000 ili akomboe ng’ombe wake. Ina maana akikamatiwa ng’ombe mara tano atabaki na fimbo na zizi bila ng’ombe, wote wataishia mikononi mwa Serikali ya CCM. Madiwani na Mbunge wa CCM hawana msaada kwa wafugaji wetu.
3. Wafanyabiashara wetu katika masoko ya Soko ya Kasusura, Soko la Stend ya wilaya, Soko jipya na wale wa Soko la Kabindi, Soko la Nyakanazi na Nemba wanadhulumiwa Tsh. 10,000 kila mwezi kwa kutozwa ushuru mkubwa zaidi ya ulioamriwa kulipwa. Mbunge wa CCM hana maumivu na hili.
4. Watumishi wenzangu, walimu, manesi, madaktari, maaskari, watumishi idara za Halmashauri wanaibiwa kiinua mgongo chao kupitia kikokotoo limbikizi cha 33% ambapo pamoja na kuchangia pesa zao wenyewe kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii lakini Serikali ya CCM inapofika muda wa watumishi wetu kustaafu inawawekea formula ngumu kuwalipa hela yao halali. Pesa ni ya kwao kwanini serikali itumie formula ngumu kuwalipa?
Kwa mfano rahisi ni hivi, ikiwa mtumishi amechangia michango ya Tsh. 10,000,000 katika muda wake wote wa Utumishi basi Serikali ya CCM inampa kwa mkupuo Tsh. 3,300,000 tu halafu 6,700,000 inabaki Serikalini. Hii si haki kwa kuwa hii pesa, Mstaafu akishalipa madeni yake, akalipia ada za watoto vyuoni hatobakiwi hata na pesa ya kufanya mradi wa kisasa wa ufugaji kuku. Ni uonevu huu kwa wapambanaji hawa wanaofanya kazi katika mazingira duni.
5. Serikali ya CCM imepandisha gharama za matibabu utafikiri ni huduma ya anasa. Hapa kwetu tukiugua tukaenda hospitali tunalipishwa pesa ya kufungua file la kutibiwa, tunalipia pesa ya kumuona daktari, tunalipishwa pesa ya vipimo maabara, tunalipishwa pesa ya kitanda tukilazwa na hata tunapokufa huwa tunalipia gharama za vifo vyetu Mortuary. Hutotoa mwili wa Ndugu yako aliyekufa hospitali mpaka mmelipana na Serikali ya CCM. CCM hawatuonei huruma hata tukiwa maiti, wanataka tulipie gharama ya kufa.
6. Nina ushahidi wa kuaminika wa ubadhirifu wa Tsh. 54,660,000 uliofanywa na Mbunge wa jimbo hili kwenye Halmashauri yetu. Wizi umekuwa unafanywa na Mbunge kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu wa Halmashauri yetu. Ninapoendelea na uchunnguzi ninapata harufu ya wizi wa zaidi ya Tsh. 400,000,000 kwenye Halmashauri hiihii.
CHADEMA tunashauri mambo yafuatayo ili kupanua wigo wa kiuchumi kwa wilaya yetu:
1. Kuchorwa upya kwa mipaka ya hifadhi ili wakulima na wafugaji wapatiwe maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli zao za kimaendelo. CHADEMA tunapendekeza eneo la hifadhi libaki 1800km².
2. Serikali iache kuwaibia wafugaji wetu kwa kuwatoza fine kubwa na rushwa pale inapokamata mifugo yao badala yake CHADEMA tunaishauri serikali ipime na kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ya Mifugo yao. Hii itasaidia kumaliza ugomvi kati ya wakulima na wafugaji unaoendelea kwenye Vijiji vyetu.
3. CHADEMA tunaisistiza Halmashauri kuzingatia Sheria ndogo za Ada na Ushuru za Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo zilizochapishwa katika gazeti la Serikali na- 162 la tarehe 13/06/2014. Kanuni zinaelekeza wafanyabiashara watozwe Tsh. 5,000 kama ushuru wa vibanda kwa mwezi na sio 15,000 mpaka 30,000 ilivyo sasa.
4. CHADEMA tunashauri Watumishi wastaafu walipwe 75% kwa mkupuo ya kiinua mgongo na 25% iliyobaki walipwe kama pensheni ya kila mwezi mpaka kufa kwao. CHADEMA tunashauri suala la maslahi ya watumishi wastaafu liandikwe kwenye KATIBA MPYA, tofauti na sasa ambapo linaamriwa na WANASIASA WALAFI.
5. Serikali izingatie kuwapatia matibabu bila malipo Wazee wetu, wajawazito na watoto kama Sera ya Afya ya 2007 inavyoelekeza.
6. Mbunge alipe pesa za Halmashauri ndani ya siku 21 kuanzia leo, wakishindwa, asije kusema Mjomba okansisila. Nitawaburuza mahakamani Mbunge na genge lake lote waliohusika na ubadbirifu huo.
Kwenye Uchaguzi wa mwaka 2020 hapa Biharamulo, CCM walituibia kura, hapa jimboni wakanipiga mimi na madiwani wangu wote kipigo cha Mbwa mwizi lakini kwenye Uchaguzi wa mwaka 2025 na Mimi nataka niwapige kipigo cha paka aliyekula dagaa wa mboga.
Huyu Mbunge wa sasa alitudanganya kuwa akipata Ubunge ataishi hapa lakini mpaka leo hajawahi kuishi hapa, anakuja Biharamulo shughuli ya mazishi ya Ndugu zake kwa kufikia kwa Mama yake. Wananchi wanahudumiwa na makatibu wake ambao wamezagaa kila mtaa.
Nawasihi wananchi wenzangu mjiandae kugombea nafasi za vitongoji, Vijiji na mitaa yetu hapo mwaka kesho 2024, hawa walioteuliwa kutuongoza wamekuwa wafanya biashara wa kugonga mihuri tu. Badala ya kutuongoza, wanatutongoza kutoa Rushwa ya kugongewa mihuri yao tu.
Kuna watu walinifanyia noma kwenye utawala wa awamu ya 5, nilipotangaza hadharani msimamo wa kupinga hifadhi yetu ya Burigi isichukuliwe kwenda Chato, walitumwa, wakaniwinda, wakanikamata, wakanilaza kwenye chumba kilichojaa maji, wakanichoma kwa spoku za moto, wakanipa kesi ya kuanzisha shule kinyemela na kulawiti wanafunzi wangu Dar es salaam,
Nilishawasamehe na ninawapenda. Na ninawakaribisha nyumbani mwangu pale Maendeleo tule mikate kwa Asali. Hiyo ipo kila siku.
NAWAAMBIA: Inye ntiniswa muyaga nkebhisenkele bye ngemu.
Ahsanteni wote kwa usikivu.
Recent Comments