MIAKA 60 YA MUUNGANO WA TANZANIA MSUGUANO WA MUUNDO

By Simamia Ngara Apr 27, 2024

NA, ANKO G

Katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania wilayani Ngara maadhimisho hayo yamepambwa na maonyesho ya vitu mbalimbali vya asili vinavyo patikana wilayani Ngara.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokea tarehe 26 Aprili 1964 ukawa mwanzo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hadi tarehe ile kulikuwa na mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa dola la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo kufikia mwaka huu wa 2024 ni Miaka 60 sasa imepita.

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar. Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi tarehe 26 Aprili 1964.

Tarehe 27 Aprili 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano.

Muundo wa Muungano wa Tanzania kama ulivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, una vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Zanzibar; na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashughulikia mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Visiwani.

Asilimia kubwa ya watanzania wa Tanzania bara na visiwani wanakukubali muungano uendelee kuwepo lakini wanakataa muundo uliopo ambao wengi wao wanaona kuwa kuna haja ya kubadilisha muundo huku wengine wakienda mbali zaidi na kutamani muungano usiwepo kutokana na muundo wa muungano huo.

Mapendekezo ya walio wengi kuhusiana na Muungano na muundo wake wanatamani muundo wa Serikali moja ambayo ni serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ama Serikali tatu kwa maana ya Jamhuri ya Tanganyika, Jamhuri ya Zanzibar pamoja na Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo itakua serikali mama.

Namalizia makala hii fupi kwa kuishauri serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kupitia mapendekezo ya wananchi ili kuboresha muungano huo na kuweka muundo ambao ni mzuri kwa ustawi wa taifa la Tanzania kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *